SERIKALI YASISITIZA MATUMIZI YA CHANJO ILI KUPATA MIFUGO BORA
Saturday, December 26, 2020
Na. Edward Kondela
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amesema Tanzania ina chanjo za kutosha dhidi ya magonjwa ya mifugo na kuagiza wafugaji wote nchini pamoja na maeneo ambayo serikali inafuga kuhakikisha mifugo yao inachanjwa ili kuondokana na magonjwa hayo.
Akizungumza 24.12.2020) mara baada ya kutembelea Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI) iliyopo Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani, wakati wa ziara yake ya siku mbili mkoani humo, Waziri Ndaki amesema ili kuhakikisha Tanzania inakuwa na mifugo bora inayokidhi soko la kimataifa ni lazima mifugo ichanjwe dhidi ya magonjwa ili yapatikane mazao bora ya mifugo.
“Tunayo chanjo ya kutosha hivyo niwatake wafugaji wote ikiwa ni pamoja na sisi serikali kwenye maeneo ambayo tunafuga tuchanje mifugo yetu ili tupate mifugo iliyo bora, tunataka sasa nchi yetu iende kwenye ubora badala ya uwingi wa mifugo, ili tupate nyama bora na maziwa bora kwa maana ya mazao bora ya mifugo ili tuweze kuuza katika soko la kimataifa.” Amesema Mhe. Ndaki
Katika ziara hiyo kwenye taasisi ya TVI, Waziri Ndaki alitaka kufahamu namna agizo alilolitoa hivi karibuni la ng’ombe waliopo kwenye ranchi 14 za taifa kuchanjwa dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu kutokana na baadhi ya mifugo hiyo kuathiriwa na ugonjwa huo katika Ranchi ya Kongwa iliyopo Mkoani Dodoma, ambapo Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) ambayo inaisimamia TVI, Dkt. Stella Bitanyi amesema chanjo zimesambazwa kutokana na mahitaji ya ranchi hizo na sasa wapo katika hatua ya chanjo hizo kuwafikia majirani wa ranchi hizo ili kuweza kuchanja ng’ombe wao.
Aidha, Waziri Ndaki amejionea ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha chanjo cha HESTER kilichopo Wilayani Kibaha na kupongeza hatua mbalimbali ambazo zimefikiwa katika ujenzi huo na kusema mara kiwanda hicho kitakapoanza kufanya kazi Mwezi Aprili Mwaka 2021, kitasaidia kuongeza wigo wa uwepo wa chanjo nyingi hapa nchini na kusaidia endapo magonjwa ya mifugo yatajitokeza.
“Hii inaonesha umuhimu wa kuwa na chanjo tayari kwa ajili ya mifugo yetu yote ili ikitokea magonjwa ya milipuko tuweze kupata mahali pa kusaidiwa kwa karibu na pengine kwa bei nafuu kwa kuwa chanjo hizi zitakuwa zinazalishwa hapa nchini.” Amefafanua Mhe. Ndaki
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amefika pia katika kiwanda cha kuchinja na kuchakata nyama cha TAN CHOICE kilichopo Wilayani Kibaha, na kubainisha kuwa umuhimu wa uwepo wa viwanda hivyo kutasaidia kubadilisha fikra za wafugaji kwa kuingia kwenye ufugaji bora.
Kuhusu changamoto ya vibali vya kuingiza nyama zilizochakatwa kwenye baadhi ya nchi kutoka Tanzania, Waziri Ndaki amesema wizara itawasiliana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa pamoja na Wizara ya Viwanda na Biashara ili kufahamu changamoto zinazovikabili baadhi ya viwanda kushindwa kusafirisha nyama kwenda baadhi ya nchi kutokana na kukosa vibali vya kuingiza nyama hizo kutoka Tanzania.
Pia, amefafanua kuwa uwepo wa viwanda vya kuchinja na kuchakata nyama nchini kunazidi kusaidia kukuza biashara ya mifugo nchini na kuongeza wigo wa soko la mifugo hivyo ni muhimu kwa wafugaji kuanza kuhakikisha wanakuwa na mifugo iliyo bora ili waweze kuuza mifugo yao kwa bei nzuri na waweze kunufaika kiuchumi na taifa pia liweze kupata mapato ya kutosha kupitia biashara ya mifugo.
Awali akiwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amekutana na mkuu wa mkoa huo Mhandisi Evarist Ndikilo ambapo wamezungumza mambo mbalimbali yanayohusu sekta za mifugo na uvuvi.
Katika mazungumzo hayo Mhandisi Ndikilo amesema kwa sasa migogoro ya wakulima na wafugaji imepungua kwa kiasi kikubwa huku akitaka juhudi zaidi zifanyike katika kuwapatia wafugaji elimu ya kuwa na mifugo michache na yenye tija badala ya kuwa na mifugo mingi ambayo haitoshi kutokana na uwepo wa maeneo ya kufugia.
Kwa upande wake Waziri Ndaki amesema changamoto zinazohusu wizara atahakikisha zinafanyiwa kazi ili sekta za mifugo na uvuvi ziwe endelevu na kuondokana na migogoro isiyo na tija kwa taifa.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amemaliza ziara ya kikazi ya siku mbili Mkoani Pwani, ambapo katika siku ya kwanza (23.12.2020) alipata fursa ya kuzungumza na baadhi ya wafugaji Wilayani Rufiji na kuwataka kuheshimu maeneo waliyopewa na uongozi wa mkoa kwa ajili ya ufugaji na kuacha kuingia katika maeneo ya wakulima.
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin