Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ATAKAYEUZA ARDHI ALIYOPEWA NA SERIKALI KUPOKONYWA NA KURUDISHWA SERIKALINI


Serikali imewatahadharisha Wananchi wa Kilosa Mkoani Morogoro kutouza ardhi watakayopewa  na Serikali baada ya kufutwa kwa baadhi ya mashamba  na kwamba atakayebainika kuiuza ardhi hiyo kwa matajiri atanyang’anywa na ardhi kurejeshwa serikalini.

Akizungumza na Wananchi wa eneo la Kimamba A na Magomeni Wilayani Kilosa Waziri wa Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia ni Mbunge wa Kilosa amesema ardhi itakayotolewa ni lazima itumike kwa kuzingatia mpango wa matumizi bora ya ardhi ili kuepuka migogoro ya mara kwa mara inayosababisha uhasama na vifo kati ya wakulima na wafugaji.

Amesema Serikali imepanga kufuta mashamba makubwa yanayomilikiwa na watu na makampuni,taasisi na watu binafsi bila kuyaendeleza ambapo takribani heka elfu tatu zinatarajiwa kufutwa na kugawiwa kwa wananchi ambao hawana ardhi Wilayani Kilosa na kuwasihi kuachana na hulka ya kuyauza mashamba hayo tena kwa matajiri na baadae kuililia Serikali kwa kukosa ardhi ya kilimo na ufugaji jambo ambalo linasababisha migogoro isiyoisha.

Prof. Kabudi amewasisitizia wananchi hao kuwa Serikali haina mpango wa kuyafuta mashamba yote ya mkonge Wilayani humo kutokana na ukweli kuwa thamani ya mkonge imeanza kuongezeka katika soko la dunia baada ya mifuko ya plastiki kuonekana ina athari kimazingira .


Amesema Mkoa wa Morogoro uko kimkakati kutokana na uwepo wa ardhi yenye rutuba ya kutosha na kuwataka Wananchi wa Kilosa kujipanga upya kufufua zao la Mkonge na Pamba kutokana na uwepo wa usafiri wa uhakika baada ya kukamilika kwa ujenzi wa reli mpya ya kisasa ambayo itatumika kuyasafirisha mazao hayo kwenda bandarini na baadae katika soko la dunia.

Ameongeza kuwa katika Mashamba yatakayofutwa pia ni lazima kutengwe maeneo ya uwekezaji ambayo yatatumiwa kwa uwekezaji na ujenzi wa viwanda mbalimbali vya kuchakata mazao mbalimbali ikiwemo mbogamboga,mkonge na Pamba jambo litakalosaidia kuongeza thamani ya mazao hayo na hivyo kuongeza ajira na kipato.

Baadhi ya wananchi Wilayani Kilosa wameishukuru Serikali kwa kusikia kilio cha cha ukosefu wa ardhi kutokana na kukodi mashamba kwa shilingi elfu 50 kwa heka moja au kulipa mazao wakati wa mavuno jambo ambalo linawafanya kuendelea kuwa watumwa na kutoona faida ya kilimo…



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com