Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DC MBONEKO AINGILIA SAKATA LA ANAYEUGUZA MGONJWA KUPIGWA NA MLINZI HOSPITALI YA MKOA WA SHINYANGA...ATOA MAAGIZO

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko akiondoka katika Wodi ya Wanawake katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga baada ya kumaliza kuendesha kikao cha kujadili tukio la Mlinzi wa Kampuni ya Suma JKT Guard, Geofrey Paul anayetuhumiwa kumpiga Daudi Lefi aliyekuwa akifuatilia dawa za mama yake aliyelazwa hospitalini hapo.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko akizungumza katika kikao kuhusu tukio la mlinzi kupiga mwananchi aliyekuwa anahudumia mgonjwa wake katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.
Mlinzi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga Gofrey Paul akimshambulia Daudi Lefi kama inavyoonekana kwenye video ya tukio hilo iliyosambaa mtandaoni. 

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko ameiagiza Kampuni ya Ulinzi ya Suma JKT Guard kumuondoa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga na kutopangiwa lindo lolote mkoani Shinyanga Mlinzi wake Geofrey Paul anayetuhumiwa kumpiga Daudi Lefi (45) aliyekuwa akifuatilia dawa za mama yake aliyelazwa hospitalini hapo. 

Mbali na kuagiza kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa mlinzi huyo Mboneko pia ameitaka Kampuni hiyo kuwaondoa hospitalini hapo walinzi wanaolalamikiwa kuonea na kutumia lugha mbaya kwa wananchi wanaofika hospitalini.

Mboneko amechukua uamuzi huo leo Jumamosi Januari 23,2021 wakati akiongoza kikao cha kujadili kuhusu tukio hilo lililotokea katika hospitali hiyo Januari 22,2021 kilichodumu takribani saa tatu kilichohudhuriwa na wajumbe wa kamati ya Ulinzi na Usalama wilaya ya Shinyanga, Uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Shinyanga pamoja na Viongozi wa Kampuni ya Ulinzi ya Suma JKT Guard. 

Mboneko amesema viongozi wa serikali waliona taarifa ya tukio kupitia mitandao ya kijamii na kuanza kuchukua hatua mara moja ili kubaini ukweli kuhusu tukio hilo ambapo amevipongeza na kuvishukuru vyombo vya habari vilivyoripoti kuhusu tukio hilo. 

“Tumeona tukio hili kupitia mitandao ya kijamii, kama uongozi wa serikali hatukufurahishwa na jambo hili,baada ya kuona tukio hili tulianza kupata ufafanuzi kutoka hospitalini lakini pia nilimuagiza Mkuu wa Polisi wilaya ya Shinyanga kwa ajili ya kufuatilia tukio hili ambapo tayari hospitali walikuwa wameshaanza kuchukua hatua. Kwa hiyo ikapendeza kuwa leo Jumamosi tufanye kikao kujadili tukio hili, pia tuwaita wahusika kwa maana ya yule kijana aliyepigwa bwana Daudi Lefi na Mlinzi Geodfrey Paul aliyekuwa akimpiga, tumepata ufafanuzi kutoka pande zote mbili, uongozi wa hospitali na kiongozi wa Suma JKT Guard kanda ya Ziwa kwamba ni hatua gani wamechukua”,ameeleza Mboneko. 

"Kwa sababu tuko na mkataba na Suma JKT Guard na tukio hili limetokea kwa mara ya kwanza kutokea,tumewapa nafasi ya kutafuta walinzi wazuri wawalete na tumewaambia kwamba hatutaki kusikia tukio jingine likihusisha walinzi kuharibu taswira ya hospitali yetu. Kwa hiyo kuanzia sasa nimewaambia warekebishe", amesema. 

Amesema serikali inakemea jambo hilo na isingependa kuona linaendelea mahali popote penye hospitali zetu, zahanati na vituo vya afya na sehemu zingine na kwamba serikali inataka watu wapate huduma nzuri hospitalini. 

“Jambo hili limetokea baada ya watu hawa kupishana lugha lakini nimewaelekeza SUMA JKT Guard na Idara ya afya wahakikishe wanatoa elimu kwa watoa huduma hospitalini na walinzi wanaolinda hospitali kuhusu namna ya kuhudumia watu,namna ya kuzungumza na watu kama huyu changamoto yake ilikuwa ni kumhudumia mama yake zaidi alitakiwa kuelimishwa kuliko kupigwa”,amesema Mboneko. 

Amesema wamelikemea jambo hilo na kumwelekeza kiongozi wa SUMA JKT Guard Kanda kuchukua za kinidhamu mara moja juu ya mtumishi wao na watuletee maandishi ofisini kwangu kuhusu hatua za kinidhamu walizochukua. 

