Wana Vituo vya Taarifa na maarifa , madiwani na watendaji wa halmashauri ya Msalala wakifanya ziara kwenye halmashauri ya Kishapu.
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Wanamtandao wa Jinsia kupitia Vituo vya Taarifa na Maarifa halmashauri ya Msalala wametembelea Vituo vya Taarifa na Maarifa halmashauri ya Kishapu mkoani Shinyanga na kujionea namna halmashauri hiyo ilivyofanikiwa katika uandaaji wa Bajeti kwa mrengo wa kijinsia na jinsi jamii na serikali wanavyoshirikiana katika shughuli za maendeleo.
Ziara hiyo ya mafunzo ya siku tatu iliyoanza Jumatatu Desemba 28,2020 na kuhitimishwa leo Jumatano Desemba 29,2020 ililenga kujifunza uandaaji wa bajeti ya mrengo wa kijinsia na umuhimu wake kupitia mradi wa Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wanawake kiuchumi unaotekelezwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kupitia shirika la Watu na Makazi Duniani (UNFPA.
Ziara hiyo ambayo pia imeshirikisha Madiwani, Maafisa Maendeleo, Watendaji wa kata na wataalamu wa halmashauri ya Msalala na Kishapu ilikuwa na lengo la kujenga uelewa wa pamoja kuhusu bajeti yenye mrengo wa kijinsia na umuhimu wake,kubadilishana uzoefu na mbinu kuwezesha ushawishi uingizwaji wa masuala ya jinsia katika bajeti na ujenzi wa vuguvugu za pamoja kupitia jamii.
Wakiwa katika Halmashauri ya Kishapu, Wanaharakati hao wa haki za wanawake na watoto kupitia vituo vya taarifa na maarifa vya kata ya Shilela na Lunguya wametembelea Vituo vinne vya Taarifa na maarifa wilayani Kishapu ambavyo ni vya kata ya Mwaweja, Ukenyenge, Maganzo na Songwa ambavyo ni sehemu ya vituo 9 wilayani humo ambapo vingine ni Kiloleli, Mondo, Kishapu, Mwadui Luhumbo na Bunambiyu.
Miongoni mwa mambo yaliyowafurahisha wanaharakati hao ni pamoja na ujenzi wa vyoo na uanzishwaji wa vyumba vya siri kwa ajili ya wanafunzi wa kike wanapokuwa katika hedhi ambapo vyumba hivyo vina vifaa vyote vinavyohitajika ikiwemo maji na taulo za kike ‘pedi’mfano katika shule ya msingi Bulimba iliyopo katika kata ya Ukenyenge,shule ya sekondari Ukenyenge na shule ya sekondari Songwa ambako ujenzi vyoo na chumba cha siri kwa ajili ya wanafunzi wa kike wanapokuwa katika hedhi.
Hali kadhalika wametembelea Zanahati ya Kijiji cha Mwaweja inayoendelea kujengwa pamoja na mradi wa maji ya Ziwa Victoria katika kata ya Ukenyenge ambao utaanza kutoa huduma hivi karibuni ili kuwapunguzia wanawake adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma ya maji.
Pia wameshuhudia ujenzi wa bweni la wanafunzi wa kike katika shule ya sekondari Ukenyenge,kuona madarasa matatu yaliyotokana na mchango wa vituo vya taarifa na maarifa wilayani Kishapu ambavyo vimekuwa vikihamasisha jamii kushiriki katika miradi ya maendeleo badala ya kusubiri serikali ifanye kila kitu.
Mbali na shule ya sekondari Ukenyenge, pia wametembelea shule ya maalumu ya Sekondari ya Wasichana maarufu ‘Kishapu Wasichana Sekondari’ iliyoanzishwa mwaka 2020 ikichukua wanafunzi wa kike wilayani Kishapu waliofanya vizuri katika matokeo yao ya mtihani wa darasa la saba sasa ikiwa na wanafunzi 115.
Madiwani wa halmashauri ya Kishapu akiwemo Underson Mandia wa kata ya Ukenyenge, Underson Mandia, Abdul Ngolomole (Songwa) na Bujiku Buganga Nyanda (Mwaweja) wamesema vituo vya taarifa na maarifa ni sehemu ya jamii vinafanya kazi ya jamii kwa kuibua miradi ya maendeleo.
Wamesema vituo hivyo vinatoa elimu ya umuhimu wa wananchi kuchangia kwa hiari bila shurti katika shughuli za maendeleo kwa kushirikiana na serikali.
