Simu za mkononi ni nyenzo muhimu katika kurahisisha mawasiliano, lakini matumizi yasiyo sahihi ya simu hizo yanaweza kuleta athari kwa mtumiaji.
Kwa mujibu wa watalamu kupitia utafiti, mionzi aina ya `ultra violate’ iliyopo kwenye simu inaweza kumletea athari mtumiaji endapo ataitumia au kuitunza kwa njia isiyokuwa sahihi.
Akizungumza na Mwananchi, Dk Annely Godable alisema nguvu ya mionzi inayotokea wakati simu inapokelewa ni kubwa hivyo si sahihi kuipokea ikiwa sikioni.
Dk Godable ambaye ni miongoni mwa wanasayansi wa Afrika Mashariki waliofanya utafiti kuhusu matumizi ya simu kupitia taasisi ya `Wema Ministry Association’, anaonya kuhusu athari za mionzi mwilini pale simu inapokuwa sikioni, kulala nayo kitandani, kuitumia ikiwa kwenye chaji, kuiweka kifuani, kuweka kwenye mfuko wa nguo, kuishikilia simu kwa kutumia bega wakati ukiendelea kuzungumza.
Matumizi mengine yasiyo sahihi ni kugeuza simu na kusikilizia upande wa spika, kuiweka sikioni muda wote kama wafanyavyo waendesha bodaboda kwa kuibana kwenye helmeti, kusikiliza muziki wa kwenye simu kwa muda mrefu kwa kutumia vifaa vya kusikilizia (hearphones) na kutumia simu jirani na vifaa vya umeme au moto.
‘‘Ikitokea simu inatumika isivyo sahihi mionzi hiyo itaingia kwenye mwili na mtumiaji na upo uwezekano wa kumsababishia kupata saratani ya ubongo, tezi dume, kuharibu uzalishaji wa mbegu za kiume, kuathiri kiumbe kilichopo tumboni kwa mjamzito, kupunguza nguvu za kiume na kumuondolea mwanamke hamu ya tendo la ndoa,’’ alisema.
Via Mwananchi