WAITARA ASHTUKIA MADUDU FEDHA ZA MIRADI YA UJENZI,KAMATI ZA MANUNUZI KUTOSHIRIKISHWA, ASEMA LAZIMA UCHUNGUZI UFANYIKE

Mbunge wa jimbo la Tarime Vijijini ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais,Muungano na Mazingira Mwita Waitara akizungumza na baadhi ya wananchi kijiji cha Nyangoto alipokuwa akikagua ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa shule ya Sekondari Nyamongo

Na Dinna Maningo, Tarime

Mbunge wa jimbo la Tarime Vijijini ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais,Muungano na Mazingira Mwita Waitara amemuomba Mdhibiti na Mkaguzi mkuu  wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi kwenye miradi ya ujenzi iliyojengwa kwa fedha za serikali kuu,fedha za mapato ya ndani ya halmashauri na fedha zinazotolewa na mgodi wa dhahabu wa Barrick(CSR).

Waitara alisema kuwa katika ziara yake ya ukaguzi wa miradi ya ujenzi ikiwemo ya ujenzi wa madarasa na nyumba za waalimu amebaini uwepo wa matumizi mabaya ya fedha katika ujenzi ambayo hayaendani na hali halisi ya soko kama inavyotakiwa katika miradi inayoelekezwa kwa mfumo wa Force Account.

Mbunge huyo alisema kuwa katika ukaguzi wa miradi hiyo amapeta malalamiko mengi kutoka kwa viongozi wa Serikali za vijiji zikiwemo kamati za manunuzi za vijiji kutoshirikishwa katika manunuzi licha ya miradi ya ujenzi kufanyika ndani ya vijiji.

Akiwa kwenye ukaguzi wa ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa shule ya Sekondari Nyamongo na ujenzi wa nyumba ya mwalimu shule ya Msingi Nyangoto alishangazwa kuona ujenzi ukigharimu fedha nyingi zikiwemo gharama kubwa za manunuzi ya vifaa vya ujenzi lakini pia vifaa kuzidi zaidi ya mahitaji.

Akisoma taarifa ya utekelezaji wa miradi ya jamii inayojengwa kwa fedha za Mgodi wa Dhahabu wa Barrick (CSR) katika vijiji vinavyozunguka mgodi, Mtendaji wa kijiji cha Nyangoto Chacha Turuya alisema kuwa miradi inayojengwa ni vyumba vitatu shule ya sekondari Nyamongo vitakavyogharimu sh.Milioni 88,761,465 na nyumba ya mtumishi pacha(2 in 1) sh.Milioni 88,734,528,jumla ya fedha zote ni sh.Mil.177,496,013.

Turuya alizitaja changamoto katika utekelezaji wa miradi hiyo kuwa ni pamoja na manunuzi kushindwa kufanyika kwa wakati,wataalamu wa ujenzi kushindwa kufanya ujenzi kwa wakati,mchakato wa malipo ya mafundi kuchukua muda mrefu,mafundi kutofika maeneo ya kazi kwa wakati kwa sababu mbalimbali.

"Gharama kubwa za malighafi za ujenzi hususani zinazotengenezwa viwandani kama vile mchanga na kokoto ikilinganishwa na bei halisi ya soko kama inavyotakiwa katika miradi inayotekelezwa kwa mfumo wa (force account)",alisema Turuya.

Baada ya Taarifa kusomwa Mwenyekiti wa kijiji cha Nyangoto Mwita Msegi na wajumbe wa kamati mbalimbali za kijiji wakatoa nyongo zao na kudai kutoshirikishwa katika hatua za manunuzi na kutolipwa posho zao za usimamizi wa ujenzi.

Msegi alisema kuwa serikali ya kijiji wala kamati ya manunuzi ya kijiji haikushirikishwa kwenye manunuzi ya vifaa vya ujenzi bali halmashauri ya wilaya ya Tarime kupitia idara ya manunuzi ndiyo inahusika katika mchakato mzima wa bei za vifaa na manunuzi.

