Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

JOE BIDEN AAPISHWA KUWA RAIS WA 46 WA MAREKANI..AHUTUBIA TAIFA


Joe Biden amekula kiapo na kuwa rais wa 46 wa taifa la Marekani. Biden amekula kiapo mbele ya jaji wa Mahakama Kuu John Roberts.

Baada ya kula kiapo Biden amelihutubia taifa kwa mara ya kwanza akiwa Rais wa Marekani akisema ''hii ni siku ya kidemokrasia''. Siku ya kihistoria na matumaini.

''Marekani imejaribiwa na kunyanyuka tena dhidi ya changamoto. Leo tunasheherekea ushindi si wa mgombea isipokuwa ushindi wa demokrasia''.

''Ninawashukuru watangulizi wangu wa vyama vyote walio hapa hii leo,'' alisema Rais mpya. Marais wa zamani Clinton, Bush na Obama wamehudhuria sherehe hiyo.

Biden amesema alizungumza kwa njia ya simu na Rais Jimmy Carter- ambaye sasa ana miaka 96, na kumpongeza kwa utumishi wake.

Mtangulizi wake, Donald Trump hajahudhuria tukio hilo muhimu, na hatua hiyo imemfanya kuwa rais wa kwanza kutohudhuria sherehe za kuapa kwa mrithi wake tangu mwaka 1869.
Rais mpya ametangaza msururu wa maagizo yanayolenga kugeuza sera kuu za Bw Trump.

Makamu wa Rais mteule Harris aliapishwa mbele ya Bwana Biden - kuwa mwanamke wa kwanza na mtu wa kwanza mweusi na mwenye asili ya Asia na Amerika aliyeinuliwa kuhudumu katika nafasi ya pili muhimu baada ya Urais.

Shughuli za uapisho zimefanyika wakati kukiwa na ulizi mkali baada ya waandamanaji wanaomuunga mkono Trump kufanya vurugu tarehe 6 mwezi Januari.

Wanajeshi 25,000 wanalinda eneo linalofanyika sherehe hizo, sherehe ambazo zimekosa kuhudhuriwa na maelfu ya watu kama ilivyo desturi yake kwa sababu ya janga la corona.

Kilichofanyika siku ya uapisho
Mapema Jumatano Bw Biden alihudhuria Misa katika kanisa kuu huko Washington - pamoja na viongozi wanne wa baraza kuu la Katoliki, wote wa Democratic na Republican - kabla ya kwenda Capitol.

Akiwa na umri wa miaka 78, Bwana Biden ndiye rais wa Marekani mwenye umri mkubwa zaidi kuwahi kuapishwa.

Makamu wa Rais anayemaliza muda wake Mike Pence pia amehudhuria sherehe hiyo. Hakwenda kwenye hafla ya salamu ya kijeshi ya Bwana Trump katika uwanja wa Andrews.

Awali wasaidizi walisema Bw Biden atatumia hotuba yake kutoa wito wa matumaini wa umoja wa kitaifa baada ya utawala wa mtangulizi wake kutoka chama cha Republican.

Sherehe hizo zilipambwa na watumbuizaji kama vile Lady Gaga- aliyeimba wimbo wa taifa, halikadhalika Jenifer Lopez na Garth Brooks.

Tamasha la jioni litahodhiwa na Tom Hanks na Bruce Springsteen, John Legend, Jon bon Jovi, Justin Timberlake na Demi Lovato.

Je Trump anafanya nini?

Katika hotuba yake katika kambi ya kijeshi ya Andrews Air Force , rais anayeondoka aliangazia kile alichokitaja kuwa ufanisi wa utawala wake kama rais.

Tulichofanya kimefanikiwa kwa kiwango kikubwa, alisema bwana Trump.

Bwana Trump mwenye umri wa miaka 74 aliondoka ili kuanza maisha ya bila urais katika uwanja wa mchezo wa gofu huko Mar-a lago katika ufukwe wa bahari wa Palm Beach.

Katika saa zake za mwisho katika madaraka bwana Trump aliwapatia uhuru zaidi ya watu 140 , akiwemo mshauri wake wa zamani Steve Bannon , ambaye alikabiliwa na mashtaka ya kufanya udanganyifu.

Je historia itamkumbuka vipi Trump?
Matukio ya kisiasa yanayomzunguka hayajaisha. Bunge la Seneti linatarajiwa kumshtaki kufuatia kushtakiwa na bunge la uwakilishi kwa mara ya pili kwa kuchochea ghasia za Capitol.

Siku ya Jumanne , Kiongozi wa Republican katika bunge la seneti Mitch McConell , alisema kwamba waandamanaji hao walichochewa na rais Trump na kuambiwa uongo.

Je Biden atafanya nini katika siku yake ya kwanza?
Bwana Biden ametoa maagizo mengi ya urais. Katika taarifa yake siku ya Jumatano , alisema kwamba atatia saini maagizo 15 baada ya kuapishwa.

Watabadilisha hatua ya rais Trump kuindoa Marekani katika mkataba wa mazingira wa paris.
Kufutilia mbali cheti cha kuruhusu kampuni ya mabomba ya Keystone XL Pipeline , ambayo inapingwa na wanamazingira na makundi ya Wamarekani asilia.

Kufutilia mbali sera ya Trump kuhusu uhamiaji na fedha za dharura zilizosaidia kujenga Ukuta wa Mexico mpakani.

Kuwataka watu wavalie barakoa mbali na kukaa mbalimbali miongoni mwa wafanyakazi wa majimbo, pamoja na ofisi ya Ikulu kutokana na virusi vya corona.Mipango ya uongozi wa Biden huenda ikaathiriwa na idadi ya wabunge alionao katika bunge la seneti pamoja na bunge la uwakilishi.

Siku ya Jumanne , Bwana Biden alitoa hotuba katika jimbo lake la nyumbani huko Delaware , akiwaambia waandishi wa habari kuwa ,'' hizi ni siku mbaya , lakini kuna nuru'' , kabla ya kuelekea Washington .

CHANZO - BBC SWAHILI

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com