Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko (kulia) na Mkaguzi Mkuu wa Nyama Manispaa ya Shinyanga, Verani Mwaluko wakilitazama vazi la muuza nyama ambalo limeonekana kuwa chafu kukithiri, hivyo akawataka wauza nyama kuwa wasafi
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko akizungumza na baadhi ya watendaji wa serikali wanaosimamia machinjio ya manispaa ya Shinyanga iliyopo eneo la Nguzo Nane
Muonekano wa hali ilivyo katika machinjio ya Manispaa ya Shinyanga iliyopo eneo la Nguzo Nane kata ya Kambarage
DC Mboneko akiendelea na ukaguzi katika machinjio hiyo
Baadhi ya maeneo ya machinjio hiyo ambazo zimeonekana kuwa chafu na kulalamikiwa na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko na kutaka wasimamizi wafanye usafi haraka
DC Mboneko (kulia) akizungumza na wafanyabaishara wa nyama katika soko la Nguzo Nane
**
Na Damian Masyenene - Shinyanga
MKUU wa Wilaya ya Shinyanga mkoani Shinyanga, Jasinta Mboneko ameonyesha kukerwa na kusikitshwa na hali ya kukithiri kwa uchafu na mazingira yasyo ya kuridhisha katika machinjio ya Manispaa ya Shinyanga, hivyo kulazimika kutoa maagizo kwa wasimamizi kuhakikisha kuwa ifikapo kesho Januari 26, mwaka huu usafi uwe umefanyika.
DC Mboneko ametoa maagizo hayo leo Jumatatu Januari 25,2021 alipotembelea machinjio hiyo ikiwa ni ufuatiliaji wa sakata la nyama ya ng’ombe isiyo halali iliyoingizwa kwenye machinjio hiyo kinyume na taratibu.
Akiwa katika machinjio hiyo akizungumza na viongozi mbalimbali akiwemo afisa mifugo wa wilaya, mkaguzi mkuu wa nyama manispaa ya Shinyanga, Verani Mwaluko, Mwenyekiti wa Mtaa wa Majengo Kata ya Kambarage, Majjid Ally na afisa afya kata ya Kambarage, Costancia Michael, Mkuu huyo wa wilaya amesema kuwa eneo la machinjio ni chafu kuliko maelezo na mazingira yanasikitisha na kunuka sana, hali ambayo itawafanya walaji kupata magonjwa.
“Lazima pawe pasafi na kesho nitapita hapa nikute mabadiliko hapa. Muda ambao watu hawafanyi uchinjaji muutumie kufanya usafi, muwabane watu wafanye usafi kabla ya kuchinja ama baada ya kuchinja,” ameagiza.
Akizungumzia sakata la nyama ya ng’ombe inayodhaniwa kuwa kibudu iliyoingizwa katika machinjio hiyo kinyume na utaratibu, Mboneko amepiga marufuku mnyama aliyekufa kuletwa buchani wala wafanyabiashara ya nyama za ng'ombe mjini Shinyanga kusafirisha nyama hizo kwa kutumia pikipiki huku nyama zikiwa zimewekwa kwenye mifuko ya sandarusi.
“Mifugo isiyo halali isiingie kwenye machinjio yetu, likijirudia tena hili basi mtaadhibiwa vikali idara ya mifugo. Hili lisijirudie tena. Tunaomba sana, wale wanaochinja wazingatie taratibu za uchinjaji.
Tunataka nyama yote inayoingia kwenye bucha zetu iwe ni halali, aliyeleta na aliyepokea na kugonga mhuri tunawataka tuwawajibishe. Wauza nyama zingatieni taratibu za afya, na msipokee nyama isiyoeleweka na uongozi wa wafanyabiashara wa nyama katika soko la Nguzo Nane usimamie vyema usafi na kutoingizwa nyama isiyo halali. Kuanzia leo ni marukufu nyama za ng’ombe zinazochinjwa nje ya chinjio hili kuingizwa hapa au waliokondeana”, amesema.
