Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 18,2021
Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linamsaka mtuhumiwa Dela Megejuwa Lwaho (44) kwa kusababisha kifo cha mtoto wake Juma Dela Megejuwa (12) na watu wengine wawili kuzirai baada ya kuwapa dawa ya miti shamba idhaniwayo kuwa na sumu ili wasafishiwe nyota zao.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Jumatatu Januari 18,2021 Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba amesema tukio hilo limetokea Januari 16,2021 majira ya saa tisa na nusu alasiri katika kijiji cha Mwaningi kata ya Bulige wilayani Kahama mkoa wa Shinyanga.
Amesema Mganga huyo wa jadi alitwanga dawa kwenye kinu ambayo ilitakiwa waioge ili kuosha nyota zao badala yake akawaambia wainywe.
“Juma Dela Megejuwa ambaye ni mtoto wa mganga wa jadi (mtuhumiwa) Dela Megejuwa Lwaho alifariki dunia baada ya kunywa dawa ya kienyeji inayodhaniwa kuwa na sumu akiwa na watu wawili nyumbani”,amesema.
“Watu hao wawili waliokuwa nyumbani kwa mtuhumiwa ni Loya Nsalala Ngusa (66) jirani wa mtuhumiwa na Bahati Ludahila Ngusa (25) mkazi wa Shilima Kwimba Mwanza ambaye ni mgeni aliyefikia nyumbani hapo kwa mtuhumiwa ambao walikunywa dawa hiyo ya kienyeji na kuzirai papo hapo na kukimbizwa kituo cha afya Chela kwa matibabu na hali zao zinaendelea vizuri”,ameeleza Kamanda Magiligimba.
Amesema mtuhumiwa (mganga wa jadi) alikimbia mara baada ya tukio hilo na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Halmashauri Mji Kahama kwa uchunguzi zaidi.
Kamanda Magiligimba ametoa wito kwa waganga wa jadi kuwa na uhakika na matumizi ya dawa zao pamoja na matumizi mazuri ya vibali/leseni zao ili kuepuka kusababisha vifo na madhara kwa wateja wao na jeshi la polisi halitamuonea muhari mganga yeyote anayekwenda kinyume na maelekezo ya vibali/leseni zao.
Social Plugin