Nyama ikiwa imening'inizwa kwenye machinjio ya Manispaa ya Shinyanga kata ya Kambarage
Mkaguzi Mkuu wa nyama wa Manispaa ya Shinyanga, Verani Mwaluko amemsimamisha kazi mchinja Ng'ombe mkuu wa machinjio ya manispaa ya Shinyanga, Rashid Masanja kwa tuhuma ya kuruhusu kuingizwa ndani ya eneo la machinjio nyama ya ng'ombe wawili wanaodhaniwa wamekufa (Kibudu).
Amesema mchinja ng'ombe huyo alihalalisha nyama hiyo ikauzwe kwenye mabucha ya nyama mitaani hali ambayo inadaiwa kuwa ingeweza kuleta madhara ya magonjwa kwa wananchi wa manispaa hiyo.
"Nilipata taarifa kwamba kuna ng'ombe wameingizwa machinjio wakiwa wameshakufa, nikafuatilia kwa wakaguzi na madaktari wa eneo hili wakakanusha kuhusika na jambo hilo, ndipo nikafuatilia kwa Bakwata (Rashid) ambaye alienda huko porini. Kisheria mnyama aliyekufa bila kuchinjwa kwa sababu za aina yoyote lazima ataketezwe kwa sababu kuna magonjwa mnyama akishachinjwa hayawezi kuonekana.
"Hatua zitakazochukuliwa sasa ni kumsimamisha mchinjaji wa Bakwata na kumkabidhi kwao kwa ajili ya taratibu za kimaadili, pia hii nyama lazima iteketezwe na hatua za kisheria zitafuata ikiwemo kwenda polisi na mahakamani," amesema Mwalukwa.
Mmoja wa madaktari katika machinjio hiyo ya Ernest Nigo akizungumzia suala hilo, amesema alipigiwa simu na Rashid (mchinjaji) kujulishwa kuwa kuna ng'ombe wameshawachinja na akawaelekeza wawatafute madaktari.
"Nikawaambia cha kufanya wakiwa wanakuja wamtafute mhusika, sasa hadi usiku napigiwa simu ng'ombe wakawa wameshafika bila mimi kujulishwa wakati niliwaambia wamtafute mhusika na wakimkosa wanijulishe tujue tunafanya nini, sasa nakuta nyama iko hapa tayari," amesema.
Kwa upande wake Rashid Masanja ambaye ni mchinjaji wa Bakwata Mkoa wa Shinyanga ameeleza "ninapopigiwa simu nakuwa najua kwamba mawasiliano yote ya wahusika na taratibu zote zinakuwa zimekamilishwa.
Mazoea tuliyonayo ni kwamba mfanyabiashara anapopata ng'ombe wa bei rahisi humtafuta daktari na mchinjaji, kwahiyo mimi niliambiwa kuchinja na mwenye ng'ombe siwezi kuwa na utaalam wa kujua kama kitaalam wana shida ama la,".
Kwa upande Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa nyama, Abdi Kidodo ameeleza kuwa ng'ombe siyo kwamba walikuwa wamekufa bali wamechinjwa nje ya tukio (machinjio) na kuletwa machinjioni bila kufuata utaratibu wa kuchinjwa kwenye machinjio, ambapo amewataka wafanyabiashara kufuata taratibu na watakaokiuka watasimamishwa.
"Kwahiyo, itabidi tuanze kuwaelimisha wachinjaji na wenye mabucha kufuata sheria na utaratibu...kwahiyo wito kwa wafanyabiashara wafuate sheria ng'ombe wote ziletwe kwenye machinjio zichinjwe pale na watakaokiuka ni kuwasimamisha kufanya biashara," amefafanua.
Mkaguzi Mkuu wa nyama wa Manispaa ya Shinyanga, Verani Mwaluko
Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Nyama, Abdi Kidodo
Rashid Masanja ambaye ni mchinjaji wa Bakwata Mkoa wa Shinyanga