Shirika la Bima la Taifa Tanzania (NIC) limetoa mchango wa shilingi 14, 700,000 kwa ajili ya kufanikisha mashindano ya soka ya Kombe la Mapinduzi ya mwaka huu yanayotarajiwa kuanza tarehe 5.1.2021 katika kiwanja cha Amani, Mjini Zanzibar.
Mkurugenzi Mtendaji wa NIC Dkt. Elirehema Doriye alimueleza Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Tabia Maulid Mwita kwamba wameamua kuyapa msukumo mashindano hayo baada ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kukaribisha Mashirika, Wafanyabiashara na wadau wa michezo kuchangia mashindano hayo.
Alisema lengo la mchango huo ni kusaidia gharama za uendeshaji wa mashindano na zawadi ya mchezaji bora kwenye michuano hiyo inayoshirikisha timu tisa, nne kutoka Zanzibar na tano kutoka Tanzania Bara.
Mkurugenzi Doriye alimuahidi Waziri Tabia Maulid Mwita kwamba NIC itaendelea kuwa washirika wa karibu wa mashindano ya Kombe la Mapinduzi kwa miaka mengine ijayao.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika Wizarani kwake Migombani, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Tabia Maulid Mwita alilishukuru Shirika la Bima la Taifa Tanzania kwa msaada huo na ahadi walizotoa kwa miaka ijayo katika kuendesha mashindano hayo.
Alisema mchango wa shilingi milioni 14 na laki saba waliotoa utasaidia sana katika kufanikisha mashindano ya mwaka huu ambayo yemekua endelevu tokea yalipoanzishwa kitaifa mwaka 2007.
Waziri Tabia aliwaeleza viongozi wa Shirika la Bima la Taifa Tanzania kuwa Serikali imeazimia kuimarisha michezo mbali mbali ikiwemo Ligi kuu ya Zanzibar na michango ya wadau inahitajika katika kufanikisha lengo hilo.
Social Plugin