Mlinzi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga wa Kampuni ya Ulinzi ya Suma JKT Guard Geofrey Paul akimshambulia Daudi Lefi leo jioni ambapo video ya tukio hilo imesambaa mtandaoni
Mlinzi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga Geofrey Paul akimshambulia Daudi Lefi
Mlinzi wa hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Shinyanga akiamua ugomvi uliotokea mlinzi mwenzake akiendelea kumshambulia Daudi Lefi.
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Katika hali isiyotarajiwa mwanaume aliyejulikana kwa jina la Daudi Lefi (45) amejikuta katika wakati mgumu baada ya kushambuliwa na Mlinzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga Geofrey Paul akiwa na mwenzake wanaodaiwa kumtaka aondoke wodini kwamba muda wa kusalimia wagonjwa umeisha.
Tukio hilo lililozua gumzo la limetokea leo Ijumaa Januari 22,2020 majira ya saa 11 na dakika 45 jioni wakati kijana huyo akiwa katika wodi ya wanawake namba 1 ambako mama yake mzazi Victoria Lugano Mwakagari amelazwa hospitalini hapo jana.
Akisimulia kuhusu tukio hilo, ndugu wa kijana huyo Lydia Lefi ameiambia Malunde 1 blog kuwa kaka yake amekutwa na mkasa huo wakati akiwa katika harakati za kulipia dawa za mama yao ambaye amelazwa katika hospitali hiyo jana Januari 21,2021 lakini jina lilikuwa halionekani kwenye Computer.
“Kaka alikuwa alipie dawa, alipewa karatasi ya kwenda kulipia dawa, alipoenda kufuata Control number ili alipie, jina likawa halionekani kwenye Computer, ikabidi aende wodini kwa mgonjwa kuangalia/kuulizia amesajiliwa kwa jina gani,akiwa wodini hao walinzi ndipo walipoingia wodini na kumtaka aondoke kwamba muda umekwisha.
"Walivyomtaka aondoke wodini akawaambia amekuja kuangalia jina gani mgonjwa ameandikishwa, wale walinzi wakamwambia aondoke muda huo huo, akawaomba lakini wakamwambia Huwezi kutupangia kazi. Kaka akasema nitaondokaje mama hajapata huduma ,wale walinzi wakaanza kumsukuma, ndipo mlinzi mmoja akachomoa mkanda wa suruali na kuanza kumshambulia huku mwingine akimsukuma, wakati purukushani zikiendelea baadae akaja mlinzi wa kike akasogea na kuwaachanisha”,ameeleza Lydia.
Daudi Lefi amesema walinzi hao wanaodaiwa kuwa ni wa Suma JKT walidhani amefika muda huo huo hospitalini wakati yeye alikuwa amefika hospitalini hapo muda mrefu lakini Computer za Hospitali zikawa hazisomi jina la mgonjwa wake wakati anataka kununua dawa.
"Sikurusha ngumi kupigana kwa sababu ni eneo la hospitali wangesema nimeenda kufanya vurugu. Walionishambulia walikuwa wawili lakini mmoja ndiyo aliyeanza kwa kunichapa na mkanda akisema nitamtambua kuwa yeye ni nani huku akinitukana,nami nikamsihi aache kutumia lugha chafu eneo la kazi",amesema Daudi.
"Hayo yote yametokea wakati nikimweleza kuwa nimefika wodini kuulizia ndugu zangu na mgonjwa kuwa wameandikisha jina gani mapokezi kwani jina halionekani mapokezi ili nilipie dawa,wakati naendelea kushambuliwa nikamuona mama yangu mgonjwa akitoka wodini huku akihema presha imepanda akifuatilia nini kinaendelea ndipo nikaanza tena kumrudisha wodini kumhudumia nikaulizia jina aliloandikisha nikaenda kuchukua dawa nikamletea wodini", ameeleza Daudi.
Daudi amesema kutokana na kipigo hicho ameumia mkono wa kushoto ambao umevimba na kuchanika kwenye kiwiko.
"Baada ya tukio hilo wamenifuata na mkubwa wao na kuniomba tuyamalize kwamba kijana wao amekosea nami nimeamua kuwasamehe. Katika hali ya ubinadamu nimeamua kumsamehe kijana huyo baada ya kuomba radhi",ameongeza.
Baadhi ya wagonjwa na watu wanaouguza wagonjwa wameeleza kusikitishwa na kitendo cha mlinzi kumpiga ngumi na mkanda na kuongeza kuwa baadhi ya walinzi katika hospitali hiyo wana lugha mbaya na wanatumia ubabe hawaangalii utu.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga, Luzila John Boshi amekiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa atatoa taarifa baadae na kwamba yupo kwenye kikao.
TAZAMA VIDEO HAPA CHINI
Social Plugin