Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Albert Msovela akitangaza matokeo ya wanafunzi waliohitimu elimu ya msingi mwaka 2020 na kutangaza majina ya wanafunzi waliofaulu na kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2021.
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Jumla ya wanafunzi 26,382 (wavulana 12,304 na wasichana 13,804) waliohitimu mtihani wa darasa la saba mwaka 2020 mkoani Shinyanga wamefaulu na kupangiwa shule kwa ajili kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza mwaka 2021.
Hayo yamesemwa leo Ijumaa Desemba 18,2020 na Katibu Tawala mkoa wa Shinyanga, Albert Msovela wakati wa kikao cha kutangaza matokeo ya wanafunzi waliohitimu elimu ya msingi mwaka 2020 na kutangaza majina ya wanafunzi waliofaulu na kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2021.
Msovela amebainisha kuwa jumla ya wanafunzi 234 (mvulana mmoja na wasichana 233) wamebaki watapangiwa shule kadri ujenzi wa madarasa utakavyokamilishwa ambapo mkoa umepanga kukamilisha ujenzi wa madarasa ifikapo Januari 28,2020 ambapo serikali imetoa agizo ujenzi wa madarasa kukamilika ifikapo Februari 28,2020 ili wanafunzi ambao hawajapangiwa shule waanze masomo.
Hata hivyo alisema hakuna mtoto hata mmoja aliyefaulu lazima aende shule ifikapo Januari 28,2021.
Akielezea kuhusu matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2020, Msovela amesema mkoa una jumla ya shule 603 zilizofanya mtihani ambapo wanafunzi waliosajiliwa kufanya mtihani walikuwa 33,767 kati yao wavulana ni 15,714 na wasichana 18,053.
“Waliofanya mtihani ni 33,435, wavulana 15,547 na wasichana 17,888 sawa na asilimia 99 ya wanafunzi wote waliosajiliwa”,alieleza Msovela.
Alieleza kuwa katika matokeo hayo, Manispaa ya Shinyanga imekuwa ya kwanza kimkoa huku ikishika nafasi ya 17 kitaifa, Halmashauri ya Kahama Mji ni ya pili na ya 84 kitaifa, Msalala ya tatu na ya 138 kitaifa, Kishapu ya nne na ya 140 kitaifa, Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga ya tano na ya 151 kitaifa, huku Ushetu ikishika mkia ngazi ya mkoa kwa kushika nafasi ya sita na ya 169 kitaifa.
Alisema hivi sasa mkoa wa Shinyanga unaendelea kufanya vizuri katika matokeo ya mitihani na kufanikiwa kuingia katika shule 10 bora kitaifa akiitaja shule ya Kwema Modern iliyoshika nafasi ya nne kitaifa ya kwanza kimkoa na Rocken Hill iliyoshika nafasi ya 10 kitaifa na ya pili kimkoa.
“Tumefanikiwa pia kupata wanafunzi walioingia 10 bora kitaifa ambao ni Huma Masala Huma (nafasi ya pili kitaifa), Andrea Elias Mabula (4), Emmanuel Kashindye Paul (7) na Emmanuel Peter Marwa (8) wote kutoka shule ya Kwema Modern iliyopo katika Halmashauri ya Kahama Mji”,alieleza Msovela.
Msovela alisema ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora ili waweze kutimiza ndoto zao hivyo ni lazima hatua kali za kisheria zichukuliwe kwa wale wote watakaowasababishia wanafunzi kukatiza masomo yao.
“Ni jukumu letu kuhakikisha tunaimarisha mbinu za usimamizi na uendeshaji wa elimu kwa maana ya kutumia rasilimali zilizopo ili mazingira ya kujifunza na kufundishia kuwa rafiki. Ni wajibu wa kila halmashauri kujenga vyumba vya madarasa,hosteli,maabara,nyumba za walimu, matundu ya vyoo na kununua samani za shule”,aliongeza Msovela.
Kwa upande wake Afisa Elimu Mkoa wa Shinyanga, Mohammed Kahundi alisema alisema jumla ya wanafunzi Waliochaguliwa kujiunga shule za bweni ni 108 (wavulana 66 na wasichana 42) na Wanafunzi 26,148 (wavulana 12,304, wasichanam13,844) wamechaguliwa kujiunga na shule za kutwa.
Aidha Kahundi aliipongeza Halmashauri ya wilaya ya Kishapu kwa kujenga shule kwa ajili ya wanafunzi wa kike 80 wenye ufaulu mzuri na kuziomba halmashauri zingine kujenga shule maalumu kwa ajili ya wasichana ili kupunguza mimba na ndoa za utotoni.
Wakitoa mapendekezo na kutoa ushauri namna ya kuboresha elimu na kumaliza changamoto, mmoja ya wadau waliohudhuria kikao hicho, Katibu Tawala Wilaya ya Kahama, Timoth Ndanya alishauri uandaliwe utaratibu wa kisheria, kesi zinapotokea za kukatisha masomo ya wanafunzi hususan wa kike ziwe na ukomo wa kuendeshwa ili zimalizike kwa wakati na hatma ya mwanafunzi ijulikane mapema.
Akichangia hoja hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba ameeleza kuwa katika kikao cha wadau wa kupinga ukatili wa kijinsia mkoa wa Shinyanga kilichofanyika Desemba 15, mwaka huu, kiliazimia kwamba kesi zote zinazofika mahakamani siku hiyo hiyo shahidi awepo na zianze kushughulikiwa (kusikilizwa) kabla ya pande zote hazijarudi nyumbani na kuanza kumalizana/ kuelewana.
Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Albert Msovela akitangaza matokeo ya wanafunzi waliohitimu elimu ya msingi mwaka 2020 na kutangaza majina ya wanafunzi waliofaulu na kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2021.
Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Albert Msovela akitangaza matokeo ya wanafunzi waliohitimu elimu ya msingi mwaka 2020 na kutangaza majina ya wanafunzi waliofaulu na kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2021.
Afisa Elimu Mkoa wa Shinyanga Mohammed Kahundi akizungumza wakati wa kikao cha kutangaza wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2021.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga ACP Bebora Magiligimba akizungumza wakati wa kikao cha kutangaza wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2021.
Wadau wa elimu wakiwa ukumbini.
Mkuu wa wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Talaba akizungumza wakati wa kikao cha kutangaza wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2021.
Mkuu wa wilaya ya Kahama , Anamringi Macha akizungumza wakati wa kikao cha kutangaza wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2021.
Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga , Albert Msovela akizungumza wakati wa kikao cha kutangaza wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2021.
Wadau wakiwa ukumbini.
Afisa Elimu Mkoa wa Shinyanga Mohammed Kahundi akizungumza wakati wa kikao cha kutangaza wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2021.
Wadau wa elimu wakiwa kwenye kikao
Wadau wa elimu mkoa wa Shinyanga wakiwa kwenye kikao cha kutangaza wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2021.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Soma pia
Tazama hapa Orodha ya Wanafunzi waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza Tanzania Bara kwa mwaka 2021.
CHAGUA MKOA ULIKOSOMA
Social Plugin