TCRA YATOA ONYO KWA WANAORUSHA MATANGAZO YA RUNINGA KWA NJIA YA WAYA 'CABLE TV'


Mkuu wa TCRA Kanda ya Ziwa, Mhandinsi Francis Mihayo (katikati) akizungumza kwenye kikao hicho kilichofanyika jijini Mwanza kikiwashirikisha warusha matangazo kwa njia ya waya 'Cable TV' kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa.
***
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewaonya warusha matangazo ya runinga kwa njia ya waya 'Cable TV' kurusha matangazo mbalimbali ikiwemo mpira pamoja na tamthilia kutoka kwenye chaneli za kulipia bila kuwa na kibali kutoka kwa wamiliki wa chaneli hizo.

Mkuu wa TCRA Kanda ya Ziwa, Mhandinsi Francis Mihayo alitoa onyo hilo Januari 13, 2021 kwenye kikao baina ya mamlaka hiyo na wamiliki wa 'Cable TV' na wadau wengine ikiwemo shirikisho la soka Tanzania (TFF) pamoja na warusha matangazo kupitia visimbuzi vya kulipia.

Mhandisi Mihayo alisema watoa huduma za matangazo kwa njia ya waya 'Cable TV" hawaruhusiwi kurusha matangazo kutoka kwenye chaneli za kulipia bila kuwa na kibali kutoka kwa makampuni yaliyopewa haki miliki ya matangazo hayo kama vile Azam Media, Multchoice/ DSTV, Zuku, Star Times.

Alibainisha kuwa hapo awali kulikuwa na ukiukwaji wa sheria kwa 'Cable TV' kurusha matangazo kutoka kwenye chaneli za kulipia (Pay TV) ambapo ni kinyume pia na leseni yao inayowataka kurusha matangazo kutoka kwenye chaneli za bure (Free to Air) hivyo kikao hicho kitasaidia watoa huduma hao kufanya kazi kwa kufuata sheria ya haki miliki ya mwaka 1999 na kanuni zake.

Nao baadhi ya warusha matangazo kwa njia ya waya 'Cable TV' walilalamikia adha wanayoipata kwa kurusha chaneli za bure kutoka nje ya nchi na kushauri TCRA kuondoa mkanganyiko huo kwani leseni yao inawaruhusu kurusha chaneli za bure ambapo wamekuwa wakiitwa majina yasiyofaa 'maharamia' wakati wanafanya shughuli zao kwa kuzingatia sheria.

Via BMB Blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post