“Vituo vya taarifa na maarifa vimekuwa msaada mkubwa sana, vimekuwa daraja kati ya wananchi na serikali. Wana vituo vya taarifa na maarifa wanaturahishia sana kazi sisi madiwani. Na kutokana na ushirikiano huu tulionao ndiyo maana mnaona kila mradi tunaoanzisha unafanikiwa kwa sababu wananchi wapo tayari kushirikiana na serikali”,wameongeza madiwani hao.
Nao wenyeviti wa vijiji vya Mwaweja Edward Ngoyeji na Damas Francis wa kijiji cha Songwa wamesema vituo vya taarifa na maarifa vimechangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa mimba za utotoni na matukio ya ukatili wa kijinsia ikiwemo vipigo kwa wanawake.
Mwenyekiti wa kituo cha taarifa na maarifa kata ya Ukenyenge, Fredina Said amesema suala la hedhi siyo jambo la aibu hivyo ni vyema elimu ikatolewa kwa jamii kuanzia ngazi ya familia kuwapatia watoto wa kike mahitaji yanayotakiwa wakiwa katika hedhi na watoto wa kiume wafundishwe elimu ya hedhi shuleni kuwa hedhi siyo ugonjwa wala siyo tatizo.
Mwenyekiti wa Vituo vya taarifa na maarifa wilaya ya Kishapu, Rahel Madundo ameiomba serikali kuendelea kushirikiana na vituo vya taarifa na maarifa kwani vimekuwa chachu ya maendeleo huku pia akiiomba TGNP kutoa mafunzo ya masuala ya jinsia kwa viongozi wa vijiji na kata ili kuongeza kasi zaidi ya maendeleo.
Afisa Maendeleo ya Jamii halmashauri ya wilaya ya Kishapu, Joseph Swalala ameeleza kufurahishwa jinsi madiwani, wanavituo vya taarifa na maarifa wanavyoshirikiana na halmashauri hiyo kutekeleza miradi ya maendeleo.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Msafara wa Wana Vituo vya Taarifa na maarifa kutoka halmashauri ya Msalala, Loyce Kabanza ambaye ni mwenyekiti wa kituo cha taarifa na maarifa kata ya Lunguya amesema ziara hiyo imekuwa na mafanikio makubwa na kwamba wataenda kuboresha zaidi kazi wanazofanya katika halmashauri yao.
Naye diwani wa kata ya Lunguya, Benedict Mussa na Diwani wa kata ya Shilela Philbert Elikana wamepongeza jinsi madiwani wa Kishapu wanavyoshirikiana pamoja na vituo vya taarifa na maarifa pamoja na halmashauri hiyo katika kutekeleza miradi ya maendeleo na mipango mbalimbali ikiwemo kutenga bajeti kwa ajili taulo za kike,ujenzi wa vyumba vya siri kwa wanafunzi wa kike.
Wamesema mambo yanayofanywa na vituo vya taarifa na maarifa na serikali wilayani Kishapu ni ya kuigwa wakitolea mfano kuanzishwa kwa shule maalumu ya wasichana Kishapu ili kupunguza matukio ya mimba na ndoa za utotoni sambamba na kuwapunguzia umbali wa kusafiri kwenda shuleni.
Akizungumza wa niaba ya Mkurugenzi wa TGNP, Afisa Programu wa TGNP, Anna Sangai amesema vituo vya taarifa na maarifa wilayani Kishapu pamoja na halmashauri ya Kishapu wamekuwa wa mfano wa kuigwa katika kutenga bajeti ya mrengo wa kijinsia wakiweka mstari wa mbele masuala ya hedhi kwa mtoto wa kike.
“TGNP tunao ujasiri wa kusimama kifua mbele kuizungumzia Kishapu, wamefanya kazi kubwa ya kujitolea kuleta maendeleo kwa wananchi hususani katika kutenga bajeti ya mrengo wa kijinsia ndiyo maana TGNP iliwapata tuzo kwa hatua hiyo. Tunaamini kabisa kuwa vituo vya taarifa na maarifa ni daraja kubwa la wanajamii na viongozi kuelekea kwenye maendeleo. Ili kufikia malengo yaliyokusudiwa ni lazima kila mtu atomize wajibu wake kuanzia ngazi ya familia,kijiji,kata hadi Halmashauri kwani mabadiliko yanaanza na sisi”,amesema Sangai.
