Raia wa Burundi wakamatwa kwa kuishi nchini kinyemela


Raia wawili wa Burundi wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa madai ya kuingia na kuishi nchini bila kuwa na vibali vinavyotambulika kisheria

Akisoma hati ya mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Yusto Ruboroga, Wakili wa Serikali Shija Sitta amedai kuwa washitakiwa hao Sindandugu John na Chekelo Aziz walikamatwa eneo la Msimbazi, jijini Dar es Salaam Novemba 24 mwaka huu kwa tuhuma ya kuingia nchini bila vibali na kuishi nchini bila kuwa na nyaraka zinazotambulika kisheria.

Aidha Wakili Sita amedai kuwa washitakiwa hao baada ya kuingia nchini walianza kufanya kazi ya kuendesha pikipiki maarufu bodaboda.

Hata hivyo washitakiwa hao wamekana shitaka lao na kesi hiyo imeahirisha hadi Disemba 14 mwaka huu kwa ajili ya washitakiwa kusomewa hoja za awali.

Akizungumza kwa niaba ya Idara ya Uhamiaji mara baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo Wakili Sitta amewataka wananchi kuepuka kutoa ajira kwa watu wanaoingia nchini bila kuwa na taarifa kamili za uraia wao kwa ajili ya usalama wa Taifa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post