Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BASI LA FRESTER LAUA NA KUJERUHI KAHAMA BAADA YA KUKAGULIWA NA POLISI.... 'DREVA ALIJIDUNGUA SPEED KALI'

Na Salvatory Ntandu - Malunde 1 blog Kahama
Mtoto mmoja ambaye hajafahamika jina wala makazi yake mwenye umri unaokadiriwa kuwa ni miaka 7 amefariki dunia na watu wengine 23 kujeruhiwa katika ajali ya basi la Kampuni ya Frester lenye namba za usajili namba T 965 DST likitoka Kahama mkoani Shinyanga kwenda Musoma mkoani Mara kupinduka katika eneo la Phantom/Nyakato Mjini Kahama.

Ajali hiyo imetokea leo Alhamis Desemba 17,2020 majira ya saa 12:00 asubuhi muda mfupi baada ya Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini Wilbroad Mtafungwa kulikagua basi hilo na kuliruhusu kuendelea na safari.

Kamanda Mutafungwa amesema basi hilo lilipofika katika eneo la Nyakato nje kidogo ya mji wa Kahama lilipinduka kutokana na mwendokasi bila ya kuchukua tahadhari kwa watumiaji wengine wa barabara.

Kamanda Mutafungwa amesema kabla ya kuanza Safari kwa mabasi yote yaendayo mikoani leo alikutana na madereva hao na kuwakumbusha kuhusiana na kuzingatia sheria za Usalama barabarani ikiwa ni pamoja na kutoendesha kwa mwendo kasi na kuzingatia alama za barabarani.

“Dereva huyu ni mzembe haiwezekani upatiwe elimu ya Usalama barabarani halafu muda huo huo ukiuke sheria na kusababisha ajali kwa uzembe ambayo imesababisha ajali kwa watu zaidi ya 23 na kusababisha kifo cha mtoto mmoja,tutachukua hatua kali dhidi yake pindi atakapokamatwa baada ya kukimbia kufuatia ajali hiyo”,amesema Mtafungwa.

Ameongeza kuwa basi hilo lilikuwa na abiria 47 ambapo 23 wamejeruhiwa watatu hali zao sio nzuri huku wengine wakiruhusiwa kuendelea na safari baaada ya kupata michubuko ambapo kampuni hiyo ililazimika kuwatafutia usafiri mwingine na kuendelea na safari yao ya kuelekea Musoma mkoani Mara.

Mmoja wa Majeruhi wa ajali hiyo, Kasiani Msaki amesema kuwa dereva wa basi hilo alikuwa anaendesha kwa mwendokasi ambapo alipofika eneo la tukio alishindwa kulimudu gari hilo wakati akilikwepa gari dogo lililokuwa mbele yake ndipo lililopoteleza na kuingia mtaroni na kupinduka.

“Dereva wa basi hili alikuwa anafanya mashindano na mabasi mengine ,tunaiomba serikali ichukue hatua kali dhidi yake,amesababisha kifo na ulemavu kwa watu bila sababu ya msingi kwa kushindwa kuchukua tahadhari licha ya kupatiwa elimu na maafisa wa Usalama barabarani,”amesema Msaki.

Mkuu wa wilaya ya Kahama Anamringi Macha amezitaka mamlaka zinazosimamia Usalama barabarani kuhakikisha wanachukua hatua kali za kisheria kwa madereva ambao ni wazembe kwa kufungia leseni zao ili waweze kujifunza umuhimu wa kuzingatia sheria za usalama barabarani.

“Haiwezekani tuendelee kuwavumilia madereva wa mabasi wanaoendelea kufanya mashindano barabarani huku wakiwa na abiria,tutatuchua hatua kali kwao ili kudhibiti ajali zinasababisha vifo kwa watu wasiokuwa na sababu na kupunguza nguvu kazi ya taifa,”amesema Macha. 
Basi la Frester likiwa limepinduka
Basi la Frester likiwa limepinduka

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com