Baraza la mchele Tanzania(RCT) kwa kushirikiana na taasisi ya utafiti Tanzania (REPOA) wanaendesha mafunzo kwa wasindikaji wa mpunga 100 kutoka mikoa ya Geita,Shinyanga, na Tabora ili kuwajengea uwezo wa kusindika bidhaa hiyo kwa viwango vya kimataifa.
Hayo yamebainishwa jana na Mkurugenzi mkuu wa baraza hilo, Winnie Bashagi katika hafla ya ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu kwa wasindikaji wa zao la mpunga kutoka mikoa ya kanda ya ziwa na kusema kuwa mchele wa Tanzania unakosa soko kimataifa kutokana na kutofungashwa kwa viwango vya kimataifa.
Alisema zaidi ya asilimia 80 ya mchele unaozalishwa na wakulima wadogo katika wilaya zaidi ya 64 hapa nchini unakosa sifa katika masoko ya kikanda ya jumuia ya afrika mashariki (EAC) na (SADC) kutokana kutosindikwa kwa viwango vinavyotakiwa licha ya kuwa na uzalishaji mkubwa.
“RCT na REPOA tulifanya utafiti katika wilaya zinazolima zao hili tulibaini kukosekana kwa elimu ya usindikaji,wasindikaji wengi wanachanganya madaraja,usafi,usimamizi usiridhishwa wa magahala ya kuhifadhia mpunga,matumizi yasiyosahihi ya pembejeo kwa wakulima wakati wa kuandaa mashamba,”alisema Bashagi.
Awali akifungua mafunzo hayo ya siku tatu Katibu tawala wa wilaya ya Kahama Timoth Ndanya kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga Bi. Zainab Telack aliwataka (RCT) kufungua ofisi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa lengo la kuwajengea uwezo wakulima na wasindikaji katika kuongeza thamani mazao yao.
“Kahama tunazalisha mpunga wa kutosha hakikisheni mnawajengea uwezo wasindikaji na wakulima wa zao hili la biashara ili kuwainua kiuchumi hakuna sababu ya wao kuendelea kukosa masoko ilihali wanamchele safi ambao unahitaji kupangwa katika madaraja yanayotakiwa kimataifa,”alisema Ndanya.
Naye Steven Mombela mtafiti kutoka (REPOA) alisema wao kwa kushirikiana na baraza la mchele wanatekeleza mradi huo ujulikanao kama Tradecom II kwa ufadhili wa jumuiya ya ulaya (EU) na waliandaa mafunzo hayo ili kuwajengea uwezo ili waweze kuzalisha mchele wenye viwango vinavyokidhi ushindani katika soko la ndani na nje ya nchi.
“Mradi huu ni wa miaka miwili ulianza mwaka 2020 na unatarajiwa kukamilika mwaka huu,na tukimaliza kwa kanda hii tutaelekea katika kanda nyingine inayojumuisha wasindikaji kutoka mikoa ya Morogoro,Njombe,Iringa na Mbeya,”alisema Mombela.
Asha Hassan Msangi ni mmoja wa wasindikaji wa zao mpunga kutoka Kahama ameiomba Serikali kuboresha mazingira ya biashara ya mchele ikiwa ni pamoja na kufungua masoko ya mchele na kuwazuia wafanyabiashara wa nje kununua mpunga kwa wakulima.
Social Plugin