SERIKALI YAIMARISHA MIFUMO YA UKUSANYAJI WA MIRAHABA YA KAZI YA WASANII


Na Anitha Jonas – WHUSM, Dar es Salaam
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali amesema kuwa tangu COSOTA ihamie wizara hiyo imeboresha Kanuni mbalimbali ambazo zitasaidia kuongeza ukusanyaji wa mirabaha na imeongeza adhabu ya faini kutoka milioni 5 mpaka milioni 20 kwa mtu anayekamatwa na uharamia wa kazi za Sanaa, pia Kanuni hizo zimetoa nafasi ya Mtendaji wa COSOTA kuwa na mamlaka ya kutoza faini hiyo papo kwa papo.

Dkt. Abbasi ameyasema hayo  jana Desemba 03, 2020 Jijini Dar es Salaam katika mwendelezo wa mikutano yake ya kukutana na makundi  mbalimbali ya Sanaa, ambapo kwa siku hii alikutana na  MaDJ’s,  Wataarishaji wa Muziki na Filamu na Waongozaji wa Filamu.

Akiendelea kuzungumza katika mkutano huo Dkt.Abbasi alitoa msisitizo kwa BASATA na Bodi ya Filamu kuweka juhudi zaidi katika kujenga sekta ya Sanaa badala ya  kudhibiti au kufungia.

“Serikali kwa sasa ipo katika hatua za kuboresha mifumo ya hakimiliki ili kuhakikisha wasanii wa makundi yote wananufaika na ubunifu wa kazi zao kwa kila zinapotumika katika mazingira yoyote hivyo basi ni muhimu kwa kila msanii kusajili kazi yake ili aweze kunufaika na kwa upande wa waandaaji wa muziki ni vyema wakafahamu umuhimu wa kuwa na umiliki wa midundo ‘beats’ wanazoandaa na kusajili,”alisema Dkt. Abbasi.

Pamoja na hayo naye Mtendaji Mkuu wa COSOTA Doreen Sinare aliwasihi Watayarishaji wa kazi za Muziki  kusajili kazi zao kwani hawawezi kupata haki zao kama hawatasajili ‘beats’ wanazoandaa, ambapo alifafanua mara nyingi imekuwa ikionekana kama Mwanamuziki ndiyo mwenye umiliki wa kila kitu katika muziki na ubunifu wa mtayarishai huyo kusahaulika.

Halikadhalika katika mkutano huo Dkt. Abbasi aliwasihi wadau wa Sanaa kuanisha utitiri wa kodi zinazosumbua sekta hiyo ili serikalini iweza kujenga hoja ya namna zinaweza kupunguzwa,pia aliwasihi wasanii hao kuanisha mahitaji ya mafunzo yatakayowasaidia kuongeza ufanisi katika kutekeleza kazi zao kwa kushirikiana na Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa).



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post