Mbunge wa Jimbo la Kishapu Mhe. Boniphace Butondo mwenye nguo za bluu akishiriki ujenzi wa madarasa
**
Mbunge wa Jimbo la Kishapu Mhe. Boniphace Butondo amewapongeza wananchi kwa nguvu kazi na michango ya fedha kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na maabara wilayani Kishapu mkoa wa Shinyanga.
Mhe. Butondo ametoa pongezi hizo alipokuwa kwenye ziara yake ya siku mbili Jimboni humo ambapo alizindua kamati ya mfuko wa Jimbo na kutambulisha kikao cha kwanza kupitia mwenyekiti wa mfuko huo.
Kikao hicho kiliazimia kutoa fedha kwa ajili ya kufunga mkono miradi ya maendeleo iliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi hasa maabara na madarasa kwa lengo la kutekeleza agizo la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa la kuongeza Madarasa ili ifikapo Februari 2021 wanafunzi wapate mazingira mazuri ya kujisomea.
Katika ziara yake alitembelea tarafa ya Kishapu, Negezi na Mondo ambapo jumla ya miradi ya maendeleo 15 wilayani Kishapu imenufaika na mfuko huo wa Jimbo huku jumla ya kiasi cha fedha Tsh. Milioni 42, 612,000/= kilitolewa na Mhe. Butondo kupitia mfuko wa Jimbo.
Fedha hizo zitaenda kukamilisha ujenzi wa madarasa na maabara ambayo yameanzishwa kwa nguvu za wananchi ikiwa ni kuunga mkono jitihada za serikali ya awamu ya tano elimu bure.
Aidha, Mhe. Butondo ameunga mkono mradi wa Ujenzi wa Ofisi ya Makao Makuu ya Polisi Wilaya ya Kishapu iliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi.
Kadhalika, Mhe. Butondo amepongeza na kuwashukuru a wananchi wa Jimbo la Kishapu kwa kuwachagua kwa kushindo Rais, Wabunge na madiwani katika uchaguzi Mkuu uliopita na kuahidi kuwatumikia kwa nguvu zote.
"Wananchi wa Jimbo la Kishapu mlinichagua kwa kuwa mna imani na Mimi, naomba tushirikiane ili kwa pamoja tuweze kujiletea maendeleo katika Jimbo letu, namba tushikane mkono hasa katika mradi mkakati huu wa ujenzi wa vyumba vya madarasa ili watoto wetu wapate elimu kwenye mazingira rafiki", alisema Butondo.
Aidha, Mbunge huyo amewaasa viongozi wa ngazi zote kuanzia kata, vijiji na vitongoji kusoma taarifa za mapato na matumizi kwa wananchi kupitia vikao na mikutano ya hadhara kwani kufanya hivyo kutawajengea uaminifu na wananchi wao.
Katika ziara hiyo alisisitiza pia suala la usimamizi wa thamani ya fedha kutokana na utekelezaji wa miradi na kuwataka wataalamu ngazi ya Halmashauri kusimamia ujenzi uwe katika kiwango kinachotakiwa ili miradi hii iweze kudumu muda mrefu.
Mbunge wa Jimbo la Kishapu Mhe. Boniphace Butondo mwenye nguo za bluu akishiriki ujenzi wa madarasa
Social Plugin