Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MWIGULU NCHEMBA ATAKA SHERIA, MWENENDO WA MASHAURI NA HUKUMU ZIANDIKWE KWA LUGHA YA KISWAHILI


 Na Mathias Canal, Wizara ya Katiba na Sheria-Dar es salaam
Serikali imedhamiria kuwasaidia kwa umakini mkubwa wananchi katika tasnia ya sheria ambapo imeagiza kuanza haraka uandaaji wa sheria kwa lugha ya kiswahili ikiwemo mwenendo wa mashauri na hukumu.


Agizo hilo kwa katibu mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria  limeelekeza kutafutwa haraka iwezekanavyo wataalamu watakazitafsiri sheria zote zilizoandikwa kwa lugha ya kingereza na kuwa katika lugha ya Taifa ya Kiswahili.

Waziri wa katiba na Sheria Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba ametoa agizo hilo tarehe 22 Disemba 2020 alipotembelea Taasisi ya mafunzo ya uanasheria kwa vitendo Tanzania (Law School of Tanzania) wakati akiwa katika siku ya pili ya ziara ya kikazi Jijini Dar es salaam.

"Kwenye kauli nzuri za kuvutia tunasema kiswahili ndio lugha nzuri tena ya kuvutia hivyo ni lazima tuanze kufundisha kwa kufuata muelekeo wa lugha ya Taifa ili kuachana na utumwa wa matumizi ya lugha za kikoloni katika sheria zetu" Amekaririwa Mhe Nchemba

Amesema kuwa Sheria ambayo mwananchi anahukumiwa imeandikwa kingereza, hukumu anayopewa imeandikwa katika lugha ya kingereza hilo ni eneo la haki za watu hivyo inapaswa kwanza lugha ya kiswahili ndiyo itumike kwenye sheria kisha lugha zingine kama kingereza ziwe nyongeza.

Dkt Mwigulu amesema kuwa Sheria zinaandikwa katika lugha ya kingereza na kuwaambia wananchi kutokujua kwao sheria sio sehemu ya utetezi jambo hilo ni kinyume na utaratibu hivyo lazima kufanya mapitio ya sheria zilizopo.

"Zipo nchi nyingi Duniani zimeendelea pasina kuwa zinajua lugha ya kingereza hivyo ni wajibu wetu sasa rasmi kuitumia lugha ya kiswahili" Amesisitiza

Waziri Mwigulu amesema kuwa katika mikutano mingi ya usaili wa kazi inatumika lugha ya kingereza wakati huo huo viongozi wakuu wa usaili wanatumia lugha ya kiswahili katika familia zao, na hata kazini.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Geofrey Mizengo Pinda amesema kuwa uhitaji wa wataalamu wa kisheria katika maeneo mengi ni mkubwa hivyo taaluma hiyo inapaswa kutolewa kwa weledi mkubwa kwa maslahi makubwa ya Taifa.

Amesema kuwa mahitaji ya msaada wa kisheria ni makubwa hivyo ni muhimu kuona ulazima wa kutembelea katika maeneo mbalimbali hususani vijijini kutoa msaada wa kisheria kwani kumekuwa na manyanyaso kwa wananchi wengi.

Ameongeza kuwa Taasisi ya mafunzo ya uanasheria kwa vitendo Tanzania ni sehemu ya ukombozi kwa wananchi hivyo kuna kila sababu ya kutengeneza chombo kama hicho kuwafikia wananchi kirahisi.
MWISHO



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com