“Natoa wito kwa vituo vya taarifa na maarifa kushirikiana na Wataalamu wa halmashauri kwani wana vitu vingi mnavyopaswa kujifunza kutoka kwao.Tumieni majukwaa mbalimbali kuzungumzia maendeleo na mkumbuke kuwa vituo vya taarifa na maarifa siyo upinzani bali ni kwa ajili ya kusaidia watu katika jamii”,ameongeza Sangai.
ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Jumatano Desemba 30, 2020 : Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Kishapu, Margareth Mapunda (katikati) akionesha mabweni kwa ajili ya wanafunzi wa kike wanaosoma katika shule hiyo kutoka wilaya ya Kishapu 'Kishapu Wasichana Sekondari' wakati wa ziara ya Wana Vituo vya Taarifa na maarifa , madiwani na watendaji wa halmashauri ya Msalala kwenye halmashauri ya Kishapu kujifunza masuala ya uandaaji wa bajeti kwa mrengo wa kijinsia na umuhimu wake na kubadilishana uzoefu iliyoandaliwa na TGNP. Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Kishapu, Margareth Mapunda (katikati) akionesha madarasa na mabweni kwa ajili ya wanafunzi wa kike wanaosoma katika shule hiyo kutoka wilaya ya Kishapu 'Kishapu Wasichana Sekondari' iliyopo katika kata ya Maganzo wakati wa ziara ya Wana Vituo vya Taarifa na maarifa , madiwani na watendaji wa halmashauri ya Msalala kwenye halmashauri ya Kishapu.
Afisa Maendeleo ya Jamii halmashauri ya Kishapu, Joseph Swalala akielezea namna Vituo vya taarifa na maarifa vilivyopaza sauti kuomba ijengwe shule ya Sekondari ya wasichana Kishapu kwa ajili ya wasichana ili kupunguza mimba za utotoni na kusafiri umbali mrefu kwenda shuleni ambapo amesema halmashauri hiyo iliamua kukarabati majengo yaliyopo katika mgodi wa Mwadui na kuanzisha shule hiyo inayochukua wanafunzi wa kike kutoka wilaya ya Kishapu waliofanya vizuri katika mtihani wa darasa la saba.
Mwenyekiti wa Vituo vya taarifa na maarifa wilaya ya Kishapu Rahel Madundo akielezea namna vituo vya taarifa na maarifa vilivyopaza sauti kuhusu changamoto wanazopata watoto wa kike na hatimaye shule ya Sekondari ya Wasichana Kishapu ikaanzishwa mwaka 2020.
Muonekano wa mabweni ya shule maalumu ya sekondari ya wasichana Kishapu.
Diwani wa kata ya Songwa halmashauri ya Kishapu, Abdul Ngolomole akielezea kuhusu ujenzi wa vyoo vya kisasa katika shule ya Sekondari Songwa unaoendelea kwa nguvu za wananchi baada ya kuhamasishwa na vituo vya taarifa na maarifa na serikali ambapo pia wametenga chumba cha siri kwa ajili ya wanafunzi wa kike kujisitiri wanapokuwa katika hedhi.
Wana Vituo vya Taarifa na maarifa , madiwani na watendaji wa halmashauri ya Msalala wakiangalia vyoo na chumba cha siri kwa ajili ya wanafunzi wa kike katika shule ya sekondari Songwa iliyopo katika halmashauri ya Kishapu.
Muonekano wa vyoo na chumba cha siri kwa ajili ya wanafunzi wa kike kujisitiri (cha kwanza kulia) ujenzi ukiendelea katika shule ya sekondari Songwa.
Muonekano wa vyoo ujenzi ukiendelea katika shule ya sekondari Songwa.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kishapu, Underson Mandia (kushoto) ambaye ni Diwani wa kata ya Ukenyenge akielezea mipango inayofanywa na halmashauri kuboresha mazingira ya shule ya sekondari Songwa ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vyoo vya walimu.
Mwenyekiti wa kituo cha taarifa na maarifa kata ya Ukenyenge, Fredina Said akisisitiza umuhimu wa kutoa elimu ya hedhi kwa wanafunzi wa kiume ili kuondoa dhana ya kwamba hedhi ni ugonjwa waache tabia ya kucheka watoto wa kike wanapokuwa katika hedhi lakini pia wazazi kuwapa mahitaji muhimu watoto wa kike kama vile taulo za kike.
Afisa Programu wa TGNP, Anna Sangai akizungumza katika kituo cha taarifa na maarifa Songwa halmashauri ya Kishapu na kupongeza kazi nzuri inayofanywa na vituo vya taarifa na maarifa na serikali kuwaletea maendeleo wananchi.
