Na Salvatory Ntandu - Kahama
Kufuatia kutokea kwa mlipuko wa ugonjwa wa homa ya nguruwe wilayani Kahama mkoani Shinyanga Serikali imelazimika kupiga marufuku, uuzaji, usafirishaji na ulaji wa nyama ya nguruwe kwa muda usiojulikana baada ya kuripotiwa ugonjwa huo kusambaa kwa kasi na kusababisha vifo vya wanyama hao zaidi ya 800.
Kauli hiyo imetolewa jana na Mkuu wa wilaya ya Kahama Anamringi Macha wakati akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake kuhusiana na hatua zilizochukuliwa na serikali baada ya kujitokeza kwa ugonjwa huo na namna walivyojipanga kuudhibiti ili usiendee kuleta madhara kwa wafugaji.
Alisema kuwa wamelazimika kuchukua hatua hiyo ili kudhibiti kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa huo ambao unaua wanayama aina ya nguruwe kwa kasi na watakaobainika kukiuka agizo hilo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
“Kwa sasa Kahama biashara ya wanyama aina ya nguruwe imepigwa marufuku, lengo letu ni kudhibiti ugonjwa huu,wataalamu wetu wanaendelea kufanya utafiti ili kuhakikisha wanaudhibiti mapema ili kuzuia madhara yasijitokeze zaidi,”alisema Macha.
Sambamba na hilo Macha aliwataka walaji wa nyama ya nguruwe kuacha kula nyama hiyo hadi watakapotangaziwa na serikali na badala yake watumie vitoweo vya wanyama wengine kama vile ng’ombe,mbuzi,kondoo na kuku ambapo ugonjwa huu hujawaathiri.
Kwa upande wake mkuu wa Idara ya Mifugo wa Halmashauri ya Mji Kahama Dk. Damin Kilyenyi alikiri kuwepo kwa ugonjwa wa homa ya nguruwe na kusema kuwa unasababishwa na mwingiliano wa nguruwe pori na wanaofungwa nyumbani na kwa Kahama uliwahi kujitokeza mwaka 2017 na kuwataka wafanyabiashara kuwa na subira wakati suala hilo likitafutiwa ufumbuzi wa kina.
“Ugonjwa huu unawaathiri wanyama aina ya nguruwe tu, na hauna madhara kwa binadamu na wanyama wengine dalili zake ni mnyama kuacha kula,kutokwa damu damu masikioni na kwenye macho na huishi kwa siku tatu ndio anapoteza maisha,”alisema Kilyenyi.
Aliongeza kuwa mpaka sasa ugonjwa huo hauna chanjo wala dawa na mnyama akipata lazima afe na kuwataka wafugaji kuchukua tahadhari ikiwa ni pamoja na kuwatenga wanyama ambao wameonekana na dalili za ugonjwa huo ili kudhibi usienee kwa wengine.
Evans John Kishiwa ni mfugaji wa nguruwe katika mtaa wa Mhongolo alisema kuwa mpaka sasa nguruwe 17 katika banda lake wamekufa kutokana na ugonjwa huo na kuiomba serikali kulitafutia ufumbuzi wa kina ili mifugo yao isiendelee kuangamia.
“Nguruwe akipata ugonjwa huu anaanza kutetemeka,hali chakula, anatokwa damu masikioni na kwenye macho,anaanza kubadilika rangi na baada ya hapo hufa ghafla,nimepata hasara ya zaidi ya shilingi milioni 2",alieleza.
Wilaya ya Kahama inatajwa kuwa na wafugaji wengi wa wanyama hao huku idadi ya nguruwe ikitajwa kufikia 2000.
Social Plugin