Dereva wa Lori Emmanuel Nobert Msuya (30) mwenye shati la bluu akishambuliwa kwa ngumi na mateke na abiria wa basi la Frester wakimtuhumu kutaka kusababisha ajali eneo la Samuye barabara ya Shinyanga - Mwanza.
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linamshikilia dereva wa Basi la Frester lenye namba za usajili T.915 CGU Mwita Chacha Chaguche na abiria watatu Joyce Charles, Athuman Mussa na Christopher Langati kwa kosa la kumshambulia kwa ngumi na mateke dereva wa lori aitwaye Emmanuel Nobert Msuya (30) wakimtuhumu kutaka kusababisha ajali eneo la Samuye barabara ya Shinyanga - Mwanza.
Kuanzia Desemba 21,2020 kumekuwa na Video (Clip) ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii ikionesha abiria wa basi la Frester wakitoa matusi huku wengine wakimsukuma na kupiga ngumi na mateke dereva wa lori wakisema anataka kusababisha ajali kwa kubana basi upande wa kushoto.
Sasa leo Desemba 23,2020, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba ametoa ufafafuzi kuhusu video hiyo na kueleza kuwa tukio hilo limetokea Desemba 21,2020 majira ya saa 11 jioni katika kijiji cha Samuye,kata ya Samuye wilaya ya Shinyanga.
Akisimulia kuhusu tukio hilo, Kamanda Magiligimba amesema :
"Gari lenye namba za usajili T.971 DTQ Fuso Lori likiendeshwa na Emmanuel Nobert Msuya (30) mkazi wa Moshi likitokea Moshi kuelekea Mwanza lilipofika katika Mizani ya Tinde, mkoa wa Shinyanga lilifanyiwa vurugu kwa kubanwa ubavuni na basi la Kampuni ya Frester namba T.915 CGU likitoka Kahama kwenda Mwanza lililokuwa likiendeshwa na Mwita Chacha Chaguche mkazi wa Kahama kwa lengo la kutaka kupimwa uzito kabla ya lori hilo"
".......Lakini mwenye lori hilo hakumruhusu mwenye basi na alifanikiwa kupima kabla ya basi na kuendelea na safari bila kusababisha ajali yoyote ile", anasimulia Kamanda Magiligimba.
Amesema baada ya basi la Frester kupimwa uzito wake na kuondoka eneo la Mizani likiwa njiani lilifuata lori hilo ambalo lilikuwa tayari limetangulia na kulibana upande wa kushoto huku dereva wa basi akimuoneshea dharau ya kuwa pamoja na kuwahi kupima lakini amemkuta na kumpita pia.
"Ndipo mwenye lori naye akalipita basi na kulifuata upande wake, dereva wa basi alipoona hivyo alikwenda nje ya barabara kumkwepa ambapo magari yote yalisimama,madereva wote wakashuka",amefafanua Kamanda Magiligimba.
"Baada ya madereva wote kushuka ndipo dereva wa basi Mwita Chacha Chaguche akisaidiwa na abiria watatu ambao ni Joyce Charles, Athuman Mussa na Christopher Langati walianza kumshambulia dereva wa lori Emmanuel Nobert Msuya kwa ngumi na mateke", ameongeza Kamanda Magiligimba.
Amesema watuhumiwa wanashikiliwa na jeshi la polisi na watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.
Aidha katika tukio hilo madereva wote wawili walishtakiwa kwa kosa la matumizi mabaya ya barabara na kutaka kusababisha ajali.
Kamanda Magiligimba anatoa wito kwa wananchi kuacha kujichukua sheria mkononi na badala yake wapeleke malalamiko yao kwenye vyombo husika huku akiwaasa madereva wawapo kwenye majukumu yao kuheshimiana na kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali zisizo za lazima.
Dereva wa Lori Emmanuel Nobert Msuya (30) mwenye shati la bluu akishambuliwa kwa ngumi na mateke na abiria wa basi la Frester wakimtuhumu kutaka kusababisha ajali eneo la Samuye barabara ya Shinyanga - Mwanza.
Dereva wa Lori Emmanuel Nobert Msuya (30) mwenye shati la bluu akishambuliwa kwa ngumi na mateke na abiria wa basi la Frester wakimtuhumu kutaka kusababisha ajali eneo la Samuye barabara ya Shinyanga - Mwanza.
Dereva wa Lori Emmanuel Nobert Msuya (30) mwenye shati la bluu akishambuliwa kwa ngumi na mateke na abiria wa basi la Frester wakimtuhumu kutaka kusababisha ajali eneo la Samuye barabara ya Shinyanga - Mwanza.
Muoneko wa Lori na basi la Frester