Pia mkuu huyo ameagiza kupelekwa ofisini kwake kwa mfanyabiashara mwenye ng’ombe walioingizwa machinjioni ikidaiwa tayari waliisha kufa pamoja na mkaguzi wa nyama aliyewapiga mihuri ili kuonesha nyama yake ilikuwa inafaa kwa matumizi ya binadamu.
Mboneko alisema kitendo cha kuingizwa machinjioni kwa ng’ombe waliokufa na nyama yake kutaka kuingizwa sokoni kingeweza kuhatarisha maisha ya walaji wa nyama hiyo na kwamba moja ya majukumu yake akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya ni kuhakikisha wananchi wako salama wakati wote.
Kuhusu suala la bei ya nyama kuuzwa kwa shilingi 7,000/= katika baadhi ya bucha mjini Shinyanga, Mkuu huyo amemuagiza Ofisa anayehusika na suala la mifugo kuitisha mara moja kikao na wafanyabiashara ili kuzungumzia suala la bei kuwa juu wakati wengine wakiuza shilingi 6,000/= kwa kilo moja.
Kwa upande wake, Mkaguzi Mkuu wa Nyama Manispaa ya Shinyanga, Verani Mwaluko ameahidi kuyatekeleza maagizo yote kuhusu usafi na ukaguzi katika machinjio hiyo, huku akibainisha kuwa ubebaji nyama kwenye sandarusi na bodaboda (pikipiki) umepigwa marufuku na watakaoendelea basi watashughulikiwa.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Majengo Kata ya Kambarage ilipo machinjio hiyo, Majjid Issa Ally amesema uongozi wa mtaa umeyapokea maagizo hayo na utaingia kazini kuyafanyia kazi, huku Afisa Afya Kata ya Kambarage, Costancia Michael akieleza kuwa uchukuaji nyama kiholela kutoka kwenye machinjio hiyo hauruhusiwi na kuwataka wasimamizi wakiwemo maafisa mifugo waruhusu magari yaliyosajiliwa kisheria kwa ajili ya kubeba nyama.
Mhasibu wa Umoja wa Wafanyabiashara wa Nyama Manispaa ya Shinyanga, Ngassa Mashema amesema suala la nyama isiyo halali kuingizwa sokoni linasababishwa na wafanya biashara wengi kuendeshwa na tamaa na kutaka ng'ombe wa bei rahisi, ambapo ameahidi kuyafanyia kazi maagizo ya Serikali na kwamba suala hilo halitojitokeza tena.
Akizungumza baada ya kulalamikiwa na wafanyabiashara wengi kuwa anauza nyama bei rahisi na kumaliza mapema akihusishwa na uuzaji wa nyama isiyo halali na kumlazimu Mkuu wa Wilaya kumfuata nyumbani kwake kufahamu undani wa jambo hilo, Mwenyekiti Wafanyabiashara wa Nyama Manispaa ya Shinyanga, Abdi Kidodi amekanusha tuhuma hizo na kueleza ng’ombe wote anawachinjia kwenye machinjio ya manispaa na wanakaguliwa na wataalam wa afya.
“Sakata hili na hizi lawama zinakuja kwa sababu kulizuka mgogoro wa bei ya nyama wapo waliotaka tuuze kilo moja Sh 7,000/= sisi tukakataa na kujiengua tukaunda umoja wetu tukabaki na kilo moja Sh 6,000, kwa hiyo kuna mgawanyiko wa makundi mawili na hapo ndipo kunatengenezwa hizi tuhuma zisizo za kweli,” amefafanua.
Akizungumzia mlipuko wa ugonjwa wa homa ya Nguruwe ulioanzia katika wilaya ya Kahama, DC Mboneko amekazia maelekezo ya serikali ya marufuku ya biashara ya nyama ya nguruwe (Kitimoto), huku akiwataka maofisa mifugo kupita kwenye bucha kukagua na kutoa taarifa, pia kuwatembelea wafugaji kuwaelimisha na kufanya ukaguzi kuhakikisha biashara hiyo haifanyiki.
Social Plugin