WAZIRI MKUU AWAONYA WATAALAMU WA UNUNUZI NA UGAVI


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ametoa onyo kali kwa wataalamu wa ununuzi na ugavi ambao bado wanaendekeza vitendo viovu kama rushwa, upendeleo, kuingilia michakato ya ununuzi kwamba waache mara moja kwani Serikali haitomhurumia yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo hivyo.

Waziri Mkuu ametoa onyo hilo leo (Jumatano, Desemba 2, 2020) alipofungua Kongamano la 11 la Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) linalofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC). Kongamano hilo la siku tatu linatarajiwa kufungwa Desemba 4, 2020.

“Mjitahidi kuwa mstari wa mbele kuepuka vitendo viovu vinavyohusishwa na fani hii ya ununuzi na ugavi. Mtambue sheria kali zipo na kwamba Serikali haitakuwa na huruma kwa yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo vya rushwa. ”

Pia, Waziri Mkuu amezitaka taasisi zote zitekeleze maagizo ya Serikali ya kufanya manunuzi kwa njia ya mtandao kwa kupitia mfumo wa kisasa wa manunuzi unaofahamika kwa jina la TANePS, ambao unasaidia kuongeza kasi ya utekelezaji, uwazi, kupunguza gharama na mianya ya rushwa.

Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi zinazolenga kupunguza au kuondoa kabisa uzembe na ukiukwaji wa maadili katika fani ya ununuzi na ugavi kwani pesa nyingi za serikali, zinatumika kupitia taaluma hiyo.

Amesema manunuzi katika utekelezaji wa bajeti ya Serikali ni zaidi ya asilimia 70, hivyo shughuli hiyo isipofanyika kwa kuzingatia weledi ni dhahiri kuwa wananchi hawataweza kupata huduma iliyokusudiwa na miradi haitatekelezwa kwa viwango kusudiwa.

Kufuatia hali hiyo, Waziri Mkuu ameitaka bodi inayosimamia taaluma hiyo ijiridhishe kwamba wataalamu wanaofanya manunuzi wana sifa stahiki na lazima watahiniwe ili kuhakikisha wana viwango na maadili yanayotakiwa.

 “Bodi katika kusimamia weledi wa wataalam wa manunuzi na ugavi ihakikishe inafanya kazi kwa umakini, weledi na uadilifu ili kuhakikisha haki inatendeka bila ya uonevu, pia wakuu wa taasisi wote nchini wawatambue maafisa manunuzi na ugavi kwa kiwango sawa na timu ya menejimenti ili wazishauri taasisi husika ipasavyo.

Waziri Mkuu amewataka wataalamu wa manunuzi na ugavi wahakikishe wanatoa ushauri wa kitaalamu kwa taasisi kwa kuzingatia sheria na taratibu za manunuzi ya umma ili kupata matokeo yenye uthamani wa fedha iliyotumika.

“Simamieni vizuri uandaaji wa mikataba ya manunuzi ili kuepuka nyongeza ya kazi (Variations) na hivyo kuziepusha taasisi katika gharama zilizo nje ya bajeti kwa kuzingatia uwepo wa uwazi katika utayarishaji na utekelezaji wa zabuni ikiwemo kujiepusha na migongano ya kimaslahi au kufuata maelekezo kutoka kwa watu wenye kutaka kufikia malengo binafsi.”

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema amefarijika sana na mada kuu ya kongamano hilo ambayo ni “Wajibu wa Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi Katika Kufikia Ubora wa Juu wa Usimamizi wa Mnyororo wa Ununuzi na Ugavi” kwa lugha nyingine “Reaching Excellence in Procurement Supply Chain and Management)”.

“Mada hii imejikita katika kutambua wajibu wa wataalam wa ununuzi na ugavi katika kufikia ubora wa juu wa usimamizi wa mnyororo wa ununuzi na ugavi. Serikali inatambua umuhimu wa taaluma hii kwani ndiyo wasimamizi wa mnyororo wa ununuzi na ugavi kwa taasisi za umma na sekta binafsi.

Amesema wakati huu ambao Serikali inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati na kuibua miradi mipya katika sekta mbalimbali za kiuchumi, utekelezaji madhubuti wa miradi hiyo unategemea sana weledi na ujuzi wa wataalam hao.

Waziri Mkuu amesema kuwa uzembe na ukosefu wa weledi katika kusimamia mnyororo wa ununuzi na ugavi unachangia kukwamisha utekelezaji wa miradi au kufanyika chini ya kiwango na aghalabu kutokamilika kwa wakati.

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango amesema kila mwaka TSPTB imekuwa ikiandaa kongamano kwa ajili ya kutafakari mwenendo halisi wa ununuzi na ugavi nchini ili kubaini kasoro, msfanikio na kushauri namna ya kuboresha.

Amesema kongamano la mwaka huu litajikita kujadili namna ya kufikia umahiri katika kusimamia mnyororo wote wa ununuzi na ugavi ikiwa ni pamoja na matumizi ya teknolojia, mbinu mpya za kuhakikisha manunuzi yanaendana na thamani ya fedha zilizotumika pamoja na mafanikio na changamoto za kutumia mfumo wa force account.

“Matumaini yangu na Wizara ya Fedha ni kuwa kongamano hili litawatendea haki Watanzania hasa wanyonge, ambao fedha zao zinaibiwa kutokana na udhaifu mkubwa katika manunuzi na ugavi kwenye Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji. Mada ziwasilishwe kwa lugha ya kiswahili ili tuelewane vizuri katika jitihada za kufyeka kichaka cha wizi, ubadhilifu, rushwa na ufisadi kupitia ununuzi na ugavi.”

Waziri Dkt. Mpango amesema Maafisa Ununuzi na Ugavi hawazingatii maadili ya taaluma zao na kwamba uzalendo wao ni wa mashaka, wanatumia utaratibu wa force account kama kichaka cha kuiba, mfano wa bei za vifaa zinazotolewa na Ofisi ya Rais-TAMISEMI zinatumika nchini kote.

“Mlango shilingi 400,000 Uvinza, Dar es Salaam na Mwanza. Bei ya tofali la block shilingi 2,000 inatumika hata pale wanapotumia tofali za udongo za kuchoma, pia bei ya lori la mawe shilingi 180,000 Mwanza, Dodoma, Mbeya, Kisarawe. Hii si sawa kwani hata katika maeneo ambayo vifaa vinapatikana kwa ukaribu bei ilingane na maeneo ambayo vifaa vinapatikana mbali.”

Awali, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi, Godfred Mbanyi alisema Bodi imeandaa kongamano hilo kwa lengo la kuwakutanisha na kuwaleta pamoja wataalamu wa ununuzi na ugavi na wadau wengine ili waweze kujifunza, kujadili na kubadilishana uzoefu katika usimamizi wa mnyororo wa ununuzi na ugavi kwenye maeneo yao ya kazi.

Pia, katika kongamano hilo mada sita zinazotokana na mada kuu isemayo kufikia ubora wa juu katika usimamizi wa mnyororo wa ununuzi na ugavi zitajadiliwa. Ambapo, madhaifu na changamoto zinazojitokeza katika michakato ya manunuzi, zitajadiliwa ikiwa ni pamoja na kuweka maazimio na mikakati ya utatuzi wake ili Serikali iweze kupata thamani ya fedha katika manunuzi yake.

(mwisho)
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMATANO, DESEMBA 2, 2020


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post