NDAHANI APONGEZA UFANISI VETA SINGIDA...AWAFUNDA WAHITIMU

 

Kaimu Afisa Vijana Mkoa wa Singida ambaye ni mgeni rasmi wa Mahafali ya 31 VETA-Singida, Frederick Ndahani akihutubia sherehe za mahafali hayo juzi.

Wahitimu wakijiandaa kuingia ukumbini.

Wazazi na baadhi ya walimu wakishiriki sherehe hizo.
Wazazi na baadhi ya walimu wakishiriki sherehe hizo.
Wanachuo wa VETA Singida-wakifuatilia matukio ya sherehe hizo.

Baadhi ya wahitimu wakiwa kwenye picha ya pamoja.

Sherehe zikiendelea ndani ya ukumbi.


Baadhi ya wahitimu wakiwa kwenye picha ya pamoja.

Mkuu wa Chuo cha Veta-Singida, Paul Batoleki akimpongeza mmoja wa wahitimu.

Ndahani akikabidhi vyeti kwa wahitimu.

Mgeni rasmi akiwa kwenye karakana ya Ufundi Bomba.

Mratibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Singida (Singida Press), Domician Mwalusito (kulia) na Katibu wa chama hicho Revocatus Gervas wakiwa na mmoja wa wahitimu kwenye mahafali hayo.


Na Godwin Myovela, Singida

KAIMU Afisa Vijana mkoani hapa Frederick Ndahani amepongeza umahiri wa mafunzo na mifumo ya kiteknolojia inayotumika kutoa mafunzo ya nadharia na vitendo kwa vyuo vya VETA nchini, huku akiwataka wahitimu wake kutumia stadi za mafunzo hayo katika kulifikisha Taifa kwenye uchumi wa juu.

Ndahani alitoa pongezi hizo jana wakati akihutubia Sherehe za Mahafali ya 31 ya kuhitimu Mafunzo ya Ufundi Stadi VETA Singida.

"Tafsiri ya kuhitimu kwenu leo maana yake ni kuongeza tija kwa taifa letu na kuzidi kutatua changamoto ya upungufu wa ajira hususani kwa vijana," alisema.

Alisema ili kuikwamua nchi katika sekta mbalimbali serikali imejiwekea mikakati kadhaa ya utekelezaji, ikiwemo kuhuisha uwiano wa viwango vya mafunzo vyenye ujuzi wa juu yaani (Engineers), ujuzi wa kati (Technicians) na mafundi wa kazi za mikono (Artisans) kwa uwiano wa 1:5:25.

"Nawasihi tumieni ujuzi na umahiri mlioupata kwenye kujiajiri ili kujikwamua na wimbi la umasikini. Funguo ya mafanikio kwanza ni kuwa na ujuzi na maarifa, pili ni tabia na tatu ni vitendo," alisisitiza Ndahani.

Sanjari na kupongeza juhudi za serikali kupitia VETA Singida- kwa kuchagiza maendeleo ya vijana kiuchumi, Ndahani alitoa wito kwa wakurugenzi kuwatumia wahitimu wa vyuo hivyo na vijana wengine katika ujenzi wa miradi inayotumia 'Force Account'.

Alisema mfumo huo ulianzishwa na kutolewa maelekezo na Rais John Magufuli kwa maksudi, lengo likiwa ni kuwasaidia mafundi waliopo mitaani kupata ajira kupitia miradi hiyo.

Imeelezwa kwamba mfumo wa makandarasi umekuwa ukiwaumiza mafundi kwa kuwakosesha fursa mbalimbali hususani vijana wa kundi la kazi za mikono, huku baadhi ya Mabaraza ya Halmashauri na Wakurugenzi wakishindwa kusimamia ipasavyo.

"Niwasihi sana wakurugenzi kuwatumia sana vijana wa taifa hili wakiwemo hawa wanaopita kwenye mikono ya VETA katika ujenzi wa miradi hii ambayo kwa sasa ipo kila kona ya nchi" alisema Mgeni rasmi wa mahafali hayo Ndahani, ambaye pia ni Kaimu Afisa Vijana Mkoa wa Singida.

Kwa upande wake, mwenyeji wa mahafali hayo, Mkuu wa Chuo cha Veta-Singida, Paul Batoleki, alisema kupitia mahafali hayo, jumla ya wanachuo 156 wamehitimu fani mbalimbali kwa Ngazi ya Pili na Tatu.

Alizitaja fani hizo kuwa ni pamoja na Mifugo, Ufundi Magari, Uchomeleaji, Useremala, Ujenzi, Ushonaji, Umeme, na Ufundi Bomba, huku pia kukiwa na fani nyingine ya Uhazili na Kompyuta inayofundishwa chuoni hapo ambayo hata hivyo haikuwa na muhitimu kwenye mahafali hayo.

Batoleki alipongeza serikali kupitia Mamlaka hiyo ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini kwa kutenga jumla ya shilingi milioni 340 Kwa ajili ya ujenzi wa madarasa na maabara chuoni hapo kwa fani ya ufugaji wa wanyama.

Awali, kupitia risala yao, wahitimu hao Kwa kuzingatia ongezeko la tija chuoni hapo wameiomba serikali kutatua uhaba uliopo wa baadhi ya vitabu vya masomo ya fani.

Changamoto nyingine ni mamlaka ziangalie uwezekano wa kuwagharamia wanafunzi wawapo kwenye mafunzo kwa vitendo, hasa kwenye maeneo ya viwanda ambako wengi hujikuta wakifanya 'fields' zao katika mazingira magumu.

"Tunaomba pia tuongezewe walimu wa masomo ya muambata mfano 'LifeSkills' lakini kubwa serikali iangalie uwezekano wa kutuongezea vifaa kulingana na teknolojia za kisasa ili kuongeza tija na ufanisi,"  alisema Rais Mstaafu wa Chuo hicho, Elisha Ezekiel.

Mkoa wa Singida una jumla ya viwanda 1,805 ambapo kati yake kiwanda kikubwa ni 1, kati 10, vidogo 309 na vidogo sana 1,485 hatua ambayo imeendelea kupanua wigo wa fursa za ajira hususani kwa makundi ya vijana na wanawake kulingana na fani mbalimbali walizonazo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post