" Bei zao ni kubwa mfano kokoto zinapatikana hapa Nyamongo kwa sh.120,000 kwa tripu moja wao wanaleta tripu moja ya kokoto kwa roli lenye ujazo wa 4.5 gharama yao ni 360,000,mchanga wa kutoka Nyasaricho ambao serikali ilituelekeza kuchukua huko tripu ni 180,000 wao wanauleta kutoka huko huko kwa ujazo huo kwa 360,000, wananchi wanajenga nyumba zao kwa kutoa mchanga mto Mara na ule unaokusanywa mvua zinaponyesha  tripu ni sh.100,000.

"Tukiwauliza wanasema wao ni wataalamu ndiyo wanaojua manunuzi wanafanya wao wenyewe bila kushirikisha kamati yetu ya manunuzi na mradi uko kwenye kijiji na mpaka sasa jengo liko kwenye hatua za uezekaji lakini hatujawahi kumuona mhandisi akifika kukagua tangu ujenzi uanze hatua ya msingi",alisema Msegi.

Mwenyekiti wa kamati ya mapokezi Tatu Kadama alisema kuwa elimu yao ni ya darasa la saba lakini anashangaa kuona halmashauri ikiwapatia makadirio ya bei za vifaa vya ujenzi (BOQ) zikiwa zimeandikwa kwa lugha ya Kiingereza jambo linalowachanganya .

"Mimi siulaumu mgodi maana halmashauri ndiyo inapitisha inapeleka mgodini nao wanalipa,halmashauri ndiyo inanunua vifaa kupitia wazabuni wake,kazi yangu ni kupokea tu vifaa kama sasa nimepokea mabati 147 ya kuezeka madarasa matatu lakini mabati kumi yamepungua,nimepokea mabati 100 ya nyumba ya mtumishi na kwanini waandike Kiingereza wengine elimu ni ndogo.

" Kinachonishangaza hivi vifaa tunavipokea kutoka kwa watu tofauti tofauti,utaona misumari analeta huyu,mabati analeta mwingine,nondo mwingine,mbao mwingine yaani ni changanyikeni hakuna utaratibu,mpaka sasa hatujalipwa posho yoyote, natumia gharama zangu za usafiri kwenda shuleni kupokea vifaa hadi wajumbe wengine wamekata tamaa kuja kusimamia",alisema Tatu.

Katibu wa kamati ya ujenzi Chacha Sultani alisema kuwa licha ya kuelezwa kulipwa milioni 3 ambazo zigegawanywa kwa awamu tatu kuwalipa wajumbe 10 kama posho za usimamizi wa ujenzi  ulioanza tangu Septemba 2020 lakini hawajawahi kulipwa kiasi chochote cha fedha na wanapofuatilia huambiwa kuwa wasimamie bure kwa kuwa ni jukumu lao kusimamia shughuli zinazofanywa ndani ya kijiji.

Waitara alimtaka kaimu afisa elimu Sekondari halmashauri wilaya ya Tarime Mukama Mazigo kutoa ufafanuzi kuhusu mambo yaliyoelezwa na wajumbe wa serikali ya kijini ambapo alisema kuwa ukaguzi unatakiwa kufanywa kila hatua ya ujenzi na kwamba tatizo ni idara kutokuwa na gari na halmashauri ina upungufu wa gari zisizotosheleza.

Mbunge Waitara alisema kuwa hata kama idara haina gari ilipaswa kutumia gari zingine za halmashauri kwani kutofanya ukaguzi wa ujenzi imesababisha majengo kujengwa chini ya viwango,lakini pia alisema kuwa haiwezekani madarasa matatu kujengwa zaidi ya milioni 88.

