Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

JESHI LA POLISI SHINYANGA LAONYA WAHALIFU SIKUKUU ZA KRISMASI NA MWAKA MPYA......"ULEVI BARABARANI, DISKO TOTO, KUJAZA UKUMBI MARUFUKU"

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba akizungumza na waandishi wa habari

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limewataka wananchi kusherehekea Sikukuu ya Krismasi ambayo huadhimishwa kila ikifikapo Desemba 25 kila mwaka na Mwaka Mpya 2021 kwa amani na utulivu mkubwa bila kujihusisha na vitendo vya uhalifu ama vitendo vingine vyenye viashiria vyovyote vya uvunjifu wa sheria.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa salamu za Krismas na Mwaka mpya 2021,Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba amesema ni vyema wananchi wakachukua tahadhari kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kuhakikisha vitendo vyote vya uhalifu na wahalifu katika maeneo mbalimbali vinathibitiwa mapema iwezekanavyo endapo vitajitokeza.

"Wananchi waendelee kushirikiana na jeshi la polisi kwa kutoa taarifa mapema pale wanapowatilia mashaka watu wasiowafahamu au wanaowafahamu kuwa ni wahalifu pindi watakapowabaini katika maeneo yao ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa haraka kabla madhara hayajatokea",amesema Kamanda Magiligimba.

Hata hivyo Kamanda Magiligimba amesema jeshi la polisi limejipanga kikamilifu kuhakikisha wananchi wote wanasherehekea kwa amani na utulivu kwani ulinzi umeimarishwa maeneo yote ya Ibada, sehemu za kumbi za starehe na burudani na maeneo yote ya wazi yatakayokuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu.

Aidha amewatahadharisha watumiaji wote wa barabara kuwa makini kwa kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani ikiwa ni pamoja na madereva kutoendesha vyombo vya moto kwa mwendokasi na kuendesha wakiwa wametumia vilevi.

Kamanda Magiligimba pia amewataka wamiliki wa kumbi za starehe kuhakikisha wanazingatia uhalali wa matumizi ya kumbi zao katika uingizaji  wa watu, umri unaostahili na zaidi kujali uwezo wa  ukumbi husika.

"Tabia za kimazoea zikiwemo zile za kuendekeza tamaa za fedha na kujaza watu ukumbini kupita kiasi pamoja na disco toto ni marufuku. Vitendo hivi havitavumiliwa kamwe na yeyote atakayethubutu kufanya hivyo basi hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake kwa mujibu wa sheria",amesema Kamanda Magiligimba.

 Kamanda Magiligimba amewaasa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuendelea kuwa makini zaidi na uangalizi wa watoto wao, watoto wa majirani na watoto wa jamii kwa ujumla waepuke kuwaacha wakitembea peke yao au kuzurura barabarani na maeneo mengine ili kuepuka ajali na maafa au matukio mengine.

"Wananchi watakaolazimika kutoka katika makazi yao kwenda katika ibada, sehemu za starehe na maeneo mbalimbali wahakikishe kuwa hawaachi nyumba,makazi yao wazi au pasipo uangalizi",ameeleza Kamanda Magiligimba.

"Napenda kutumia fursa hii muhimu kuwatakia wananchi wote wa mkoa wa Shinyanga kila la heri katika Sikukuu ya Krismasi na Mwaka mpya 2021 kwa kuhakikisha kuwa Jeshi la Polisi linatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni zilizowekwa pamoja na miongozo inayotolewa mara kwa mara, hivyo halitawajibika kumuonea muhali,huruma ama upendeleo mtu yeyote atakayekwenda kinyume cha sheria",amesema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com