Mfano wa moto
Na Suleiman Abeid,TimesMajira Online,Shinyanga
MTOTO mwenye umri wa miaka 11 (jina limehifadhiwa) mkazi wa Mtaa wa Majengo Kata ya Kambarage Manispaa ya Shinyanga amejeruhiwa miguu yake yote miwili baada ya kupigwa na kuchomwa na mama yake mzazi kwa jiko la mkaa wenye moto akituhumiwa kuunguza maharage.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa kwa waandishi wa habari jana mjini Shinyanga, mtoto huyo ametendewa ukatili huo mwishoni mwa wiki iliyopita na mama yake mzazi aliyetajwa kwa jina Hanifa Athumani mkazi wa Mtaa wa Majengo Kambarage Shinyanga.
Pamoja na kutendewa ukatili huo mtoto huyo hakupelekwa hospitali huku mama yake akificha kitendo hicho kuwa siri ambapo hata pale viongozi wa Serikali ya Mtaa wa Majengo walipopata taarifa hizo mtuhumiwa huyo alidiriki kumficha mwanaye huyo kwenye uvungu wa kitanda.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na majirani mbele ya waandishi wa habari na viongozi wa Serikali ya Mtaa wa Majengo imedaiwa mama huyo alitenda ukatili huo baada ya kuchukizwa na kitendo cha mtoto kuzembea na kusababisha kuungua kwa maharage yaliyokuwa jikoni na yeye kutoyaangalia yasiungue.
Mmoja wa majirani hao, Mariamu Thomas amesema, siku hiyo ya tukio alimuona mtoto huyo akitembea kwa shida akichechemea na alimuuliza kwa nini anatembea akiwa na hali hiyo ambapo mtoto alimjibu ameungua kidogo miguuni hata hivyo hakuendelea kumuuliza zaidi.
“Mimi siku hiyo nilipofika hapa nyumbani nilimuona huyu mtoto akitembea kwa shida kwa kuchechemea, ilibidi nimuulize kwa nini alikuwa akitembea hivyo, lakini mtoto alinijibu kwa kifupi kwamba ameungua kidogo miguuni.
“Kwa kweli kwa vile mimi siku hiyo sikushinda nyumbani sikuendelea kumuuliza zaidi nikaamini huenda kweli kaumia kidogo japokuwa alikuwa akitembea kwa shida, na niliendelea na shughuli zangu,” ameeleza Mariamu.
Jirani mwingine amesema aliyejitambulisha kwa jina la Asha Nassor amesema wakati tukio hilo lilitokea hakuwepo nyumbani lakini aliporudi jioni nyumbani alimuona mtoto huyo akiwa ameungua miguuni na alimuuliza ni nani aliyemchoma huo moto ambapo alijibu amechomwa na mama yake.
“Siku hiyo asubuhi sikuwepo nyumbani, nilishinda msibani, niliporudi jioni mtoto akaniambia, mama Saidi nimeungua moto, nikamuuliza umeunguzwa na nani? Akajibu mama ameniunguza eti kwa sababu nimeunguza maharagwe.
“Amesema baada ya mama kukuta maharagwe yameungua alinifokea akawa amenichoma, nikamuuliza alichomwa au alirushiwa jiko, akajibu mama yake alimsukumia jiko, asubuhi yake nilimpatia dawa nikampakaa, lakini baadae sikuendeleza, baadae mama yake aliendelea kumwekea manyoa ya sungura,” ameeleza Asha.
Kwa upande wake mama wa mtoto huyo, Hanifa Athumani amesema siku ya tukio alimpatia mwanaye shilingi 600 akanunue maharagwe na akija ayatenge jikoni kwa ajili ya mboga, na yeye aliingia ndani kujipumzisha.
“Siku hiyo mimi nilimpatia shilingi mia sita akanunue maharagwe na aje ayatenge jikoni kwa ajili ya mboga, mimi niliingia ndani kujipumzisha kidogo, muda mfupi nikasikia majirani wanamwita huku wakimuuliza mbona maharagwe yanaungua?”
“Nilishituka nikatoka nje haraka na kukuta kweli maharagwe yote yameungua hadi juu, nilimwambia sasa umefanya nini, yeye akaniangalia kwa jicho baya kama vile amefanya makusudi, ndiyo nikashikwa hasira nikampiga teke, sasa alipamia jiko na kumwagikiwa majivu yenye moto,” ameeleza Hanifa.
Hata hivyo mtuhumiwa huyo alidai hakuweza kumpeleka hospitali mwanae ili aweze kutibiwa badala yake alimnunulia dawa na kumtibisha akiwa hapo nyumbani huku akidai kuwa amekuwa na tabia ya utundu na udokozi wa vitu vidogo vidogo hali ambayo haimfurahishi.
Viongozi wa Serikali ya Mtaa wa Majengo, Majid Issa ambaye ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa na Kamanda wa Sungusungu, Hamisi Mkondo walithibitisha kutokea kwa kitendo hicho na kwamba tayari wamechukua hatua za kumwita ofisini mtuhumiwa huyo.
“Ni kweli tulipata taarifa za mtoto huyu kufanyiwa ukatili huu kwa kuchomwa moto na mama yake mzazi, ni jambo linalosikitisha, maana vitendo kama hivi watoto hutendewa na mama zao wa kambo, si mama mzazi, lakini huyo amemtendea mwanae wa kuzaa.
“Tayari tumechukua hatua za kumtaka afike ofisini ili tuweze kumsikiliza kwa kina sababu za yeye kuchukua hatua ya kumfanyia ukatili huu mwanae, na baada ya hapo hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa kwa kumfikisha kwenye vyombo vya dola,” ameeleza Mwenyekiti Issa.
Kwa upande wake Kamanda wa Mtaa, Hamisi Mkondo amesema mara baada ya kupata taarifa kutoka kwa majirani za kuumizwa kwa mtoto huyo walifika nyumbani kwa mtuhumiwa ili kupata ukweli lakini alisema mwanaye wakati huo hakuwepo pale nyumbani.
“Sisi viongozi tulipoletewa taarifa tulifika kwa mama huyu kwa lengo la kumuona mtoto ili tuweza kubaini ameumia kiasi gani, lakini huyu mama alidai mwanaye hakuwepo pale nyumbani, ilibidi mimi nitumie nguvu na kuingia ndani, nikakuta mtoto kafichwa kwenye uvungu wa kitanda ambako nilimtoa nje,” ameeleza Mkondo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Debora Magiligimba amesema, hakuwa na taarifa juu ya tukio hilo na kwamba atafuatilia na kisha atalitolea taarifa baada ya kupata habari kamili.
CHANZO - TIMES MAJIRA
Social Plugin