Madiwani Wanne Meatu Walalamikia Kukamatwa Bila Kuelezwa Kosa.


Samirah Yusuph
Meatu. Madiwani wanne wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika halmashauri ya Meatu Mkoani Simiyu wamesikitishwa na kitendo cha kukamatwa na jeshi la polisi kisha kuwekwa mahabusu bila kuelezwa kosa walilofanya.

 Tukio la kukamatwa madiwani hao limetokea Novemba 30,2020  ikiwa ni siku moja kabla ya kufanyika uchaguzi wa kumchagua mwenyekiti wa halmashauri hiyo,ambapo miongoni mwa waliokamatwa yumo Masumbuko Pesa diwani wa Kata ya Mbugayabanh'ya ambaye alikuwa anagombea nafasi ya mwenyekiti wa halmashauri ya Meatu.

Akizungumza na mtandao huu, Masumbuko Pesa ambaye pia alikuwa miongoni mwa wagombea watatu wa nafasi ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Meatu,alibainisha kuwa hajui ni kosa gani lililosababisha wakamatwe licha ya kuachiwa kwa dhamana na kwenda kushiriki uchaguzi uliofanyika jana wilayani humo.

Madiwani hao walikamatwa majira ya saa 5 usiku katika Kata ya Mwandoya ambapo ni makao makuu ya Jimbo la Kisesa wakati wakipata chakula kwenye moja ya mgahawa,ambao ni Emmanuel Sayi diwani wa Kata ya Mwamanongu, Juma Mpina Kata  ya Lubiga na Njile Ng'waka  Kata ya Mwabuma .

“Tumeomba kuelezwa kosa la kutukamata ni lipi lakini mpaka leo tunavyoongea hatujui kosa ni nini kwa kweli kitendo hicho kimetusikitisha sana kwani huo ni udharirishaji  ukizingatia sisi ni viongozi tulikuwa katika Kata ya Mwandoya kwa majukumu ya kikazi”alisema Pesa.

Alisema jeshi la polisi walichokifanya ni kinyume na taratibu za kazi zao kwani kutoelezwa kosa pindi unapokamatwa ni kinyume na taratibu,na matokeo yake wanapelekwa mahabusu ambapo baada ya kuwahoji walidai wanahisiwa kutoa rushwa.

 Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilayani Meatu Mkoa wa Simiyu Charles Mazuri  alipoulizwa juu ya madiwani wake wanne kukamatwa alikiri  kupokea taarifa hiyo na kueleza kuwa huwenda walihusishwa na vitendo vya rushwa.

 “ Tulikuwa na zoezi muhimu la uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri yetu,baada ya kupokea taarifa za kukamatwa  kwa madiwani wetu tulifuatilia na kukuta kweli,tulienda kuomba  wadhaminiwe ili waweze kushiriki uchaguzi,” alisema Mazuri.

Katibu alisema baada ya kufuatilia walielezwa kuwa kukamatwa kwao kunahusiana na masuala ya kutoa rushwa kutokana na kuwepo madai ya kuonekana na kundi la watu ambao inahisiwa huenda walikuwa na dhamira ya kuwapatia rushwa.

Kamanda wa Jeshi la polisi  Mkoa wa Simiyu Richard Abwao amesema hana taarifa ya  madiwani kukamatwa na polisi Meatu na kuahidi kufuatilia,ili kufahamu kama kweli wamekamatwa na ni kosa gani walilofanya.

Mwisho.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post