Na Godwin Myovela, Singida
MATUKIO ya ukatili mkoani hapa yameendelea kuumiza vichwa vya viongozi wa serikali na wadau, hatua iliyopelekea kuja na mapendekezo kadhaa, ikiwemo kuomba kuangalia uwezekano wa kufuta dhamana kwa watuhumiwa wa ubakaji na mimba za utotoni.
Imebainika, baadhi ya watu ndani ya jamii wanashindwa kutoa ushirikiano ipasavyo pindi wanaposhuhudia au kuwa na taarifa sahihi za matukio hayo, kutokana wahalifu hao kupatiwa dhamana muda mfupi baada ya kufikishwa kwenye vituo vya polisi na mahakama, hali inayohatarisha usalama kwa watoa taarifa.
Matukio ya ukatili yaliyoibuliwa na shirika lisilo la kiserikali la Stars of Poverty Rescue Foundation (SPRF) chini ya ufadhili wa Foundation for Civil Society (FCS) kwa wilaya ya Ikungi pekee mkoani hapa mpaka sasa idadi yake imefikia 104, huku mengi kati ya hayo yakionekana kumalizwa katika ngazi ya familia kwa kuepusha kadhia hiyo.
Wakizungumza hivi karibuni wakati wa kikao cha kupeana mrejesho wa nini kinapaswa kufanyika ili kutokomeza matukio hayo, WADAU mbalimbali likiwemo Jeshi la Polisi wilayani hapo wametaka viongozi wa ngazi zote za utatuzi kutoruhusu kesi hizo kumalizwa kwenye ngazi za familia.
"Haiwezekani mtoto chini ya miaka 18 anapewa mimba halafu wewe mzazi unakwenda kujadiliana na mhalifu namna ya kupeana mahari haikubaliki!," alieleza Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Ikungi, Magoma Mtani.
Mtani alieleza kwamba kwa uzoefu wake ndani ya Idara ya Upelelezi kwenye jeshi hilo amebaini wahanga walio wengi, hususan watoto wanafundishwa na wazazi namna ya kuficha ukweli wa matukio hayo, hali inayopelekea kesi nyingi kuharibika.
"Kwa sasa baada ya tukio kuripotiwa hatuwaachi tena warudi nyumbani, tunahakikisha hapo hapo kesi inaenda mahakamani sababu ukisema uwaache tu warudi nyumbani basi hiyo kesi imeharibika," alisema.
Kwa upande wake Mkuu wa Kituo cha Polisi Ikungi, Stephen Chaula aliwataka baadhi ya watendaji ngazi za vitongoji, vijiji na kata kuhakikisha wanaepuka kusuluhisha kesi zinazohusiana na matukio ya ukatili wa kijinsia kwenye maeneo yao.
"Kumaliza kifamilia-familia tafsiri yake ni kuongeza na kuchochea vitendo hivi vya ukatili. Leteni Polisi ili sheria zichukue mkondo wake kama fundisho kwa wengine wenye tabia kama hizo," alisema Chaula.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa SPRF, Dk. Suleiman Muttani matukio yaliyoibuliwa na kutaarifiwa kwa kati ya mwezi Machi na Novemba mwaka huu yamefikia 48, huku 7 kati ya hayo yakimalizwa kwa majadiliano kwenye ngazi ya familia ndani ya wilaya ya Ikungi.
Muttani anasema shirika limebaini changamoto kadhaa wakati likitekeleza majukumu yake ya kukabiliana na vitendo vya ukatili, mosi ikiwa ushirikiano mdogo wa wahanga kutoa ushahidi juu ya kesi zilizoripotiwa.
Lakini baadhi ya sheria ndogo ndogo za vitongoji na vijiji sio rafiki, kutokana na kumtaka mlalamikaji kuwalipa askari mgambo kati ya shilingi elfu 5 hadi 10 ndipo atoke kwenda kumkamata mtuhumiwa, jambo linalokatisha tamaa.
Afisa Maendeleo mkoa wa Singida, Patrick Kasango alisema anaamini kama kila mtu atawajibika na kuchukua hatua stahiki kwa nafasi aliyonayo matukio hayo ya kufedhehesha yatabaki kuwa ni historia.
"Na kama inafika hatua ya jamii kwenda kwenye haki na ikaikosa haki; basi haki inaweza kutafutwa kwa njia nyingine," alisema Kasango na kuongeza:
"Wananchi hawapaswi kulilaumu jeshi la polisi kwa sababu dhamana kwa makosa hayo ni haki ya kikatiba ya mtuhumiwa...hata akidhaminiwa mara 70 sio kosa la polisi," alisema
Katekista wa Kanisa Katoliki kutoka kigango cha Munkinya, wilayani hapo Patricy Joseph, alivinyooshea kidole vyombo vya utoaji haki hususani kwenye matukio ya mimba za utotoni na ndoa za umri mdogo kwa kuingiza siasa nyingi kuliko uhalisia.
"Haiwezekani unamripoti mtuhumiwa wa tukio kubwa kama ubakaji, ulawiti au kumpa mimba mwanafunzi halafu anapewa dhamana...anarudi mtaani na kuanza kutamba na kukutishia, ndio maana jamii imekuwa na uoga. Angalieni vizuri sheria hii mtu akikamatwa kwa makosa haya asipewe dhamana," alisema Joseph.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi aliwataka watendaji wote wilayani hapo kujikita katika kutoa elimu ili kuepukana na matukio hayo.
"Mwezi Februari mwaka huu wakati ule tukiwa na matukio 56 tulikutana na kushauriana namna ya kupunguza...sasa leo zimeongezeka kesi nyingine 48 hapana hii haikubaliki! Tujikite zaidi katika kuelimisha jamii," alisema Kijazi.