Mtafiti Jacob Kateri akichukua maoni kutoka kwa wadau mbalimbali wa elimu Chamwino, Dodoma.
Na Abby Nkungu, Singida
Jumla ya wanafunzi 294 wamekatisha masomo yao katika shule 20 za msingi za halmashauri za wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma na Singida mkoani Singida katika kipindi cha mwaka 2018 kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo mazingira ya shule yasiyokuwa rafiki.
Taarifa ya Utafiti ya Action Aid chini ya Mradi wa Kuvunja vikwazo, Haki kodi na Utoaji huduma kwa usawa wa kijinsia uliojikita katika halmashauri hizo, imebaini kuwa walioacha shule ni sawa na ongezeko la asilimia 2.4 ikilinganishwa na asilimia 1.7 mwaka 2017 ambapo wanafunzi 186 tu waliacha shule.
Akiwasilisha taarifa hiyo kwenye mikutano ya wadau wa elimu katika halmashauri hizo kwa nyakati tofauti, Mtafiti Jacob Kateri alisema kuwa katika utafiti huo uliofanyika Januari na Februari mwaka jana, kati ya wanafunzi 294, Wavulana walikuwa 165 na Wasichana 129.
"Hiki ni kiwango cha juu sana ikilinganishwa na Takwimu za Kitaifa za 'Basic Education Statistics in Tanzania' (BEST) ambapo katika kipindi hicho ni asilimia 0.7 tu ya wanafunzi wote ndio walioacha shule", alisema Kateri.
Alitaja baadhi ya sababu za kuacha shule kuwa ni kupata mimba, baadhi yao kupewa uhamisho, mazingira yasiyokuwa rafiki; hasa kwa wasichana balehe na walio na ulemavu pamoja na utoro ambao takwimu zake zinaonesha kuwa upo kwa zaidi ya asilimia 30.
Alibainisha shule zilizofanyiwa utafiti wilayani Chamwino kuwa ni shule za msingi Buigiri Misheni, Chamwino, Mahama, Makang'wa, Mapinduzi, Matembe, Msanga na Sekondari za Chamwino, Mlowa Barabarani na Msanga.
Shule zingine kutoka halmashauri ya wilaya ya Singida ni shule za msingi Endeshi, Ikumese, Ilongero, Kafanabo, Madamigha, Mghunga, Mtinko na Sekondari za Ilongero, Mtinko na Mwanamwema Shein.
Meneja wa Mradi huo, Karoli Kadege alisema kuwa kuna haja ya kila mdau kuwa na jicho la kijinsia katika kuangalia uandikishaji wa wanafunzi akisisitiza kuwa kila mtoto ana haki ya kupata elimu bila kujali kama ana ulemavu au la.
"Mtoto mwenye ulemavu akisoma anampunguzia mzazi wake majukumu ya kumlea", alisema Kadege huku akiomba wazazi na walezi kuangalia uwezekano wa kuwaendeleza kielimu wanafunzi wanaopata mimba wakiwa shuleni.
Wakichangia hoja hiyo, wadau walisema kuwa kuna haja kwa kila mzazi na mlezi kuhakikisha kuwa mtoto wake anasoma hadi kuhitimu badala ya kuacha jukumu hilo kwa walimu pekee.
Walishauri Wenyeviti wa mitaa na vitongoji kutunza orodha ya wanafunzi wote wanaosoma kwenye maeneo yao na kuwafuatilia kwa karibu ili kuwachukulia hatua wazazi na walezi wanaowaachisha shule kwa ajili ya kuchunga mifugo, kulima au wasichana kupewa mimba na wengine kuozwa.
Social Plugin