"Lazima ukaguzi ufanyike fedha zimetumika nyingi ikilinganishwa na mradi wenyewe tunaomba CAG aje kufanya ukaguzi wa fedha za Serikali kuu,fedha za mapato ya ndani ya halmashauri na ufanyike uchunguzi wa kina hasa kwenye hizi fedha za CSR kwanini nyumba inayojengwa kwa fedha za Serikali itumie milioni 50 lakini iliyojengwa kwa fedha za CSR itumie zaidi ya Mil. 88 na madarasa matatu yanayojengwa kwa Mil.60 lakini CSR yanajengwa kwa zaidi ya Mil.88 sikubaliani na haya matumizi mabaya ya fedha", alisema Waitara.

Mbunge huyo pia alikagua ujenzi wa Bwalo la chakula linalojengwa kwa fedha za serikali (EP4R) sh.Milioni 100 katika shule ya sekondari Manga kata ya Komaswa ambapo alibaini vifaa kununuliwa kwa gharama kubwa na kuwepo kwa maelekezo mahali pakununua vifaa.

Mkuu wa shule ya Sekondari Manga Editha Nakei alisema kuwa mradi huo unajengwa na mzabuni Abdul Juma Sakumi ambapo vifaa vya ujenzi vinanunuliwa kwenye duka la Jura ambaye ni mzabuni wa vifaa vya ujenzi na hadi sasa zimetumika milioni 47,747,000 na ujenzi unaendelea.

Mjumbe wa bodi ya ujenzi Gorge Sorongai alisema kuwa"tumeelekezwa kununua vifaa kwa Jura huko mjini kwanini tuelekezwe pakununua na mradi upo hapa!mbao moja ya seprasi tunauziwa sh 23,000 na wakati mbao za Seregena zinapatikana kwa sh.15,000" alisema Sorongai.

Mbunge Waitara alisema kuwa halmashauri imefanya makosa kutozishirikisha kamati za manunuzi na bodi"nilichokiona hapa hakuna ushirikishwaji Mkurugenzi anapiga tu simu kachukueni vifaa sehemu fulani bila kuishirikisha 
bodi kujua bei na vifaa haya malalamiko yapo kila mahali ninakopita, karibu shule nyingi vifaa vinanunuliwa kwenye duka moja na wakati kuna maduka mengi ya vifaa kwenye kata mbalimbali,tutaunda kamati za kuchunguza kila mahali ", alisema Waitara.

Waitara alikagua ujenzi wa mabweni ya wasichana katika shule ya Sekondari Nyanungu iliyopo kijiji cha Nyamombara kata ya Nyanungu inayojengwa kwa fedha za serikali kiasi cha sh.Milioni 80 ambapo wananchi walilalamika mbao ,mchanga,mawe,kokoto kununuliwa kwa gharama kubwa licha yakwamba vinapatikana kijijini kwa bei nafuu.

Damian Sungura mjumbe wa bodi ya shule alisema"wametumia fedha nyingi mbao ya 2/3,2/6 ni sh 5,000 zao zinakuja kwa sh 15,000 kwa mbao moja na cha hajabu wanafata mbao mjini na wakati zinapatikana hapahapa miti wanayokata mbao ni hapa hapa kwetu, kwanini bei zao ziwe juu!" ,alihoji kwa mshangao.

Mwenyekiti wa bodi ya shule Shadrack Marwa alisema kuwa utaratibu unaotumika ni wa kuumiza"nina mashaka na manunuzi yanayofanywa na halmashauri maana sisi kama bodi hatujashirikishwa wanahusika walimu kwanini bodi iwekwe kando sisi tunahusishwa kusimamia tu ujenzi"alisema.

Diwani wa kata ya Nyanungu Richard Tiboche alisema kuwa tripu moja ya mchanga inauzwa 150,000 ila kwenye manunuzi inaeleza umenunuliwa kwa sh.200,000, tripu moja ya kokoto kwa bei ya soko ni sh.100,000 wao wanasema wamenunua sh.220,000 na wanazinunua huku huku kwetu,wanatuambia mlunda mmoja ni sh.8,000 na wakati hapa kijijini ni sh.3,000 na ukiupasua unatoa vipande 3 vya mbao,piga kwa bei hiyo itakuwa ni 24,000 badala ya 9,000.

