Na Prisca Ulomi, WMTH
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile amehimiza taasisi za Serikali kutumia Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data (NIDC) kuhifadhi taarifa zao kwa kuwa ni sehemu salama, ina miundombinu na mifumo ya TEHAMA ya kisasa na ina wataalamu wabobezi na ina nafasi ya kutosha kwa ajili ya kupangisha mifumo.
Dkt. Ndugulile ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya kutembelea NIDC, Dar es Salaam ambapo aliambatana na Naibu Waziri wake, Mhandisi Kundo A. Mathew, Katibu Mkuu, Dkt. Zainabu Chaula, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Waziri Kindamba na watendaji wa Wizara hiyo na kubaini kuwa ni taasisi 84 tu za Serikali zinatumia NIDC kati ya taasisi 149 zinazohifadhi taarifa zake kwenye kituo hicho.
Amezikumbusha taasisi za Serikali kuzingatia agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alilolitoa alipotembelea NIDC kuzindua Mfumo wa Kielektroniki wa Kukusanya Mapato (electronic Revenue Collection System - eRCS) mwaka 2017 ambapo umeiwezesha NIDC kuongeza makusanyo ya mapato yake kutoka shilingi bilioni 1.4 mwaka 2019 na kufikia shilingi bilioni 2.76 mwaka 2020
Naye Naibu Waziri, Mhandisi Kundo A. Mathew ameipongeza NIDC kwa kutengeneza mifumo mbali mbali ya TEHAMA ambayo inaiwezesha Serikali kuongeza makusanyo ya mapato na kurahisisha maisha kuendana na mahitaji ya wananchi ikiwemo kulipa tiketi ya mabasi ya njia ya mtandao; kuweka mafuta kwenye gari; kulipa kiingilio kwenye uwanja wa mpira wa Benjamin Mkapa; usafiri wa kivuko cha Kigamboni; usajili wa leseni BRELA; na maegesho ya magari uwanja wa ndege wa Dar es Salaam
Katibu Mkuu, Dkt. Zainab Chaula amewaeleza watendaji wa NIDC washirikiane kwa karibu na wataalamu wa Wizarani ili kuhakikisha kuwa Serikali inaendelea kuwahudumia wananchi kwa kutumia TEHAMA ili kuokoa muda wao kutafuta huduma za Serikali badala yake watumie kufanya kazi na kuongeza uzalishaji mali
Meneja wa NIDC, Geofrey Mpangala amesema kuwa wateja wanaotumia kituo hicho wamepunguza gharama za uendeshaji na uwekezaji kwenye taasisi zao kwa kuwa hawajengi miundombinu na mifumo ya TEHAMA; wateja wanapata viwango vya juu vya data yenye kasi na uhakika wa usalama wa data zao na huduma zinatolewa kituni hapo kwa saa 24.
Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba amemshukuru Dkt. Ndugulile kwa ziara yake kwa kuwa imeongeza ari na shauku ya utendaji kazi kwa wataalamu wa NIDC ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya wateja na mifumo ya TEHAMA ili kurahisisha huduma kwa wananchi
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
Social Plugin