Muathirika wa Mikopo Umiza Mwalimu Mstaafu Seleman Haji, akimkabidhi shilingi milioni 46 mke wake Magdalena Gunda baada ya kukabidhiwa na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk .Rehema Nchimbi,
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Rehema Nchimbi, akizungumza na Wajumbe wa Baraza la Madiwani la Manispaa ya Singida (hawapo pichani) baada ya kukabidhi fedha hizo.
Muathirika wa Mikopo Umiza Loth Mwangu, akiwa na fedha zake baada ya kukabidhiwa.
Na Godwin Myovela, Singida
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kwa kasi na mwendelezo ule ule imeendelea kuwafuta machozi wananchi wanyonge mkoani hapa, kwa kuokoa na hatimaye kuwakabidhi fedha taslimu zaidi ya shilingi milioni 80 walizokuwa wametapeliwa kupitia Kampuni za Mikopo zinazoendesha shughuli zake kinyume na utaratibu.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Rehema Nchimbi, amewakabidhi kiasi hicho cha fedha waathirika wote waliopitiwa na wimbi hilo, maarufu ‘Mikopo Umiza,’ mbele ya Wajumbe wa Baraza la Madiwani la Manispaa ya Singida, mkoani hapa juzi.
“Ni Serikali hii ya Magufuli ndio iliyofanikisha kuwabana hawa wakopeshaji haramu na hatimaye leo mnakabidhiwa haki yenu iliyokuwa imeporwa, tuendelee kumshukuru Rais kwa mema haya anayoendelea kutufanyia,” alisema Nchimbi.
Zoezi la urejeshaji wa fedha hizo kwa waathirika limefanyika mbele ya madiwani hao ili kuhamasisha umuhimu wa ushirikiano na utendaji wa pamoja baina yake na Taasisi hiyo katika kupiga vita vitendo vyote vya rushwa, ikizingatiwa madiwani ni miongoni mwa viongozi wanaowajibika kwa karibu zaidi na wananchi.
Akiwasilisha taarifa ya fedha zilizookolewa kutokana na Riba Umiza katika kipindi cha Oktoba na Disemba mwaka huu, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Singida, Adili Elinipenda, alisema takribani shilingi milioni 88.8 zimeokolewa na kurejeshwa kwa wahusika.
Mathalani, mbele ya Mkuu wa Mkoa na Madiwani wa Baraza la Manispaa, Elinipenda alieleza kwamba miongoni mwa matukio yaliyodhibitiwa na Taasisi hiyo katika kipindi cha miezi 3 iliyopita ni pamoja na tukio la kusisimua la mkopeshaji mmoja asiye na vibali vya kufanya biashara hiyo ya ukopeshaji alimkopesha Mwalimu Mstaafu Seleman Haji shilingi milioni 6.5 na baada ya mwalimu huyo kupokea pensheni yake mkopeshaji alimtaka amlipe shilingi milioni 46.
“Takukuru iliingilia kati makubaliano hayo ya kikandamizaji kwa kumtaka mkopeshaji huyo arejeshe shilingi milioni 39.5 na amefanya hivyo. Tunaomba Mkuu wa Mkoa umkabidhi leo hii mstaafu huyu fedha yake iliyookolewa,” alisema Elinipenda.
Hata hivyo matokeo ya ufuatiliaji na udhibiti huo umebaini kuwa baadhi ya wakopeshaji binafsi wanafanya shughuli hiyo bila ya vibali halali, hali inayosababisha kukwepa kodi na hivyo kuikosesha serikali mapato na kujipatia fedha isivyo halali.
Aidha, udhibiti umebaini kuwepo kwa utozaji mkubwa wa riba zisizovumilika za zaidi ya asilimia 100 kinyume na viwango vilivyowekwa na kuainishwa na Benki Kuu.
Aidha, kupitia ripoti hiyo iliyowasilishwa na Takukuru, imeelezwa baadhi ya wakopeshaji hawaandai mikataba ya ukopeshaji, hivyo wakopeshwaji hawana nakala za mikataba, na hata iliyopo kwa baadhi ya kampuni hizo haikidhi sifa na vigezo.
Imeelezwa, baadhi ya kampuni hizi za mikopo hazina hata wataalamu wa mahesabu hali inayowafanya kutoza riba zenye mkanganyiko, na hivyo kujikuta wakimbambikiza riba kubwa mkopeshwaji.
Pamoja na mambo mengine imebainika kuwa kuna uvujishaji mkubwa wa taarifa za watumishi wanaostaafu. Mathalani taratibu za malipo ya mafao ya mstaafu yanapokuwa yamekamilika wakopeshaji wanakuwa wa kwanza kupata taarifa kabla ya mhusika mwenyewe.
Social Plugin