Na Geofrey Kazaula, Katavi.
Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), kupitia mradi wake wa Uimarishaji wa Halmashauri za Miji – Urban Local Goverement Strengthening Program (ULGSP), umetumia shilingi billioni 7.4 kutekeleza mradi wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami katika Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda zenye urefu wa Km 7.7 ili kuwezesha wananchi kusafiri kwa urahisi.
Hayo yameelezwa na Kaimu Mratibu wa TARURA Mkoa wa Katavi Mhandisi Henry Mtawa wakati wa ukaguzi wa miradi mbalimbali iliyotekelezwa katika Mkoa huo tangu kuanzishwa kwa TARURA.
“Ujenzi huu wa barabara ulianza mwaka 2017 na kukamilika mwaka 2019 na umesaidia kuboresha mandhari ya Mji kama unavyoona hata kipindi cha usiku wananchi wanaendelea na kazi zao kutokana na taa zilizopo”, amesema Mhandisi Henry Mtawa.
Mhandisi huyo ameongeza kuwa, kutokana na mradi huo wakazi wa Halamashauri ya Manispaa ya Mpanda wameondolewa kero ya muda mrefu ya mafuriko katikati ya mji hasa kipindi cha masika, na kupitia mradi huu maji yameweza kutengenezewa njia na sasa hakuna tena mafuriko kwa wananchi.
Naye, Ndg. Juma Phinias mkazi wa mtaa wa Nsemulwa ameeleza kuwa kipindi cha nyuma kabla ya barabara hizo za lami kulikuwa na vumbi kali kipindi cha kiangazi huku kukiwa na matope kipindi cha masika lakini kwa sasa wananchi wananufaika na mradi huo na hasa hasa wanafanya biashara zao bila usumbufu tofauti na hapo awali.
“Tunaishukuru sana Serikali kwa ujenzi wa barabara hii, kwa sasa tunafanya shughuli zetu katika kipindi chote cha mwaka pamoja na biashara ndogo ndogo zinaendelea kufanyika ata usiku”. alisema Juma.
Aidha, licha ya ujenzi wa barabara hizo, TARURA katika Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda imefanikisha ujenzi wa daraja katika barabara ya Mkumbo inayounganisha kata ya Nsemula pamoja na Kashaulili lililogharimu shilingi milioni 163 na kutatua kero za kudumu kwa wakazi wa kata hizo mbili hususani kwa kipindi cha masika.
Akizungumzia uwepo wa daraja hilo mkazi wa eneo la Mtaa wa mnazi mmoja, Kata ya uwanja wa ndege katika Halamshauri ya Manispaa ya Mpanda Ndg. Nasir Mikidadi amesema hapo awali kulikuwa na daraja dogo ambalo lilikuwa kero kwa wakazi wa mitaa hiyo katika kipindi cha mvua kwani maji yalikuwa yanapita juu ya daraja na kusaabisha kukwama kwa shughuli zao pamoja na watoto kushindwa kufika shuleni, ameongeza kuwa uwepo wa daraja hilo la kudumu ni utatuzi tosha wa kero ya muda mrefu.
Wakala wa barabara za Vijijini na Mijini TARURA Mkoa wa Katavi unaendelea kuhudumia mtandao wa barabara katika Halmashauri zote tano zenye urefu wa km 2475.82 pamoja na ujenzi wa madaraja lengo likiwa ni kuwawezesha wananchi kupata huduma ya usafiri na usafirishaji pamoja na kuwezesha barabara na vivuko vyote kupitika katika kipindi chote cha mwaka.
Social Plugin