................................................
Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imeanza maandalizi ya kuifanya maabara ya Kanda ya Ziwa kuwa maabara bora na maalumu kwa uchunguzi wa dawa za kuua viini vya bakteria (vipukusi), mpango unatarajiwa kukamilishwa ndani ya miaka mitatu.
Hayo yamebainishwa na Meneja wa TMDA Kanda ya Ziwa Sophia Mziray kwa waandishi wa Habari waliozuru katika maabara hiyo jijini Mwanza kuona shughuli za uchunguzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi zinavyoendeshwa.
"Maabara hii ipo kwenye taratibu za kufanywa kuwa maabara kubwa ya kisasa, bora na bobezi ya kupima vipukusi katika Afrika; na nchi za kusini mwa Afrika (SADC)," alisema Mziray.
Amesema kuwa Mamlaka ipo kwenye hatua mbalimbali za kuwaandaa wachunguzi waweze kuwa wabobezi lakini vile vile kuandaa mahitaji ya kuifanya maabara hii iwe bora kwa Afrika katika kuchunguza vipukusi.
Mziray amesema kwasasa maabara ya kanda ya ziwa ndiyo pekee kwa nchi wanachama wa jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) yenye uwezo wa kupima vipukusi na kutoa majibu yasiyo na shaka.
""Kwa kuwa ni maabara pekee katika kanda ya ziwa tunaendelea kuchunguza dawa kutoka kanda nyingine, kutoa elimu kwa umma, na kuhakikisha Watanzania wanapata bidhaa bora, salama na zenye ufanisi," alisema Mziray.
Ameongeza: "Tunaendelea kuwaelimisha wananchi kuwa wao pia ni sehemu ya wadhibiti wa dawa na vifaa tiba, hivyo wanapotumia na kubaini madhara watoe taarifa kwa haraka kwenye ofisi zetu nasi tuzifanyie kazi."
Amebainisha kuwa maabara ina mifumo ambayo imethibitishwa. Mamlaka inaandaa nyaraka, upembuzi yakinifu ujiridhisha kama rasilimali zinatosheleza ili kutimiza nia ya kuwa na maabara bora zaidi.
"Ili kuhakikisha ubora wa dawa vifaa tiba na vitendanishi unaendelea kuwepo, tuna tumia mfumo wa ufuatiliaji na udhibiti wa dawa sokoni (PMS) uchunguzi hulenga kubaini madhara ya Dawa kuanzia kwenye vifungashio," alisisitiza.
Mziray ameeleza kuwa Kanda ya Ziwa yenye mikoa Sita bado inakabiliwa na changamoto ya udhibiti wa bidhaa kwenye mipak ya Mutukula, Sirari, Kyerwa, na pia bandari ya Mwanza South na Uwanja wa ndege wa Mwanza kwakuwa dawa hizo huvushwa kwa njia zisizohalali.
"Kanda hii ni kubwa inajumuisha mikoa ya Mwanza, Shinyanga Kagera, Simiyu na Mara, watumishi wa TMDA pekee yake hawatoshi kufanikisha udhibiti hivyo Mamlaka inashirikiana na wakurugenzi wa halmashauri ambao huteua wakaguzi toka maeneo yao kisha tunawafundisha na kuwapa vitambulisho," ameeleza.
Meneja mawasiliano na elimu kwa umma wa TMDA Gaudensia Simwanza amesema ili maabara itoe majibu yasiyo na shaka lazima iwe imekidhi vigezo elekezi vya Shirika la Afya Duniani (WHO): hivyo maabara hii imekidhi na kuwa yenye kutoa majibu sahihi yanayokubalika ya uchunguzi wa sampuli za vipukusi.
"Maabara hii imepokea vipimo vya sampuli zilizochunguzwa Ujerumani na Afrika Kusini ambako baada ya kupima majibu yalionesha kutofautiana lakini baada ya sampuli hizo kupimwa toka Maabara ya TMDA yakawa suluhisho," alieleza.
Social Plugin