WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema uimarishaji wa huduma za tiba ikiwemo matumizi ya dawa za kufubaza virusi vya ukimwi (ARVs) umechangia kupunguza vifo vitokanavyo na UKIMWI kutoka vifo vya watu 85,000 mwaka 2001 hadi kufikia vifo 21,529 mwaka 2019.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumanne, Desemba Mosi, 2020) katika maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani yaliyofanyika Kitaifa katika uwanja wa Mandela Manispaa ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro. Kaulimbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu ni ‘Mshikamano wa Kimataifa, Tuwajibike Pamoja.’
Waziri Mkuu amesema mbali na kupungua kwa vifo hivyo, pia maambukizi mapya ya UKIMWI nayo yamezidi kupungua kutoka watu 130,000 mwaka 2001 hadi kufikia watu 68,484 mwaka 2019, hivyo ametoa wito kwa wadau wote katika mapambano ya ugonjwa huo waongeze jitihada.
“Mafanikio yote haya yametokana na kuendelea kuimarika kwa huduma za tiba ikiwemo matumizi ya dawa za kufubaza VVU (ARVs) na afua za kinga zinazohusisha tohara ya kitabibu kwa wanaume na kuzuia maambukizo ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.”
Amesema Tanzania imefanikiwa kufikia malengo ya tisini tatu (90:90:90) hasa katika 90 ya pili na ya tatu. “Kwa kujikumbusha tu, ni kwamba tisini tatu zinalenga kuhakikisha kuwa asilimia 90 ya WAVIU wanajua hali zao; asilimia 90 ya wanaojua hali zao wanaanza kutumia dawa za kufubaza mapema na asilimia 90 ya walioanza dawa za kufubaza VVU kinga zao za mwili zinaimarika ifikapo mwaka 2023.”
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa wadau mbalimbali wa masuala ya mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI, waongeze jitihada hususani katika kuhamasisha upimaji wa VVU ili wafikie lengo la 90 ya kwanza.
Hata hivyo, Waziri Mkuu ametoa siku 30 kwa kila mkoa uliowahi kufanya maadhimisho hayo uhakikishe kuwa unawasilisha taarifa yake Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania ndani ya mwezi mmoja kuanzia leo (Jumanne, Desemba Mosi, 2020).
Vilevile, Waziri Mkuu ametoa agizo kwa TACAIDS, Wizara ya Afya na wadau wote wa kudhibiti VVU na UKIMWI nchini, wajipange vizuri kubaini na kufanyia kazi maeneo mbalimbali ya uwekezaji yenye gharama nafuu katika kudhibiti VVU/UKIMWI lakini yatakayoleta matokeo makubwa.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewasihi vijana wajitambue na kuthamini maisha yao kwa kujikinga na maambukizi mapya ya VVU kwa kuwa wao ni nguvu kazi na Taifa linawategemea. “Na wale wanaoishi na VVU waendelee kutumia dawa za ARV kwa ufuasi sahihi bila kuacha ili waweze kufubaza VVU na kuimarisha afya zao.”
“Vijana ni kundi linalokabiliwa sana na changamoto ya maambukizi mapya ya VVU nchini. Takwimu za maambukizi mapya ya VVU zinaonesha kwamba asilimia 40 ya maambukizi hutokea kwa vijana na katika hao asilimia 80 ni vijana wa kike.”
Amesema kwa mujibu wa takwimu hizo, ni dhahiri kuwa kundi la vijana, na hasa wa kike, lipo kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata maambukizi mapya kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuanza ngono katika umri mdogo.
“Hali hii husababisha mhusika kuwa na mahusiano ya mapenzi na watu wengi hadi anapofikia utu uzima, hivyo, kujiweka katika hatari ya kupata maambukizi ya VVU. Nawaasa vijana, msijihusishe na mapenzi katika umri mdogo. Ili vijana muweze kutimiza ndoto au malengo yenu katika maisha; ni lazima muwe na subira.”
Waziri Mkuu amesema sababu nyingine ya vijana hao wadogo wa kike kuwa na mahusiano ya kingono na wanaume wenye umri mkubwa ni kuvutika na vishawishi kama vile pesa na zawadi ndogondogo. “Kwa mara nyingine, natoa rai kwa wanaume wenye umri mkubwa kuachana na tabia ya kujihusisha na mapenzi na wasichana wadogo. Niwakumbushe tena, Serikali haitasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa yeyote atakayebainika.”
Mapema, mara baada ya kuwasili kwenye eneo hilo, Waziri Mkuu alitembelea baadhi ya mabanda ya maonesho, ambapo kupitia mabanda hayo, amejionea utoaji wa huduma za elimu, uhamasishaji na upimaji wa Virusi vya UKIMWI (VVU) na magonjwa mengine yasioambukiza. Amesema amevutiwa na huduma zinazotolewa kwenye mabanda hayo.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dkt. Anna Mghwira alisema kiwango cha maambukizi ya UKIMWI katika mkoa wa Kilimanjaro kimeendelea kupungua kutoka asilimia 7.3 mwaka 2004 hadi kufikia asilimia 2.6 mwaka 2017. “Kiwango hiki kipo chini ya wastani wa maambukizi Kitaifa ambacho ni asilimia 4.8.”
“Hata hivyo kiwango cha maambukizi kimkoa kuwa chini ya wastani wa Kitaifa haimaanishi kuwa tuko salama; hivyo sote tunapaswa kuongeza juhudi za pamoja ili tufikie lengo la maambukizi sifuri ifikapo 2030.”
Alisema licha ya mafanikio hayo, pia wanakabiliwa na changamoto kubwa ya utoaji huduma ya tiba na mafunzo kwa baadhi ya WAVIU kutokuwa na ufuasi mzuri wa dawa pindi hali zao kiafya zinapoonekana kuimarika, hivyo aliwataka watu walioanza kutumia ARV, wazingatie ufuasi wa dawa.
Kwa upande wake, Balozi wa Marekani nchini, Dkt. Donald Wright aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa jitihada zake za kupambana na UKIMWI ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa watu wote wanaoishi na virusi hivyo wanapata dawa, na kuahidi kuwa Serikali yake itaendelea kushirikiana na Tanzania.
Awali, Mwenyekiti wa Baraza la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (NACOPHA), Bibi Leticia Mourice alitumia fursa hiyo kuiomba Serikali, asasi za kiraia, taasisi za dini na vyombo vya habari viendelea kutoa elimu ya makuzi, kubadili tabia na hofu ya Mwenyezi Mungu kwa vijana, wazazi na walezi ili kuwaepusha na matendo hatarishi.
“Hatua kali zichukuliwe dhidi ya ukandamizaji na udhalilishaji wa aina yoyote ya haki kwa watoto na vijana. Pia, viongozi wa dini, kwa kuzingatia misingi ya imani zetu, tushikamane kuelimishana na kuongoza jamii ya waumini kupiga vita unyanyapaa dhidi ya VVU.”