Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KIJANA APIGWA SHOTI YA UMEME AKIIBA WAYA KWENYE TRANSFOMA

 
Na Florah Temba - Mwananchi
Riziki Mosha (23) mkazi wa mkoani Arusha amekamatwa na Shirika la umeme nchini (Tanesco) Mkoa wa Kilimanjaro kwa tuhuma za kuiba waya katika Transfoma iliyopo kijiji cha Mandaka Mnono Wilaya ya Moshi.

Tukio hilo limetokea leo Jumatano Januari 20, 2021 saa 12:00 asubuhi na alikamatwa kutokana na kushindwa kutembea kwa sababu ya majeraha aliyoyapata baada ya kupigwa shoti ya umeme wakati akiiba waya huo katika njia kuu ya umeme ya msongo wa 33 Old Rombo kwenye Transfoma yenye uwezo wa KVA 100.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Mnono Ndekio amesema alipata taarifa kutoka kwa wananchi saa 12:30 asubuhi na kufika eneo la tukio.

Amesema baada ya kufika eneo hilo alimkuta mtuhumiwa akijaribu kukimbia bila mafanikio, “alikuwa na majeraha ya moto na aliishiwa nguvi kabisa. Alikwenda kwenye moja ya duka na kuomba maji, hapo ndipo alipokamatwa.”

“Nikiwa na wananchi tuliona nyaya zimefunguliwa wakati tukiangalia jinsi zilizofunguliwa ambazo zilikuwa zimefichwa kwenye shamba la mahindi alikuja mtu mmoja na kutuambia kuna kijana amemuona kwenye duka lililopo jirani akiwa amejifunika na shuka la kimasai na ana majeraha ya moto.”

"Tulimfuata na tulipomkuta alikiri yeye ndiye mhusika, tulimzuia na kutoa taarifa polisi na Tanesco na tayari wamefika kumchukua na kuona namna ya kushughulikia tatizo ili tuweze kurudishiwa umeme"

Akizungumza katika kituo cha polisi Mosha alikiri kuhusika na wizi huo na kusema ni tukio lake la tatu.

"Nilikuwa natafuta waya wa shaba ambao tunakwenda kuuza kama chuma chakavu, na nimefanya tukio hili likiwa la tatu na sikuwahi kukamatwa," amesema Riziki.

Via Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com