MWANAHARUSI AELEZA HALI YA UTAPIAMLO MKALI KWA WATOTO WILAYANI KISARAWE



Julieth Ngarabali , Kisarawe 
Mratibu wa lishe wilayani Kisarawe mkoani Pwani Mwanaharusi Issa amesema takwimu zinaonyesha kwamba watoto wenye umri wa miaka mitano wenye utapiamlo mkali katika Wilaya ya hiyo ni asilimia 0.7 huku wenye utapiamlo wa kadri ni asilimia 13.6.

Amesema kwa hali hiyo kundi hili pia linaingia kwenye uwezekano mkubwa wa kupata magonjwa ya milipuko kama wazazi wasipokuwa makini kuanzia uandaaji wa lishe , hata mama anapotaka kunyonyesha basi ahakikishe ziwa lake safi.

"Jumla ya watoto chini ya miaka mitano waliofanyiwa tathmini ya hali ya lishe ni 43,757 , matokeo utapiamlo mkali ni watoto 315 sawa na asilimia 0.7 na kadiri ni 5,942 sawa na asilimia 13.6.",amesema Mwanaharusi.

Mwanaharusi amesema ili kupunguza tatizo la utapiamlo lililopo ,wataalamu wa afya wanatakiwa kumuelekeza mama jinsi ya kumpakata mtoto na kumweka kwenye titi ipasavyo mara baada ya kujifungua.

"Pia kumuelekeza mama aliyejifungua jinsi ya kukamua maziwa yake ili mtoto aweze kupatiwa pindi anapokua mbali na ahakikishe yapo kwenye usafi unaotakiwa kuepusha mlipuko wa magonjwa mengine ikiwemo kuhara",ameeleza.

Naye Meneja wa mradi wa Chakula na Lishe kutoka shirika lisilo la kiserikali la Feed The Children Silvia Imalike amesema takwimu za utafiti wa hali ya Kidemografia na afya uliofanyika mwaka 2015 zinaonesha kuwa asilimia 59 ya watoto wenye umri wa miezi 0 hadi miezi 6 nchini wananyonyeshwa maziwa ya mama pekee.

"Hii inamanisha asilimia 41 ya watoto wenye umri huo hawanyonyeshwwi ipasavyo hivyo wapo kwenye hatari ya kupata utapiamlo na magonjwa yanayotokana na taratibu zisizofaa za ulishaji watoto", amesema Imalike.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post