DKT. NDUGULILE AIPA SIKU 90 SHIRIKA LA POSTA KUBORESHA UTENDAJI NA UFANISI WAKE


Na Prisca Ulomi, WMTH
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile ameipa siku 90 Shirika la Posta Tanzania (TPC) kuboresha utendaji kazi na ufanisi katika kuhudumia wateja na wananchi kwa ujumla katika shughuli za kila siku za uendeshaji wa Shirika hilo

Dkt.Ndugulile ameyasema hayo kwa Bodi, Menejimenti na wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania wakati wa ziara yake ya kutembelea Shirika hilo, Dar es Salaam ambapo aliambatana na Naibu Waziri wake, Mhandisi Kundo A. Mathew, Katibu Mkuu, Dkt. Zainab Chaula na Menejimenti ya Wizara hiyo kwa lengo la kufahamu utendaji kazi wa Shirika ili kuhakikisha kuwa linahudumia vema wananchi

Ameongeza kuwa TPC ipitie mikataba yake ambayo haina maslahi kwa Shirika na isimamie vizuri rasilimali zake ikiwemo viwanja, ofisi na magari kwa kuwa rasilimali ni mtaji na mtaji sio fedha ili rasilimali hizo zitumike kuongeza mapato ya Shirika

Vile vile ameiagiza  Wizara yake kushirikiana na TPC kufanya mapitio ya sera na sheria ya posta ili ziweke kuendana na wakati kuendana na mabadiliko ya teknolojia duniani ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi

Pia, amewakumbusha kuwa na mahusiano mazuri baina ya viongozi, wafanyakazi, menejimenti na wajumbe wa bodi katika mazingira ya mahali pa kazi ili kuboresha na kuongeza utendaji kazi wa Shirika

Naye Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhandisi Kundo A. Mathew amelipongeza TPC kwa kutengeneza Mfumo wa Taarifa wa Posta ambao unasimamia na kufuatilia uendeshaji wa Shirika; malipo na ukusanyaji wa mapato; na taarifa za watumishi

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula, ameueleza uongozi wa TPC kuwa Wizara itaendelea kushirikiana nao ili kufanikisha utendaji kazi wa Shirika katika kuhudumia wateja

Mwenyekiti wa Bodi wa TPC, Kanali mstaafu, Dkt. Haruni Kondo na Posta Masta Mkuu wake, Hassan Mwang’ombe wamemshukuru Dkt. Ndugulile kwa ziara yake na kulitaka Shirika liboreshe utendaji kazi wake na wako tayari kufanyia kazi yaliyoelekezwa


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post