Afisa Programu wa TGNP, Anna Sangai akizungumza katika kituo cha taarifa na maarifa Songwa halmashauri ya Kishapu na kuwasihi wana vituo vya taarifa na maarifa kuendeleza ushirikiano walionao na viongozi wa serikali.
Mwenyekiti wa Vituo vya taarifa na maarifa wilaya ya Kishapu, Rahel Madundo akiwakumbusha wana vituo vya taarifa na maarifa kushirikiana, kudumisha mshikamano na kufanya kazi pamoja na viongozi wa vijiji,kata na halmashauri.
Katibu wa Vituo vya taarifa na maarifa wilaya ya Kishapu, Peter Nestory akizungumza wakati wa ziara ya Wana Vituo vya Taarifa na maarifa , madiwani na watendaji wa halmashauri ya Msalala kwenye kituo cha taarifa na maarifa Songwa halmashauri ya Kishapu.
Katibu wa kituo cha taarifa na maarifa kata ya Songwa, Christina Mihayo akizungumza wakati wa ziara ya Wana Vituo vya Taarifa na maarifa , madiwani na watendaji wa halmashauri ya Msalala kwenye kituo hicho halmashauri ya Kishapu.
Mwenyekiti wa kijiji cha Songwa Damas Francis akizungumza wakati wa ziara ya Wana Vituo vya Taarifa na maarifa , madiwani na watendaji wa halmashauri ya Msalala kwenye kituo cha taarifa na maarifa Songwa halmashauri ya Kishapu.
Diwani wa kata ya Songwa Abdul Ngolomole akizungumza wakati wa ziara ya Wana Vituo vya Taarifa na maarifa , madiwani na watendaji wa halmashauri ya Msalala kwenye kituo cha taarifa na maarifa Songwa halmashauri ya Kishapu.
Afisa Maendeleo ya Jamii halmashauri ya wilaya ya Kishapu, Joseph Swalala akizungumza wakati wa ziara ya Wana Vituo vya Taarifa na maarifa , madiwani na watendaji wa halmashauri ya Msalala kwenye kituo cha taarifa na maarifa Songwa.
Makamu Mwenyekiti wa halmashauri ya Kishapu, Underson Mandia akizungumza wakati wa ziara ya Wana Vituo vya Taarifa na maarifa , madiwani na watendaji wa halmashauri ya Msalala kwenye halmashauri ya Kishapu.
Kiongozi wa Msafara wa Wana Vituo vya Taarifa na maarifa , madiwani na watendaji wa halmashauri ya Msalala, Loyce Kabanza akizungumza katika kituo cha taarifa na maarifa Songwa halmashauri ya Kishapu na kupongeza kazi kubwa inayofanywa na vituo vya taarifa na maarifa kuibua changamoto zilizopo katika jamii.
Diwani wa kata ya Lunguya Benedict Mussa akizungumza kituo cha Taarifa na maarifa Songwa halmashauri ya Kishapu na kueleza kuwa ziara yao wilayani Kishapu imekuwa na mafanikio makubwa kwani sasa wataenda kuboresha kazi vizuri wakifanya kazi kwa kushirikiana zaidi.
Wana Vituo vya Taarifa na maarifa , madiwani na watendaji wa halmashauri ya Msalala wakipiga picha ya kumbukumbu na wana vituo vya taarifa na maarifa halmashauri ya Kishapu kwenye kituo cha taarifa na maarifa Songwa ambacho ni kituo cha kwanza kuanzishwa na TGNP wilayani Kishapu mwaka 2012.
Wana Vituo vya Taarifa na maarifa , madiwani na watendaji wa halmashauri ya Msalala wakipiga picha ya kumbukumbu na wana vituo vya taarifa na maarifa halmashauri ya Kishapu kwenye kituo cha taarifa na maarifa Songwa ambacho ni kituo cha kwanza kuanzishwa na TGNP wilayani Kishapu mwaka 2012.
Jumanne Desemba 29,2020 : Diwani wa kata ya Mwaweja Bujiku Buganga Nyanda akiwakaribisha Wana Vituo vya Taarifa na maarifa , madiwani na watendaji wa halmashauri ya Msalala katika kata hiyo ili kujionea na kujifunza mambo mbalimbali yanayofanywa na vituo vya taarifa na maarifa halmashauri ya Kishapu.
