Kocha Msaidizi wa Taifa Stars, Suleman Matola akitoa maelekezo kwa wachezaji wakati wa mchezo huo
Na Damian Masyenene
Timu ya Taifa ya soka ya Tanzania, Taifa Stars leo imeanza vibaya michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (CHAN) inayofanyika nchini Cameroon, baada ya kupoteza mchezo wake wa kwanza kwa mabao 2-0 mbele ya majirani zao, Zambia (Chipolopolo).
Taifa Stars ambayo imeapangwa kundi D na Namibia, Guinea na Zambia, iliuanza mchezo vyema na kutawala kipindi cha kwanza na kuwalazimisha wapinzani wao kwenda mapumziko wakiwa hawajafungana.
Lakini mambo yalienda mrama katika kipindi cha pili baada ya kupoteza umiliki wa mchezo na kukubali kufungwa mabao hayo mawili, na kufanya iwe timu ya kwanza tangu michuano hiyo ya mwaka huu ianze kufungwa mabao mengi (2).
Zambia maarufu kama Chipolopolo walipata mabao yao kupitia kwa Collins Sikombe mnamo dakika ya 64 kwa mkwaju wa Penalti na Emmanuel Chabula katika dakika ya 81
Kufuatia mwanzo huo mbaya, sasa Tanzania italazimika kuchanga karata zake vyema katika michezo miwili iliyobaki dhidi ya Guinea na Namibia ili kuhakikisha kwamba wanafuzu kusonga mbele.
Chanzo - Shinyanga Press club blog
Social Plugin