Na Malaki Philipo - Kishapu.
Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Kishapu mkoani
Shinyanga kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa kupinga vitendo vya ukatili
wa kijinsia wameadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia yakiongozwa na kauli mbiu 'Tupinge Ukatili wa Kijinsia, Mabadiliko yanaanza na mimi'.
Maadhimisho hayo yamefanyika leo Disemba 4,2020 kuanzia
majira ya saa mbili asubuhi ambapo Jeshi la polisi kupitia Dawati
la Jinsia na Watoto, wadau wa haki za binadamu na wanafunzi wa shule za msingi
na sekondari, wamekutana na kufanya maandamano kutoka eneo la mto Tungu hadi
shule ya sekondari ya Kishapu.
Wadau hao wamefanya maandamano ya amani kwa kupita
katika mitaa mbalimbali ndani ya halmashauri ya wilaya hiyo wakiwa na mabango
yenye jumbe tofauti za kuhamasisha kupinga ukatili wilaya ya Kishapu.
Maandamano hayo ni nyenzo mojawapo katika
maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, ambazo huadhimishwa
kila tarehe 25 ya mwezi Novemba hadi tarehe 10 ya mwezi Desemba
kila mwaka, siku zenye lengo la kuendelea kuhamasishana kupinga vitendo vya
unyanyasaji, ukandamizaji wa aina zote kati ya jinsi zote.
Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto wilayani Kishapu
Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la polisi Rose Mbwambo amesema maandamano hayo
yanaakisi umakini wa dawati hilo katika kutoa elimu ya haki na uwajibikaji ili
kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia na kwamba dawati hilo limekuwa
likifanya kazi kwa weledi ambapo kwa mwaka huu jumla ya wanaume tisa wamefungwa
kifungo cha miaka 30 kila mmoja.
“Ukitazama takwimu za kuanzia mwezi Januari mwaka huu
hadi mwezi Novemba tumepata taarifa 91 za ubakaji, na kati ya hizo taarifa watu
43 wamefikishwa mahakamani na tayari wanaume tisa wamefungwa miaka 30 kila
mmoja, changamoto iliyopo ni ufichwaji wa mashahidi na kufanya mapatano ya
kiamilia kumaliza kesi za namna hiyo lakini dawati linaendelea kuchukua hatua
za kisheriia kwa wanaobainika na makosa hayo” amesema Rose.
Miongoni mwa wadau walioshiriki maandamano hayo ni
shirika lisilo kuwa la kiserikali la REDESO, Benki ya NMB, Red Cross, TCRS,
pamoja na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu, ambao kwa pamoja
wamehimiza jamii kuacha ukatili kutokana na kusababisha madhara makubwa kiafya,
kiuchumi, kimwili na hata kisaikolojia na kusema kwamba vitendo hivyo vimekuwa
vikirudisha nyuma maendeleo hivyo basi jamii haina budi kuachana navyo.
Mkuu wa wilaya ya Kishapu Bi. Nyabaganga Talaba ambaye
aliyapokea maandamano hayo amesema msimamo wa serikali ni kuhakikisha hali ya
usawa, utulivu na amani katika kuvikabili vitendo vyote vinavyokiuka haki na
utu wa mtu, na kuitaka jamii kuacha imani za kishirikina, imani zinazowaweka
watoto kwenye hatari ya kubakwa na kundi la wazee katika hatari ya
mauaji.
“Wilaya ya Kishapu si kwamba imeharibiwa na mila na
desturi lakini uelewa wa baadhi ya wazazi kutambua mchango wa mtoto hasawa kike
kwenye maendeleo lakini imani za kishirikina zimekuwa mwiba unaowatia hofu ya
kubakwa kwa watoto ama kulawitiwa lakini pia wazee kuingiwa na hofu ya
kuuawa” amesema Talaba.
“Lakini serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa
maendeleo tutaendelea kutoa elimu ya kupinga ukatili na kuhakikisha tunachukua
hatua kali za kisheria kwa wale wanaoendelea na vitendo hivyo kwa sababu zao,
hatutawafumbia macho” ameongeza Talaba.
Maandamano ya dawati la jinsia na watoto wilaya ya Kishapu yametamatishwa na ugawaji wa taulo za kike, madaftari, kalamu pamoja na michezo mbalimbali ukiwemo mchezo wa mpira wa pete kati ya askari wa jeshi la polisi pamoja na wanafunzi wa shule ya sekondari ya Kishapu
.Dawati la Jinsia na Watoto,wadau na wanafunzi wakiwa kwenye maandamano wakati wa maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia wilayani Kishapu
Social Plugin