TRA SIMIYU YATAJA SABABU ZA KUVUKA LENGO LA UKUSANYAJI WA MAPATO IDARA YA KODI ZA NDANI 2019/2020


 Samirah Yusuph.

Bariadi. Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) mkoa Simiyu imeleza sababu za kuvuka lengo la ukusanyaji wa mapato idara ya kodi za ndani kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020 kuwa ni kuongezaka kwa ulipaji kodi kwa  hiari kupitia uwasilishaji wa ritani sahihi za kodi.



Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020(Julai 2019 hadi juni 2020) mkoa ulipangiwa kukusanya jumla ya tsh 8.7 bilioni na kufanikiwa kukusanya jumla ya tsh 8.6 bilioni ikiwa ni sawa na asilimia 99.5 ya lengo.

Huku katika idara ya mapato ya ndani kwa mwaka wa fedha 2018/2019 lengo lilikuwa kukusanya tsh 3.5 bilioni, makusanyo yalikuwa tsh 5.9 bilioni sawa na asilimia 169, 2019/2020 lengo lilikuwa tsh 8.7 bilioni, makusanyo yalikuwa tsh 8.6 bilioni ufanisi wa asilimia 99.5 ongezeko la tsh 2.7 bilioni sawa na ukuaji wa asilimia 46.

Akieleza sababu hizo Michael Nsobi, Meneja Msaidizi wa TRA Mkoa wa Simiyu alisema kuwa ongeko hilo limechangiwa na malipo ya kodi husika kwa wakati hasa kutoka katika sekta ya maliasili na utalii,sekta ya viwanda pamoja na sekta ya chakula na malazi.

"Mbali na sekta hizo kuchangia kwa kiasi kikubwa katika ukusanyaji wa mapato pia mpango wa serikali wa ukusanyaji wa madeni bila riba (Tax Amnesty Program),"alisema Nsobi na kuongeza kuwa:

"Kwa kipindi cha waka huu wa fedha 2020/2021 mkoa wa Simiyu umepangiwa kukusanya kiasi cha tsh 9.6 bilioni kwa idara ya kodi za ndani kwa mchanganuo wa kodi za kawaida, kodi za majengo pamoja na ushuru wa mabango".

Katika kipindi cha kuanzia julai hadi novemba 2020 mkoa ulipangiwa kukusanya lengo la jumla ya tsh 3.6 bilioni na kufanikiwa kukusanya tsh 3.4 ikiwa ni sawa na asilimia 93.4 ya lengo.

Kwa upande wao baadhi ya wafanya biashara katika soko kuu la mji wa Bariadi walisema kuwa licha ya ongezeko hilo la mapato lakini bado kuna mapato mengi yanapotea kutokana na wauzaji kutokutoa risiti na wanunuzi kutokudai risiti.

"Ni haki yetu kulipa kodi japo kuna muda unaona kuwa ni hasara lakini tukizingatia utoaji wa risiti tutaziba mianya mingi ya upotevu wa mapato," alisema John Mpanduzi mfanyabiashara wa vifaa vya ujenzi.

"Bado elimu inahitajika hasa hasa kwetu wanunuzi kwa sababu baadhi wanatoa risiti na wengine hawatoi hali hiyo inarudusha nyuma ukusanyaji wa mapato kama mtu hatoi risiti na hachukuliwi hatua yoyote mimi ninaye toa inanipa changamoto,"alisema Neema Cosmas mfanyabiashara wa vyombo.

Kwa upande wake katibu tawala wa mkoa wa Simiyu Miriam Mmbaga ameainisha kuwa makusanyo hayo ya mapata ni juhudi za TRA pamoja na wananchi katika kuhakikiaha mapato ya ndani hayapotei.

"Ongezeko hili liwe ni sababu ya TRA kuwa na matamanio makubwa zaidi ya kukusanya mapato, mzidishe ufanisi lakini pia niwatake wananchi kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha wanapa kodi pamoja na ushuru stahiki," alisema Miriam.

Mwisho.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post