Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA GEOFFREY MWAMBE ATAKA WAHITIMU CBE WAJIENDELEZE KIELIMU


Waziri wa Viwanda na Biashara Geoffrey Mwambe akizungumza kwenye mahafali ya 13 ya Chuo Cha Biashara (CBE) Kampasi ya Mwanza Januari 16 2021

Na Hellen Mtereko Mwanza

Waziri wa Viwanda na Biashara Geoffrey Mwambe amewataka wahitimu wa Chuo Cha Biashara (CBE) kuhakikisha wanajiendeleza kielimu katika ngazi tofauti na kuwa wabunifu ili kuacha dhana ya kuajiriwa.

Hayo aliyasema jana Januari 16 2021 wakati akizungumza kwenye  mahafali ya 13 ya chuo hicho kampasi ya Mwanza. 

Mwambe alisema wahitimu wenye Diploma wajiendeleze ili wafike ngazi ya Stashahada ili kuweza kuwa na nchi yenye wasomi watakaokuja kusaidia taifa.

Aliwataka wahitimu kutumia utalamu wao walioupata  kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii .

 Aliomba mashirika binafsi na ya Serikali yalete  wafanyakazi wao  ili waweze kupata Elimu katika chuo hicho. 

Aidha alisema Serikali itaboresha miundombinu ya Elimu katika vyuo vya CBE nchini kutokana na ongezeko la Wanafunzi wenye uhitaji wa kujiendeleza na sera ya Elimu bure inayoendelea kuinua wasomi wengi.

Aliiomba CBE kuhakikisha inafungua kampasi katika maeneo ya nyanda za Kaskazini na Kusini(Ruvuma/Lindi na Mtwara). 

Pia alikiagiza Chuo hicho kuhakikisha kinakuja na mkakati  wa Kukuza Ujasiriamali ili kupata wafanya biashara wenye Elimu na ujuzi kutoka chuoni hapo.

Mkuu wa Chuo cha CBE,Kampasi ya Mwanza Profesa Emmanuel Mjema alisema jumla ya wahitimu 447 wamehitimu katika ngazi tofauti. 

Mjema alisema chuo chao kipo katika mkakati wa kuweza kuanzisha kozi mpya ya Stashahada ya masoko na Utalii ili kwendana na kasi iliyopo.

Alisema Chuo chao kipo kwenye mkakati wa kuanzisha chuo  katika mkoa wa Iringa na Zanzibar kutokana na maombi mengi anayopokea kutoka kwa wananchi wenye kufahamu umuhimu wa Elimu.

Aliipongeza Serikali kwa kuwezesha kuongeza bajeti ya mikopo kwa Elimu ya juu ambapo na Chuo chao kimenufaika pia  ameipongeza Serikali kwa kuwalipia fedha za kununua eneo la chuo hicho katika eneo la Kangae mkoani Mwanza

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com