"Hizi mbao wanazotuletea kutoka mjini ni miti inayotoka kwenye vijiji vyetu kwanini wasingenunua miti hapa hapa kijijini wapasue mbao saizi wanazotaka mpaka waende mjini,na kuna maeneo mengine wamesema mbao zimetoka mjini kwa gharama kubwa lakini zimenunuliwa vijijini kwa gharama ndogo alafu wao wakaongeza bei"alisema Tiboche.

Mbunge huyo hali kadhalika alikagua ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa shule ya msingi Mangucha vinavyojengwa kwa sh.milioni 40 fedha kutoka TAMISEMI ambapo viongozi wa serikali ya kijiji na mtendaji wa kijiji walidai kutoshirikishwa .

Mtendaji wa kijiji cha Mangucha Petro  Mirumbe alisema kuwa vijiji alivyofanya kazi kulikuwa na ushirikishwaji mkubwa lakini tangu afike kwenye kijiji hicho hapewi ushirikiano kwenye miradi ya shule zaidi ya waalimu pekee kuhusika na wala hapewi mihutasari ya utekelezaji wa miradi kwa madai kuwa mradi ni wa shule na siyo mradi wa kijini.

Waitara alieleza kuwa ni lazima fedha zinapoingizwa kwenye akaunti za shule na vijiji wananchi washirikishwe kwa kuwa nao huchangia nguvu zao kwenye miradi na kuitaka halmashauri ya wilaya kufanya kazi kwa uwazi na siyo fedha za serikali kuwa shamba la bibi.

Mbunge huyo katika Ziara yake ya ukaguzi wa ujenzi wa madarasa na nyumba za walimu alikagua baadhi ya shule za sekondari ambazo ni Regicheli kata ya Regicheli,Kewamamba,Nkerege kata ya Kiore,Manga,Bukenye kata ya Komaswa,Nyanungu kata ya Nyanungu,Kangariani,Bungurere Kata ya Itiryo,Muriba,Nyamongo na shule ya msingi Mangucha,Iramba, Nyangoto na Nyabichune.
Mbunge wa jimbo la Tarime Vijijini ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais,Muungano na Mazingira Mwita Waitara akizungumza na baadhi ya wananchi kijiji cha Nyangoto alipokuwa akikagua ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa shule ya Sekondari Nyamongo
Mbunge wa jimbo la Tarime Vijijini ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais,Muungano na Mazingira Mwita Waitara akizungumza na baadhi ya wananchi kijiji cha Nyangoto alipokuwa akikagua ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa shule ya Sekondari Nyamongo
Mbunge wa jimbo la Tarime Vijijini ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais,Muungano na Mazingira Mwita Waitara akisaini kitabu cha mahudhurio wakati wa ukaguzi shule ya Sekondari Nyamongo
Mbunge wa jimbo la Tarime Vijijini ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais,Muungano na Mazingira Mwita Waitara akiwa kwenye ukaguzi wa nyumba ya mtumishi shule ya msingi Nyangoto
Mbunge wa jimbo la Tarime Vijijini ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais,Muungano na Mazingira Mwita Waitara akiwa kwenye ukaguzi wa vyumba vya madarasa shule ya Sekondari Nyamongo
Mbunge wa jimbo la Tarime Vijijini ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais,Muungano na Mazingira Mwita Waitara akiwa kwenye ukaguzi wa vyumba vya madarasa shule ya Sekondari Nyamongo
Mbunge wa jimbo la Tarime Vijijini ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais,Muungano na Mazingira Mwita Waitara akizungumza na baadhi ya wananchi kijiji cha Nyabichune wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa
Mafundi wakiwa katika ujenzi wa msingi shule ya Sekondari Nyabichune
Mbunge wa jimbo la Tarime Vijijini ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais,Muungano na Mazingira Mwita Waitara akizungumza jambo wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa shule mpya ya Sekondari Nyabichune

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post