Wana Vituo vya Taarifa na maarifa , madiwani na watendaji wa halmashauri ya Msalala wakiwa katika zahanati ya kijiji cha Mwaweja inayoendelea kujengwa ambayo pia inatokana na vituo vya taarifa na maarifa kupaza sauti juu ya changamoto wanazokumbana nazo akina mama ikiwemo kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya na kujifungulia njiani. Vituo vya taarifa vilishiriki pia kuchimba msingi na kusomba mchanga kwa ajili ya kuanzisha ujenzi wa zanahati hiyo inayojengwa kwa nguvu ya wananchi na halmashauri ya Kishapu.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwaweja Edward Ngoyeji akizungumzia ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Mwaweja.
Wana Vituo vya Taarifa na maarifa , madiwani na watendaji wa halmashauri ya Msalala wakiondoka katika zahanati ya kijiji cha Mwaweja kilichopo katika kata ya Mwaweja halmashauri ya Kishapu.
Diwani wa kata ya Ukenyenge, Underson Mandia akielezea kuhusu mradi wa maji katika kijiji cha Bulimba jinsi ulivyoibuliwa na hivi karibuni wananchi wataanza kupata huduma ya maji ili kuondokana na adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma ya maji.
Muonekano wa Tanki la maji katika kata ya Ukenyenge kupitia mradi maji kutoka Ziwa Victoria ambapo wananchi wataanza kupata huduma ya maji hivi karibuni.
Wana Vituo vya Taarifa na maarifa , madiwani na watendaji wa halmashauri ya Msalala wakiondoka katika mradi wa maji ya Ziwa Victoria katika kata ya Ukenyenge.
Afisa Programu wa TGNP, Anna Sangai akizungumza katika shule ya Msingi Bulimba kata ya Ukenyenge ambapo pamejengwa vyoo na chumba cha siri kwa ajili ya watoto wa kike kujisitiri wanapokuwa katika hedhi.
Muonekano wa vyoo (matundu 12) na chumba cha siri kwa ajili ya wanafunzi wa kike kujisitiri wanapokuwa katika hedhi katika shule ya Msingi Bulimba kata ya Ukenyenge kinachotokana na mchango wa vituo vya taarifa na maarifa halmashauri ya Kishapu.
Muonekano wa choo chenye matundu mawili (moja wavulana na moja wasichana) kilichokuwa kinatumiwa na wanafunzi wa shule ya msingi Bulimba iliyoanzishwa mwaka 1976 iliyopo katika kata ya Ukenyenge ambapo vituo vya taarifa vilipaza sauti na wananchi kuanzisha ujenzi wa vyoo vipya na chumba cha siri kwa ajili ya watoto wa kike kujisitiri wanapokuwa katika hedhi.
Wanaharakati wa haki za wanawake na watoto kupitia vituo vya taarifa na maarifa halmashauri ya Msalala wakiangalia chumba cha siri katika shule ya Msingi Bulimba kata ya Ukenyenge kwa ajili ya wanafunzi wa kike kujisitiri wanapokuwa katika hedhi.
Mwenyekiti wa kituo cha taarifa na maarifa kata ya Ukenyenge, Fredina Said akionesha vifaa vinavyopatikana katika chumba cha siri kwa ajili ya wanafunzi wa kike katika shule ya msingi Bulimba.
Makamu mwenyekiti wa halmashauri ya Kishapu, Underson Mandia ambaye ni diwani wa kata ya Ukenyenge akionesha bweni la wanafunzi wa kike katika shule ya sekondari Ukenyenge ambalo pia linatokana na vituo vya taarifa na maarifa kupaza sauti ili kuondokana na mimba za utotoni na wanafunzi kukatishwa masomo.
Makamu mwenyekiti wa halmashauri ya Kishapu, Underson Mandia ambaye ni diwani wa kata ya Ukenyenge akionesha madarasa katika shule ya sekondari Ukenyenge na kuelezea vyoo na chumba cha siri kwa wanafunzi wa kike kujisiri wanapokuwa katika hedhi ambavyo vimetokana na vituo vya taarifa kupaza sauti.
Muonekano wa madarasa katika shule ya sekondari Ukenyenge.
Wana Vituo vya Taarifa na maarifa , madiwani na watendaji wa halmashauri ya Msalala wakipiga picha ya kumbukumbu na wana vituo vya taarifa na maarifa halmashauri ya Kishapu wakipiga picha ya kumbukumbu katika shule ya sekondari Ukenyenge wilayani Kishapu.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Soma pia: