Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ELIMU YA LISHE BORA YAKOMESHA MILA POTOFU SINGIDA


Mlo wa maini ambayo awali yalizuiliwa kuliwa na watoto wa kike na wanawake


Na Abby Nkungu, Singida

MKOA wa Singida umeanza  kutoa  elimu kwa jamii juu ya uandaaji wa lishe bora na kupiga  vita mila potofu zinazozuia wajawazito kutumia baadhi ya vyakula vyenye virutubisho muhimu kiafya na kusaidia kuzuia matatizo ya utapiamlo, uzito pungufu na udumavu kwa watoto.

Ofisa lishe wa Mkoa wa Singida, Teda Sinde alisema kuwa uamuzi huo umefikiwa baada ya kubaini kuwa bado kuna  mila potofu juu ya masuala ya lishe katika baadhi ya makabila; hivyo kuchangia kuwepo utapiamlo kwa watoto walio chini ya miaka mitano kutokana lishe duni.

Kutokana na hali hiyo, alisema katika Mpango kazi wao wameanza kutoa elimu kwa jamii; hasa vijijini, juu ya umuhimu wa lishe bora na utumiaji kikamilifu wa vyakula vya asili vilivyopo  maeneo yao kwa ajili ya lishe  ya mama na mtoto katika kupunguza utapiamlo, udumavu na uzito pungufu

Hatua hiyo imekuja miezi michache baada ya wadau kueleza kuwa kuendelezwa kwa baadhi ya mila potofu juu ya lishe katika baadhi ya makabila mkoani Singida ni moja ya sababu ya watoto walio chini ya miaka mitano kukumbwa na utapiamlo kutokana na wazazi wao kutopata mlo kamili.

 

Ilielezwa kuwa jamii ya kabila la Wanyaturu, ambalo ndilo kabila kuu mkoani Singida, bado ina changamoto kubwa ya elimu juu ya umuhimu wa lishe bora kwa mama mjamzito na anayenyonyesha kutokana na kuzuia baadhi ya  vyakula  kuliwa na kundi hilo ili kutii matakwa ya kimila.

 

Mzee Patrick Mdachi ambaye ni Ofisa Maendeleo ya Jamii mstaafu na Mtafiti wa masuala ya mila anasema kuwa kulingana na mila na desturi za kabila la Wanyaturu ilikuwa ni mwiko kwa mjamzito kula mayai kwa imani kuwa mtoto atakayezaliwa hataota kamwe nywele kichwani.

 

Alitaja vyakula vingine zilivyozuiwa na Wazee wa mila kuwa ni  pamoja na utumbo mwembamba wakidai ndoa itayumba, maini kwa madai kuwa mtoto tumboni anatakuwa mnene na kuwa na uzito mkubwa hivyo kusababisha upasuaji wakati wa kujifungua huku utumbo wa ‘daftari’ ukiaminika kuleta mabaka kichwani kwa mtoto.

 

Hata hivyo, Mdachi anakiri kuwa mila hiyo potofu imeanza kutoweka hivi sasa baada ya wataalamu wa lishe kuanza  kutoa elimu jamii; hasa vijijini, juu ya kuzingatia makundi yote  matano muhimu ya vyakula kwa kila mlo ili kudumisha  afya ya mama na  mtoto baada ya kuzaliwa.

 

“Sijafanya uchunguzi au utafiti wa kina wa kitaalamu, lakini katika pita-pita yangu vijijini kukusanya data na kuongea na wananchi hasa wazee wa mila, inaonesha dhahiri wameanza kuzingatia elimu ya lishe na kuacha mila potofu” alisema Mdachi na kuongeza kuwa hali hii imechangiwa na  elimu ya wataalamu wa lishe.

 

Naye, Mzee Ramadhani Kijida (78) mkazi  wa Kijiji cha Nkuninkana wilaya ya Ikungi alisema kuwa ni kweli baadhi ya vyakula vilizuiwa kwa akinamama na wajawazito ili  kulinda afya zao  lakini baada ya  kupatiwa elimu na ustaarabu kuingia wengi wa wananchi wameanza kula vyakula vyote vinavyokubalika kiafya.

 

“Wakati huo sisi tuliamini mila zetu na kwa hakika zilikuwa zinatusaidia ndio maana vifo vya  wajawazito  vilikuwa adimu na kujifungua kwa upasuaji hakukuwepo, lakini baada ya elimu na  kuona hali halisi ya sasa wengi wetu tumeanza kubadilika na kuruhusu wale  vyakula vyote” alieleza Mzee Kijida.

 

Takwimu za Utafiti wa Kitaifa juu ya hali ya lishe mkoani Singida kwa mwaka juzi (TNNS2018)  zinaonesha asilimia 29.8 ya watoto chini ya umri wa miaka mitano wana tatizo la udumavu, asilimia 5 ukondefu na asilimia 15 wana  uzito mdogo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com