Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MHAGAMA: KAMILISHENI USIMIKAJI WA MFUMO WA VIBALI VYA KAZI KWA WAKATI


Na: Mwandishi Wetu – Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amewataka watendaji wa wizara yake kuhakikisha wanakamilisha mfumo wa vibali vya kazi kwa raia wa kigeni haraka ili kuondokana na changamoto zilizopo katika utoaji wa vibali hivyo.

Kauli hiyo ameitoa Jijini Dodoma Disemba 12, 2020 wakati alipokutana na Menejimenti ya wizara yake na taasisi zilizopo chini ya ofisi hiyo ambapo alieleza kuwa usimikaji wa mfumo wa kielektroniki wa kushughulikia vibali vya kazi itasaidia kuimarisha ushughulikiaji wa maombi ya vibali vya wageni.

“Idara ya Kazi kwa mujibu wa sheria inajukumu la kuratibu ajira za wageni nchini, hivyo kutokana na changamoto zilizopo katika utoaji wa vibali hivyo hivyo suluhisho pekee la kutoa vibali kwa wakati ni kuharakisha mfumo wa kielektroniki ambao utashughulikia vibali vya kazi,” alieleza Waziri Mhagama

Aliongeza kuwa, Mfumo huo wa kielektroniki ambao unaandaliwa utakuwa na manufaa ikiwemo kuongeza ufanisi katika kushughulikia maombi ya vibali vya kazi na kuokoa muda wa kushughulikia maombi ya vibali hivyo.

Aidha, Waziri Mhagama alisisitiza suala la uboreshaji wa sheria za kazi ili ziendane na mfumo huo unaoandaliwa.

“Hakikisheni mnafanya mapitio sheria za kazi kwa kushirikisha wadau ambao wanahusika katika uandaaji wa mfumo huo ili kuboresha utoaji wa huduma katika kushughulikia maombi ya vibali,” alisema Mhagama

Sambamba na hayo, Mheshimiwa Mhagama ameagiza kuwepo na utaratibu wa kushughulikia malalamiko mbalimbali yanayohusu vibali vya kazi ambayo yanatolewa na wadau.

Waziri Mhagama amekutana na Menejimenti ya ofisi yake pamoja na Taasisi zilizopo chini ya ofisi hiyo lengo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipokuwa anafungua Bunge la 12 na pia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi katika kipindi cha Miaka mitano (2020 – 2025).


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com