Mnyama Fisi
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Watu wawili wa familia moja wamenusurika kufa baada ya kushambuliwa na mnyama fisi aliyevamia banda la kuku na wao kutoka kwenda kuokoa kuku wao na mifugo mingine katika kitongoji cha Nyambiti, kijiji cha Kilimawe, kata ya Mwantini,wilaya ya Shinyanga mkoani Shinyanga.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba amesema tukio hilo limetokea Januari 11,2021 maji ya majira ya saa kumi kamili alfajiri katika kijiji cha Kilimawe, kata ya Mwantini wilaya ya Shinyanga.
Amewataja walioshambuliwa na fisi kuwa ni Mabuga Ndakuna (70), na Timotheo Mabuga (17) wote wakazi wa Kilimawe ambapo walijeruhiwa kwa kung'atwa na fisi sehemu mbalimbali za miili yao.
“Mabuga Ndakuna aling'atwa na kujeruhiwa sehemu za kichwani upande wa kulia na kuvunjwa mkono wa kushoto na kujeruhi mkono wa kulia, miguuni na mapajani na kwenye makalio wakati Timotheo Mabuga aling'atwa na kujeruhiwa mkono wa kulia karibu na kifundo cha mkono, mkono wa kulia karibu na bega na paja la kushoto”,ameeleza Kamanda Magiligimba.
Amesema chanzo cha tukio hilo ni baada ya mnyama fisi huyo kuvamia banda la kuku na wanafamilia hao kutoka kwenda kuokoa kuku wao na mifugo mingine na kupelekea kushambulia na fisi huyo.
Amesema majeruhi hao wanatibiwa katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Shinyanga.
“Fisi huyo alikimbilia vichakani na juhudi za kuwatafuta na kuwaondoa wanyama wakali katika eneo zinafanyika kwa kushirikiana na maafisa wa wanyapori”,ameongeza Kamanda Magiligimba.