“Lakini SUMA JKT Guard wamesema wameshachukua hatua ya kumuondoa hospitalini mtumishi wao, na sisi tunasema sawa sawa. Lakini nataka na wale wote walinzi wote wanaolalamikiwa kuwa na kauli mbaya kwenye Geti letu,kwenye mapokezi pale lakini pia kwenye kuondoa watu wanaokuja kuona wagonjwa. Nimewaelekeza wawaelimishe kuliko kufukuza watu utadhani wamekuja kuiba. 

“Waliopo hapa hospitalini wanahitaji faraja zaidi, wanahitaji upendo,wamekuja kuhudumia ndugu zao lakini pia wanatoka maeneo tofauti tofauti,pengine hawana ndugu hapa Shinyanga kwa hiyo muda anaopata yeye anakuja kuhudumia mgonjwa,akija pale mtu akajieleza,asikilizwe,apewe fursa ili apate kuhudumia mgonjwa wake kwani wengine wanakuja mbio mbio baada ya hali ya wagonjwa wao kubadilika”,ameongeza Mboneko. 

Mkuu huyo wa wilaya pia amesisitiza watoa huduma na Walinzi wa hospitali kudhibiti kauli mbaya na kuepuka vijembe wa wagonjwa na watu wanaohudumia au kuona wagonjwa huku akiwataka viongozi wa hospitali kuhakikisha wanachukua hatua dhidi ya malalamiko yanayotolewa. 

“Lakini pia nimewaelekeza kutoa namba za viongozi wa hospitali na nimeelekeza pia namba zangu ziwekwe ili wananchi waweze kutoa maoni na malalamiko yao,zionekane sehemu za kuingilia, kutoka na hata kwenye wodi wanazolala wagonjwa”,amesema. 

Amewataka walinzi kutumia muda mwingi kusaidia wananchi kuwaelimisha badala ya kuwapiga na kuwatolea lugha chafu ili watoa huduma nao wapate muda mzuri wa kuhudumia wateja wao na wanaotembelea wagonjwa wapate muda wa kufariji wagonjwa. 

Amesema lengo la serikali ni kuona kila mwananchi anafurahishwa na huduma zinazotolewa kwenye vituo vya afya kwani serikali inataka kuona wananchi wanapata huduma nzuri,bora na wanakuja salama na kuondoka salama wasipate taharuki yoyote. 

“Hatutaki taharuki hospitali, hatutaki misongamano hospitali. Tunataka watu waje kuhudumiwa na sisi tutaendelea kusimamia maboresho ya hospitali yetu. 

"Tulikuwa tumepokea pia malalamiko ya watu wanakaa muda mrefu bila kuhudumiwa kutokana na foleni kwenye eneo la Control number,Mapokezi kote huko nataka waboreshe,waweke walau watu wawili wawili ili kurahisisha huduma, mtu akija atumie muda mfupi aondoke akafanye shughuli zingine za kiuchumi na kijamii”,amesema Mboneko. 

Aidha amesema hataki kuona wala kusikia watumishi wa hospitali,zahanati na vituo vya afya wanafanya kazi huku wakichati nyakati za kazi badala yake watumie muda wao kuhudumia wagonjwa na kwamba hataki kusikia mgonjwa anatoka hospitali bila kupata dawa akiambia akanunue kwenye maduka ya dawa. 

Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Nuru Mpuya amesema tukio hilo lilizua taharuki hospitalini na kwamba tayari hatua zimeshachukulia na kuahidi kuwa tukio kama hilo lililofanywa na mlinzi wa Kampuni ya walinzi waliyoingia nayo mkataba halitatokea na kwamba wataboresha huduma ikiwa ni pamoja na kuwapa elimu walinzi hao. 

Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Shinyanga, Dkt. Luzila John Boshi amesema uongozi wa hospitali umesikitishwa na tukio hilo na kwamba kinachofuata ni kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko. 

Meneja wa Kampuni ya Ulinzi ya Suma JKT Guard Kanda ya Ziwa, Captain Manika Kihiri amesema mara baada ya kutokea kwa tukio hilo,hatua za awali walizochukua ni kumuondoa mlinzi huyo eneo la hospitali na kwamba watatekeleza maagizo yaliyotolewa na Mkuu wa wilaya ya Shinyanga na ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua za kinidhamu kwani Suma JKT haipo kwa ajili ya kuzua taharuki katika jamii bali ni kuleta amani katika jamii. 

