Na William Budoya, Afisa Habari Mkuu,
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Katavi
Hewa
ya ukaa ni biashara poa na inalipa. Kazi kubwa unayotakiwa kufanya ili uweze
kufanya biashara hii ni kuhifadhi mistu ya asili iliyo katika eneo lako na
kutunza mazingira yako. Misitu ya asili ina uwezo mkubwa wa kufyonza na
kuhifadhi hewa ya ukaa na hewa sumu.
Ukiwa
na misitu hii lazima uzuie uharibifu wa misitu mfano kukata miti, kufyeka miti,
kuchoma misitu na kufanya shughuli zingine hatarishi kwa uhifadhi wa misitu na
kupanda miti mbali mbali katika maeneo yetu. Ukiweza kufanya hayo lazima
utakuwa na uhakika wa kuvuna hewa ya
ukaa na kufanya biashara ya hewa ya ukaa.
Pengine
unaweza kujiuliza, je biashara hii ni kama biashara ya mahindi au biashara nyingine?
Kwamba mtu anaweza kupanda na kuvuna mahindi na kuuza sokoni? Hapana sivyo.
Katika biashara hii mwenye biashara anatakiwa kuhifadhi misitu asili iliyo
katika eneo lake. Aidha akishafanya uhifadhi huo basi, Carbon Tanzania watamtafutia
wateja duniani wa kutoa ruzuku kwa uhifadhi huo.
Biashara
hii imeshaingia katika Mkoa wa Katavi, Wilaya ya Tanganyika katika Halmashauri
ya Wilaya ya Tanganyika. Wananchi 21,000 katika vijiji 8 walio katika Halmashauri
ya Wilaya ya Tanganyika, wamenufaika na mradi wa hewa ya ukaa baada ya kuivuna
hewa hiyo na kupewa kiasi cha shilingi 380,000,000/= na Carbon Tanzania chini
ya mradi uitwao NTAKATA MOUNTAINS REDD Plus PROJECT.
Wananchi
katika Wilaya hiyo wamezuia uharibifu wa misitu waliyoihifadhi ili iwasaide
kutunza mazingira pamoja na mambo mengine kufyonza hewa ya ukaa na hewa sumu iliyo
katika la anga la nchi yetu na nje ya nchi. Kwa kufanya hivyo, wananchi katika
Wilaya hiyo wametengeneza biashara ya kuuza hewa ya ukaa.
Kwa
ufafanuzi, vijiji hivyo vimevuna jumla ya tani 82,000 za hewa ya ukaa na
kuiuza kwa thamani ya shilingi
250,000,000/=. Hata hivyo pamoja na uvunaji wa tani hizo, mauzo yake
hayajafikia hata nusu ya tani 270 ambazo hazijauzwa bado.
Aidha
12/11/2020 na 2/5/2020 kiasi cha fedha 130,000,000/= zilitolewa kama motisha na
wadau mbali mbali wa hifadhi kwa vijiji kabla ya kupata wateja na vyeti vya uuzaji wa hewa ya ukaa na kugawanywa
kulingana na makubaliano ya mradi. Makubaliano hayo yanabainisha kuwa 10% ya
fedha zinazopatikana zinaenda kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika ili
kugharimia shughuli za usimamizi wakati 90% zinapaswa kugawiwa kwenye vijiji
vilivyo katika mradi ambao unakadiriwa kuwa na hekta 230 katika msitu wa Tongwe
Magharibi.
Fedha
hizo zilizopatikana zitasaidia kuleta maendelao ya kijamii na kiuchumi kwa
wananchi mfano ujenzi wa madarasa na utengenezaji wa madawati, kujenga vituo
vya Afya na kuwaletea wananchi nishati ya umeme.
Katika
misitu hiyo kuna utajiri mkubwa, inaelezewa kuwa ikiwa hewa ya ukaa itauzwa kwa
wingi na ukamilifu wake uliopo katika misitu ya vijiji hivyo, basi kuna
uwezekano wa kupata kiasi cha 6,000,000,000/-. Wananchi wanatakiwa kuendelea
kuhifadhi misitu na kutunza mazingira. Miti isikatwe ovyo wala kuchomwa, waepuke
kilimo cha kuhamahama na ufugaji usiozingatia tija.
Kwa
kuvitaja, vijiji vilivyonufaika na mauzo ya hewa ya ukaa, ni Lugonesi, Mwese,
Lwega na Bujombe. Aidha vijiji vingine vilivyo katika mradi wa mauzo ya hewa ya
ukaa ni Kapanga, Mpembe, Kagunga na Katuma. Baadhi ya vijiji hivyo viko katika
Kata ya Mwese, Tarafa ya Mwese na vijiji vingine viko Kata ya Kasekese.
Carbon
Tanzania ndio taasisi inayowezesha vijiji hivyo kupata masoko ya hewa ya ukaa
ipatikanayo katika misitu ya hifadhi za vijiji na maeneo ya malisho.
