Na Anthony Mayunga - Mwananchi
Mwanamke mmoja amejinyonga kwa kutumia kanga kwenye mti wa mwembe katika kijiji cha Itununu wilayani Serengeti, kwa madai ya wivu wa mapenzi, huku akiwa na mimba ya miezi tisa.
Mkuu wa wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu alithibitisha Mkami Nyamhanga (21) kujinyonga Januari 17 kwenye mti wa mwembe uliopo shambani.
Alisema mwili wake ulionwa na watoto waliokuwa wanakwenda kuangua matunda kwenye mwembe huo na ndio waliotoa taarifa ya kifo hicho.
Kwa mujibu wa Babu, marehemu inadaiwa alikuwa anamtuhumu mume wake kuwa na mpenzi mwingine.
”Asubuhi alitoka bila kuaga mpaka alipogundulika amejinyonga kwa kutumia kitanzi cha nguo ambayo alifunga kwenye tawi la mwembe na kuning’inia,”alisema na kuongeza:
“Mganga aliyefanya uchunguzi alibaini kuwa kifo chake kimetokana na kitanzi shingoni kilichosababisha mzunguko wa damu na hewa kukosekana, ndugu walikabidhiwa mwili kwa ajili ya kuuzika na hakuna mtu aliyekamatwa lakini uchunguzi unaendelea.’’
Mganga mfawidhi wa zahanati ya Itununu, Melick Salapioni alilieleza Mwananchi kuwa mwanamke huyo alikuwa na mimba inayokaribia miezi tisa.
Alisema kutokana na mama kujiua, alikata mawasiliano ya hewa ya oksijeni kati yake na mtoto na hivyo kusababisha kichanga hicho kufa.
Via Mwananchi
Social Plugin