Tukio hilo limetokea Ijumaa Januari 22,2020 majira ya saa 11 na dakika 45 jioni wakati Daudi Lefi (45) akiwa katika wodi ya wanawake namba 1 ambako mama yake mzazi Victoria Lugano Mwakagari amelazwa hospitalini hapo alishambuliwa kwa kupigwa mkanda sehemu mbalimbali za mwili wake na mlinzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga kutoka Kampuni ya Ulinzi ya Suma JKT Guard Geofrey Paul akimtaka aondoke wodini kwamba muda wa kusalimia wagonjwa umeisha. 

Akisimulia kuhusu tukio hilo, ndugu wa kijana huyo Lydia Lefi aliiambia Malunde 1 blog kuwa kaka yake alikutwa na mkasa huo wakati akiwa katika harakati za kulipia dawa za mama yao ambaye amelazwa katika hospitali hiyo Januari 21,2021 lakini jina lilikuwa halionekani kwenye Computer. 

“Kaka alikuwa alipie dawa, alipewa karatasi ya kwenda kulipia dawa, alipoenda kufuata Control number ili alipie, jina likawa halionekani kwenye Computer, ikabidi aende wodini kwa mgonjwa kuangalia/kuulizia amesajiliwa kwa jina gani,akiwa wodini hao walinzi ndipo walipoingia wodini na kumtaka aondoke kwamba muda umekwisha. 

"Walivyomtaka aondoke wodini akawaambia amekuja kuangalia jina gani mgonjwa ameandikishwa, wale walinzi wakamwambia aondoke muda huo huo, akawaomba lakini wakamwambia Huwezi kutupangia kazi. Kaka akasema nitaondokaje mama hajapata huduma ,wale walinzi wakaanza kumsukuma, ndipo mlinzi mmoja akachomoa mkanda wa suruali na kuanza kumshambulia huku mwingine akimsukuma, wakati purukushani zikiendelea baadae akaja mlinzi wa kike akasogea na kuwaachanisha”,ameeleza Lydia. 

Naye Daudi Lefi alisema mlinzi huyo alidhani amefika muda huo huo hospitalini wakati yeye alikuwa amefika hospitalini hapo muda mrefu lakini Computer za Hospitali zikawa hazisomi jina la mgonjwa wake wakati anataka kununua dawa. 

"Sikurusha ngumi kupigana kwa sababu ni eneo la hospitali, wangesema nimeenda kufanya vurugu. Walionishambulia walikuwa wawili lakini mmoja ndiyo aliyeanza kwa kunichapa na mkanda akisema nitamtambua kuwa yeye ni nani huku akinitukana,nami nikamsihi aache kutumia lugha chafu eneo la kazi",alisema Daudi. 

"Hayo yote yametokea wakati nikimweleza kuwa nimefika wodini kuulizia ndugu zangu na mgonjwa kuwa wameandikisha jina gani mapokezi kwani jina halionekani mapokezi ili nilipie dawa,wakati naendelea kushambuliwa nikamuona mama yangu mgonjwa akitoka wodini huku akihema presha imepanda akifuatilia nini kinaendelea ndipo nikaanza tena kumrudisha wodini kumhudumia nikaulizia jina aliloandikisha nikaenda kuchukua dawa nikamletea wodini", alieleza Daudi. 

Daudi alisema kutokana na kipigo hicho ameumia mkono wa kushoto ambao umevimba na kuchanika kwenye kiwiko.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko akizungumza katika kikao kuhusu tukio la mlinzi kupiga mwananchi aliyekuwa anahudumia mgonjwa wake katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko akizungumza katika kikao kuhusu tukio la mlinzi kupiga mwananchi aliyekuwa anahudumia mgonjwa wake katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.
Wajumbe wakiwa kwenye kikao hicho.
Meneja wa Kampuni ya Ulinzi ya Suma JKT Guard Kanda ya Ziwa, Captain Manika Kihiri akizungumza katika kikao hicho na kueleza hatua za kinidhamu zilizochukuliwa na kampuni hiyo juu ya mlinzi aliyepiga mwananchi katika hospitali ya mkoa wa Shinyanga.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko akiingia katika wodi ya wanawake katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga kwa ajili ya kumjulia hali mama ambaye mwanaye alipigwa na mlinzi hospitalini hapo.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko akiwa ndani ya wodi ya wanawake katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko akiondoka katika wodi ya wanawake katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko akiondoka katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.

Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

TAZAMA VIDEO HAPA CHINI


Soma pia : APIGWA NA WALINZI WA HOSPITALI YA RUFAA MKOA WA SHINYANGA AKIHUDUMIA MAMA YAKE WODINI..Tazama Video 



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com