Uingereza leo Jumanne Desemba 8 imeanza kutoa chanjo dhidi ya virusi vya corona, huku bibi kizee wa miaka 90 akiwa wa kwanza kupata chanjo hiyo iliyotengenezwa na Pfizer-BioNTech.
Chanjo hiyo ya kihistoria ilitolewa kwa Margaret Keenan katika hospitali ya Coventry, katikati ya England.
"Najisikia mwenye bahati kuwa mtu wa kwanza kuchanjwa dhidi ya Covid-19," alisema Keenan, ambaye wiki ijayo atafikisha umri wa miaka 91.
Uingereza imeanza zoezi la kutoa chanjo ya Covid-19 iliyotengenezwa kwa ushirikiano wa makampuni ya Pfizer na BioNTech, likiwa taifa la kwanza la Magharibi, kushiriki zoezi hilo kwa umma wa watu wake, katika kile kinachoelezwa uamuzi mkubwa na muhimu wa kukabiliana na janga la virusi vya corona.
Wa kwanza kupata chanjo hiyo katika siku iliyopachikwa jina la "V-Day" walikuwa wazee wenye umri wa kuanzia miaka 80, wafanyakazi wa afya majumbani na wafanyakazi wa afya walio mstari wa mbele.