Afisa Elimu Sekondari wa Wilaya ya Ikungi, Mwalimu Ngwano Ngwano akizungumza kwa niaba ya mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo, Justice Kijazi na Mkuu wa Wilaya Edward Mpogolo amempongeza na kumshukuru Mtaturu kwa dhamira yake ya kusaidia maendeleo ya wananchi kwenye sekta mbalimbali katika jimbo hilo.
Mbunge wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu, akizungumza na wananchi wakati akitoa msaada huo.Na Dotto Mwaibale, Ikungi
MBUNGE wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu ameendelea kuwa kumbuka wanafunzi katika jimbo lake kwa kuwanunulia vifaa mbalimbali vya shuleni.
Vifaa alivyotoa ni sare za shule, madaftari na kalamu vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni 30 ambapo wanufaika ni wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wapatao 1161 kutoka katika familia zisizo na uwezo zilizopo jimboni humo.
Hatua hiyo ni utekelezaji wa ahadi yake ya kuwasaidia wanafunzi katika jimbo hilo ikiwa ni kuunga mkono jitihada za Rais Dkt. John Magufuli za kutoa elimu bure kuanzia shule za msingi hadi sekondari.
Akizungumza wakati akigawa vifaa hivyo leo hii Mtaturu alisema amekuwa akifanya hivyo tangu alipo chaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo.
“Serikali yetu ya awamu ya tano imewekeza kwenye elimu, inatoa elimu bila ya malipo nami kama mbunge wa jmbo hili nimeona niunge mkono jitihada hizo kwa kusaidia sare na vifaa vya shule ili kusiwepo kikwazo na hivyo kuwezesha lengo la serikali kutimia,” alisema Mtaturu.
Alisema katika utendaji kazi wake kipaumbele chake cha kwanza ni elimu kwa kuwa ndio msingi wa maendeleo hasa kwa watoto.
Mtaturu alisema dhamira yake hiyo ya kuwasaidia wanafunzi hao inaenda sambamba na kauli mbiu yake isemayo 'ElimuYetu, Maendeleo Yetu' inayochochea upatikanaji wa elimu kwa wote ili iwe njia ya kupatikana kwa maendeleo.
Kwa upande wake Afisa Elimu Sekondari wa Wilaya ya Ikungi, Mwalimu Ngwano Ngwano akizungumza kwa niaba ya mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo, Justice Kijazi na Mkuu wa Wilaya Edward Mpogolo amempongeza na kumshukuru Mtaturu kwa dhamira yake ya kusaidia maendeleo ya wananchi kwenye sekta mbalimbali katika jimbo hilo.