Mwanaume anayedaiwa kuiba fedha za mama lishe na kutokwa na utumbo sehemu ya haja kubwa
Na Salvatory Ntandu - Kahama
Kufuatia kusambaa kwa video katika mitandao ya kijamii ikimuonesha kijana mmoja ambaye hajafahamika jina wala makazi akiwa amechuchumaa huku utumbo ukiwa umetoka katika sehemu zake za haja kubwa, muda mfupi baada ya kutuhumiwa kuiba fedha za mamalishe aliyefahamika kwa jina la Catherin Peter mkazi wa Mtaa wa Kagongwa wilayani Kahama mkoani Shinyanga, tukio hilo limetajwa kuhusishwa na imani za Ushirikina.
Malunde 1 blog imefanikiwa kufika katika Ofisi ya Mwenyekiti wa Mtaa wa Kagongwa , Michel Shija na kuzungumza naye ili kufahamu undani wa tukio hilo ambalo limezua taharuki na gumzo katika mitandao ya kijamii kwa wakazi wengi wa wilayani hiyo na Watanzania kwa ujumla.
Shija amekiri kutokea kwa tukio hilo Jumapili Januari 17,2021 majira ya saa 4 asubuhi ambapo inadaiwa mwizi huyo ambaye mpaka sasa hajafahamika jina wala makazi alifika katika mgahawa wa Catherin na kuomba kupatiwa maji ya kunywa lakini baada ya kumaliza aliiba fedha zilizokuwepo kwenye mkoba ndipo aliulizwa akazitupa chini na kuanza kukimbia huku zingine akiwa nazo mkononi.
“Baada ya kutekeleza tukio hilo alikimbia ili asiweze kukamatwa kwani akinamama hao walianza kumpigia kelele za mwizi ndipo akaona njia salama ni kukimbia na baadhi ya fedha za Catherin ambazo alizikwapua kwenye mkoba ambao ulikuwa umetundikwa juu ya nguzo za mgahawa wake,”amesema Shija.
Amefafanua kuwa mwizi hiyo alikimbia umbali mrefu ,vijana waliokuwa karibu na eneo la tukio walianza kumkimbiza na ndipo akanguka chini na kuanza kuvua nguo zake huku utumbo ukiwa umening’inia kwenye sehemu za haja kubwa za mwili wake kitendo ambacho kiliwaogopesha watu wote walikuwa wanamkimbiza na kulazimika kumpeleka kituo cha polisi Kagongwa kwa taratibu za kisheria zaidi.
“Taarifa nilizozipata mpaka sasa ni kwamba mwizi huyo aliachiwa huru na Polisi wa kituo cha kagongwa na haijajulikana alikwenda wapi ila ninachokifahamu kuhusiana na tukio hilo ndiyo jinsi lilivyotokea na mimi sikushuhudia lakini nimepata taarifa hizi kutoka kwa mashuhuda wa tukio hili,”amesema Shija
Malunde 1 blog imemtafuta Bi. Catherin Peter ambaye anatuhumiwa kutekeleza tukio hilo ambalo linahusishwa na imani za kishirikina baada ya kuibiwa fedha zake na mteja wake ambaye baada ya wizi huo alikimbia kusikojulikana.
Bi Catherin amekiri kuibiwa fedha na mteja wake lakini kuhusiana na tukio hilo la mwizi huyo kupata madhara yeye hahusiki kwani anachokijua ni kuhusiana na kitendo cha fedha zake kupora na kisha mwizi huyo kukimbia kusikojulikana.
“Alikuja mgahawani kwangu kuomba maji ya kunywa alipomaliza aliiba fedha zangu za mauzo zilizokuwa kwenye mkoba ambazo zilikuwa shilingi elfu 90 lakini nilimwambia hivyo alizitupa chini haraka na kukimbia na shilingi elfu 27 tuu,akinamama wenzangu wakanishauri nipige kelele za mwizi lakini nilishindwa kutokana na tukio hilo kufanyika kwa haraka sana,”amesema Peter.
Ameongeza kuwa baada ya kuiba fedha hizo katika harakati za kukimbia wafanyakazi wake wa kike walimfuata nyuma na kwenda kuzirudisha fedha zote alizoziiba lakini kuhusiana na jinsi gani alivyopata madhara mwizi huyo yeye hahusiki na watu wenye nia mbaya wanataka kumharibia biashara.
“Tangu jana wateja wangu wamepungua wengi wanapaogopa wakinituhumu mimi ni mshirikina baada ya mwizi aliyeiba fedha zangu kudhurika,nina miaka 17 katika kazi yangu ya mamalishe hapa Kagongwa sijawahi kusikia ama kuona tukio kama hili,limeniathiri kubiashara kwani leo nimepata wateja wachache sana ikilinganishwa na hapo awali,”amesema Peter.
Amewataka watanzania kuzipuuzia taarifa hizo mitandaoni kuwa yeye ni mshirikina amemdhuru mwizi huyo jambo ambalo halina ukweli wowote kutokana na namna jinsi tukio lilivyotokea na kuwataka kuzipuuza kwani yeye hajihusishi na imani za kishirikina na kuwaomba wateja wake kuendelea kupata huduma katika mgahawa wake uliopo katika eneo la viwandani.
Bundala Magembe ni shuhuda wa tukio hilo ameiambia Malunde 1 blog kuwa aliona watu wakikimbiza mwizi huyo lakini alipokaribia eneo la tukio ndipo alipomwona mtuhumiwa akishindwa kukimbia kutokana na kutokwa na utumbo katika sehemu zake za haja kubwa.
Mwanaseni Ndullu mamalishe shuhuda wa tukio hilo amesema kuwa tukio hilo limezua taharuki kubwa kwa wakazi wa mtaa huo kwani haijawahi kutokea hata siku mmoja,mtu kupata madhara kama alivyopata mwizi huyo na kuwataka vijana kufanya kazi halali na kuachana na vitendo vya uhalifu mdogo mdogo.
Malunde 1 blog imefuatilia tukio hilo ili kujua hali ya Mwizi huyo na wapi anapatikana lakini haijafanikiwa kumpata.
Social Plugin