Je,
biashara hii imeanzaje? Biashara hii imeanza baada ya vijiji 8 kuwekwa kwenye
mpango wa matumizi bora ya ardhi. Matumizi bora ya ardhi ni nini? Ni uwezo wa
wananchi kujipangia namna ya kutumia ardhi yao kwa faida yao. Kwa mantiki hiyo,
wananchi katika vijiji hivyo wamejipangia ardhi yao kwa mahitaji mbali mbali
mfano kutenga maeneo kwajili ya kilimo, makazi, malisho na maeneo mengine
kuyaacha kwa ajili ya uhifadhi misitu kwa ajili ya kuvuna na kuuza hewa ya
ukaa. Matumizi bora ya ardhi ndio chanzo
cha mradi wa hewa ya ukaa . Wananchi wametenga maeneo ya hifadhi ya misiti na
kuyaacha maeneo hayo kwa ajili biashara ya hewa ya ukaa. Mradi huu,
unaokadiriwa kuwa na hekta 230, unajulikana kama NTAKATA MOUNTAINS REDD Plus
PROJECT, ambao uko chini ya usimamizi wa Carbon Tanzania.
Malengo
ya mradi huu ni kuhifadhi misitu ya asili na mazingira, kulinda na
kuhifadhi bionuai zote muhimu hasa
zilizo hatarini kutoweka kama Sokwe, kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, kutunza
vyanzo vya maji, kutunza wanyamapori na kuwawezesha wananchi , walio katika
vijiji venye uhifadhi wa misitu asili, kufanya shughuli za maendeleo yao katika
vijiji vyao kupitia mauzo ya hewa ya ukaa.
Mashuleni tunafundishwa kuwa hewa ya ukaa al
maaarufu kama C02, ni muungano wa atomi 1 ya kaboni na atomi 2 za Oksijeni
hutengeneza hewa ya ukaa(C02). Sisi binadamu hupumua hewa ya ukaa na baadaye hewa hiyo hufyonzwa na miti na
kuhifadhiwa kwenye miti na ardhini. Aidha sisi binadamu huvuta hewa ya oksijeni
kutoka kwenye mimea. Kwa asili hewa ya
ukaa ni miongoni mwa gesi zilizopo angani. Hewa kwa kawaida ina gesi mbali
mbali ikiwemo hewa ya ukaa.
Hewa
ya ukaa ni hewa chafu zinazozalishwa na shughuli mbali mbali za mwanadamu. Uzalishaji
mkubwa wa kaboni angani huchochea athari ya jopogesi na kusababisha mabadiliko
ya tabia ya nchi. Ongezeko la viwango vya hewa ya ukaa na gesi nyingine angani
zinazotokana na shughuli za binadamu husababisha kiwango cha joto duniani
kuongezeka.
Mabadiliko
haya yana maana gani? Mabadiliko haya yana maana ya kuongezeka kwa jotoridi, kuwa
na misimu ya mvua isiyoaminika, kupata mvua chache, utabiri wa majira kuwa
mgumu, makali ya ukame na mafuriko kuzidi, mvua kunyesha nje ya misimu
iliyozoeleka. Aidha kuna athari katika kilimo, uzalishaji wa chakula kupungua
kwa sababu ya uhaba wa mvua na ongezeko kubwa la joto, milipuko ya magonjwa na
wadudu waharibifu wa mazao waweza kusambaa hata maeneo ambayo hawakuwemo awali.
Ongezeko la joto duniani limesababisha kuyeyuka kwa theluji katika ncha za
duniani ambayo inasababisha ongezeko la kima cha bahari.
Binadamu
nao huongeza hewa ya ukaa angani kwa kasi zaidi kuliko uwezo wa dunia kufyonza
gesi hii. Uchomaji wa mimea husababisha hewa ya ukaa kwenda angani katika hali
ya moshi, ukataji wa misitu kwa sababu mbali mbali hupunguza uwezo wa ardhi
kuhifadhi hewa ya ukaa, tunapochoma mafuta, kuendesha magari yetu na wakati wa
kuzalisha umeme.
Hali
hiyo ni hatari kwa maisha ya mwanadamu. Sasa tunafanyaje ili kukabiliana na
mabadiliko ya tabia nchi?
Watalaam
wamefanya tafiti na kubaini kuwa njia pekee inayoweza kukabiliana na mabadiliko
ya tabia nchi ni uhifadhi wa misitu ya asili. Misitu ya asili ina uwezo mkubwa
wa kutumia hewa ya ukaa na hewa sumu kama chakula chake. Miongoni mwa vyakula
ambavyo miti hutumia ni hewa sumu zinazotokana na viwanda na zile zingine ambazo
binadamu anazalisha. Miti inapotumia hewa ya ukaa inatoa hewa ya oksijeni
ambayo hutusaidia sisi binadamu kuvuta. Misitu ya asili iliyopo Halmashauri ya
Tanganyika ni miongoni mwa misiti iliyo na uwezo wa kukabiliana na mabadiliko
ya Tabia nchi.
Misitu hiyo ndio imekuwa msitu wa kwanza ya
kitropiki Afrika kufanikiwa kuuza hewa ya ukaa. Hii ina maana kwamba kumbe
inawezekana kuwa na misitu mbali mbali katika nchi yetu kuwekwa kwenye utaratibu wa kuuza hewa ya ukaa
na ikanufaisha zaidi siyo nchi yetu tu kwa kiwango kikubwa zaidi bali na Bara
la Afrika mfano DRC Congo.
Wananchi
waliopo Mkoani Katavi na watanzania wote na Bara la Afrika hatuna budi
kuhifadhi misitu na kutunza mazingira yetu kwa manufaa yetu na vizazi vijavyo.
Tuendelee kutunza mazingira yetu kwa kupanda miti mbali mbali(mfano Korosho,
Mipeini) kwa ajili ya kutunza mazingira na kuongeza uchumi na kuzingatia kanuni
mbali mbali za kutunza mazingira.