Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAWATAKA WACHIMBAJI WALIOVAMIA MGODI WA AL-HILAL KISHAPU WAONDOKE MARA MOJA


Wachimbaji wadogo wakimsikiliza Naibu Waziri, Prof. Shukrani Manya wakati akitoa maagizo ya serikali juu ya sakata la kuvamia eneo la mwekezaji

Na Suzy Luhende, Shinyanga 
WACHIMBAJI wadogo wa madini ya Almasi waliovamia na kuanza kuchimba katika kijiji cha Mwanh'olo kata ya Mwadui Lohumbo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga wamepewa siku mbili wawe wameshaondoka eneo hilo kwa hiari ili kumpisha mwekezaji mkubwa mwenye leseni aendelee kufanya shughuli zake katika eneo hilo.

Agizo hilo limetolewa leo Januari 21,2021 na Naibu Waziri wa Madini, Prof. Shukrani Manya, akiwa kwenye ziara yake ya siku moja mkoani Shinyanga, ambapo alizungumza na wanunuzi wa madini viongozi wa ChamaCcha wachimbaji (SHIREMA) pamoja na wachimbaji wadogo wanaochimba katika kijiji cha Mwanh"olo kata ya Mwadui Lohumbo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga. 

Manya amesema serikali ya awamu ya tano inawapenda wananchi wake na inataka waweze kupata maendeleo wao wenyewe na Taifa kwa ujumla, hivyo inawaomba wachimbaji hao waweze kuondoka katika eneo hilo kwa sababu ni eneo la mwekezaji Al-Hilal ambaye tayari ana leseni yake na kwamba wao watatafutiwa eneo jingine ili waweze kuendelea kuchimba.

"Nawaombeni sana muwe wasikivu na muweze kuelewa vizuri huu ujumbe wa serikali niliouleta kwenu, kwa sababu serikali inawapenda, hivyo inawapa siku mbili mkusanye mchanga wenu mliouandaa halafu mujiunge vikundi muwe na leseni yenu, serikali itawatafutia eneo zuri ambalo mtaendelea kuchimba bila bughuza yeyote, kinachotakiwa muwe waaminifu mnapopata mali muuzie katika soko letu na serikali iweze kuingiza kipato," amesema Manya.

"Msikubali kudanganywa na mtu awanunulie madini yenu tukikuta unauza kwa mtu tunakutaifisha hiyo mali yako na usafiri ulionao, hivyo tunatakiwa kuuzia kwenye mfumo ulioandaliwa na serikali, na serikali haihitaji faida kubwa inahitaji faida kidogo tu na na mtajulishwa sehemu mtakayopelekwa baada ya kutii kuondoka hapa," ameongeza.

Naibu Waziri Manya amesema eneo hilo siyo shamba la mtu kama wanavyojua bali ni mali ya serikali ambayo imeshakatiwa leseni na mwekezaji Hamad Hilal, hivyo wanatakiwa watoke kwa hiari kwani watatafutiwa eneo jingine la kuchimba ili mwenye leseni yake aendelee kufanya shughuli zake za uchimbaji.

Baadhi ya wachimbaji wadogo wanaochimba katika eneo hilo Zainab Said na Leonard Daudi wamesema wamekubali kuondoka pale ila wapewe muda wa wiki moja ili waweze kuosha mchanga wao na waweze kujiandaa kuondoka na mchanga wao kwa sababu muda waliopewa ni mdogo sana na waambiwe watapelekwa sehemu gani ili wakaendelee na kazi zao za uchimbaji. 

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack akitoa taarifa kwa naibu waziri Manya amesema anashukuru kwa kufika naibu waziri huyo, hivyo anaamini atasaidia kuondoa mgogoro wa wachimbaji wadogo na mwekezaji Al-Hilal, maana tayari nae alikuwa na mpango wa kuwapa siku chache wawe wameshaondoka eneo hilo

"Mimi na kamati yangu ya usalama wa madini tulishaenda katika kijiji hicho na tumejitahidi na tayari wachimbaji hao tulikuwa tumeshawatoa na sasa wameanza kurudi tena, lakini tunasikia wanaowafadhili ni hawa viongozi wao na baadhi ya wanunuzi tuliwataka wawaondoe watu wao katika eneo hilo," amesema Telack

Naye Afisa Madini wa mkoa wa Shinyanga Joseph Kumburu amesema tayari ofisi ya madini April 20, 2020 ilishawatoa wachimbaji 400 ambao walivamia eneo hilo lakini wakaja kurudi tena na sasa lina wachimbaji zaidi ya 1000 ivyo ofisi ya madini ilikuwa inajiandaa jinsi ya kuwaondoa na kuwakamata wachimbaji wanaovamia katika eneo la muwekezaji Al-Hilal, na kuwakamata wale wanaojimilikisha maeneo hayo.
Naibu Waziri wa Madini, Prof. Shukrani Manya akizungumza na wanunuzi wa madini na viongozi wa Chama cha Wachimbaji wadogo wa madini mkoa wa Shinyanga (SHIREMA) katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa mkoa huo, mapema wakati wa ziara yake mkoani Shinyanga
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack (katikati) akizungumza katika kikao hicho. Kulia ni Naibu Waziri wa Madini, Prof. Shukrani Manya
Naibu Waziri wa Madini, Prof. Shukrani Manya akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini ya Almasi katika Kijiji cha Mwanh'olo wilayani Kishapu ambao wanaodaiwa kuvamia eneo la mwekezaji, Mgodi wa Al-Hilal
Maeneo ya uchimbaji wa madini ya Almasi katika Kijiji cha Mwanh'olo wilayani Kishapu yanayodaiwa kuwa ya Mwekezaji Kampuni ya Al-Hilal ambayo yamevamiwa na wachimbaji wadogo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com